KIKOSI cha Yanga kipo jijini Dar es Salaam kikiendelea na maandalizi ya michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini akili zote zikiwa juu ya mechi inayofuata ya raundi ya kwanza ya mshindi kati ya St George ya Ethiopia na Al Hilal ya Sudan.
Kwa kutambua kama itavuka raundi ya awali kwa kuing’oa Zalan ya Sudan Kusini, huenda ikakutana na Al Hilal ambayo ndio timu inayoihofia zaidi kutokana na uwekezaji iliofanya kusajili wachezaji wa maana wa bei mbaya na kocha mwenye zali na mataji ya Afrika, Florent Ibenge, mabosi Jangwani wameamua kucheza akili za Waarabu hao wa Sudan.
Inachofanya Yanga ni kupata mtu mmoja bora wa ufundi atakayeisoma Al Hilal ambayo Jumatano itacheza na Simba kwenye michuano maalumu, ili kurahishiwa kazi baada ya awali kuisoma ilipoitungua Asante Kotoko mabao 5-0 kwenye mechi hizo maalumu na pia kuisoma St George ilipokuja nchini kucheza na Simba katika tamasha la Simba Day.
Yanga itakayoanza na Zalan iliyoomba michezo yote ipigwe Dar es Salaam, kitu ambacho mabingwa hao wa Tanzania wameona mechi za raundi ya kwanza kwao sio ngumu kiviiile kama mtihani watakaokutana nao raundi ijayo dhidi ya St George na Al Hilal.
Katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa freshi, mabosi wa Yanga wamempa ajira ya muda kocha ambaye anafanya kazi ya kuwasoma Al Hilal ambao wameunda timu upya kwa mabilioni kujua mbinu zao chini ya kocha Ibenge.
Kama haitoshi Yanga wameshapewa mkanda mzima wa mechi ya Al Hilal dhidi ya Asante Kotoko ambao Wasudani hao walishinda kwa mabao 5-0.
Mechi hiyo pia kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ameiangalia kwa utulivu kisha akasema kwa kifupi kwamba: “Jamaa wana timu nzuri (Al Hilal) ni timu ngumu sana lakini tutapambana nao.”
Kama haitoshi mabosi wa Yanga wanapanga baada ya mechi ya kwanza dhidi ya Zalan watamsafirisha haraka kocha wao yeyote kwenda Ethiopia kuwasoma kwa pamoja St George dhidi ya Al Hilal.
Yanga inataka kujua ubora wa Al Hilal inavyocheza ugenini kabla ya kukutana nao ambapo mshindi wa mechi hiyo ataanzia Dar es Salaam kabla ya marudiano.
Mabingwa hao wa Tanzania wanaijua St George, lakini presha ni Al Hilal ambao wanaonekana kuwa na mabadiliko makubwa msimu huu chini ya tajiri wa biashara ya mafuta, Hisham al Sobat. Yanga haitaweza kuuangalia mchezo wa Al Hilal nyumbani kutokana na sheria ngumu za taifa hilo katika kufanya uchunguzi hatua ambayo inawalazimu kuhakikisha wanawasoma Al Hilal wakiwa nchini Ethiopia.