Home Habari za michezo JICHO LA MGALILAYA : HILI LA TUISILA KISINDA LINA HARUFU YA RUSHWA….NINI...

JICHO LA MGALILAYA : HILI LA TUISILA KISINDA LINA HARUFU YA RUSHWA….NINI KIMEWALAINISHA TFF ..?

Bodi ya ligi ndio waliosema Tuisila usajili umekataliwa Kwa kuwa Yanga walishatimiza wachezaji 12 na tayari wamepewa leseni. Na hao hao ndio Leo wamemruhusu kucheza. Tuliambiwa Yanga walikataliwa Kwa sababu walisema wamegundua Kambole ana majeraha ya muda mrefu hivyo hawezi kutumika msimu huu. Hivyo wakaamua kubadili jina Kwa sababu hizo. 


Leo inatoka kauli Kambole ameuzwa kwenye timu inayotoka Uganda. Hiyo timu ya Uganda ndio inanunua wachezaji wenye majeraha ya muda mrefu? Iwapo Kambole alipewa leseni ya kucheza ligi ya Tanzania 2022 na mpaka ligi Inaanza jina lake linasomeka ni mchezaji wa Yanga. Basi atahesabika ni mchezaji wa Yanga. 

Na iwapo Yanga watamtumia Kisinda basi itahesabika Yanga imewatumia wachezaji 13 wa kigeni kwenye ligi msimu huu. Haijalishi amecheza mechi au hajacheza ilimradi ana leseni ya Tff ya kuitumikia Yanga msimu wa 2022 mpaka ligi imeanza kuchezwa basi huyo ni mchezaji wa Yanga Kwa mujibu wa kanuni na Sheria zote.

Hivyo kama Yanga watamtumia Kisinda kwenye ligi hiyo hiyo kabla ya dirisha lingine kufunguliwa basi Tff mjiandae Kwa lolote na mje na majibu Kwa nini kanuni ivunjwe na timu itumie wachezaji 13 wa kigeni Kwa kipindi kimoja Cha usajili. Hili likisimamiwa haki inashinda mchana kweupeeee.

Nini kilisababisha kipindi dirisha halijafungwa awe sio halali na dirisha likishafungwa awe halali? Au mlikuwa mnatengeneza mazingira ya rushwa? Mmepewa nini hadi mkalegea na kutekeleza matakwa ya mabwana zenu? Kama Kisinda alikuwa halali angekuwa halali dirisha likiwa halijafungwa. Dirisha lilishafungwa na usajili unamalizika. Yaani mshindwe kumruhusu dirisha likiwa wazi mseme wazi kanuni haziruhusu na mje mumruhusu dirisha likiwa limeshafungwa na mbombela kibao.

Hili Wala huitaji kwenda chuo kikuu uwe na digrii ndio ung’amue hapa Kuna harufu ya rushwa. Unatakiwa tu uwe na kichwa kizuri kinafikiri tu umakini utagundua tu hapa ipo namna.

Tunaposema Tff hawataki kuruhusu chombo huru cha kuendesha Kwa sababu hapa ndio mahali wanatengeneza mazingira ya rushwa ni mambo kama haya. Nini kimewalainisha mpaka mkageuka jiwe la chumvi? Au ndio hakuna mkate mgumu mbele ya chai? Kama nyie wenyewe mnayumba na kanuni zenu wenyewe na kusababisha sintofahamu nani atawaamini? 

Kwa nini hamkulipitisha jina toka awali dirisha likiwa wazi? Mngelipitisha haya masongombingo yangetoka wapi? Mnatengeneza mazingira wenyewe ya kuhisiwa kuchukua rushwa. Na Kwa nini kwenye mazingira haya nisiwahusishe na mlungula? 

KWENYE HILI KILICHOFANYIKA TAFSIRI YAKE NI HAKUNA MKATE MGUMU MBELE YA CHAI.
  ( Jicho la tatu la Mgalilaya).

Makala haya yamendaikwa na Mdau wa Soka la Bongo anayefahamika kwa jina la Mgalilaya.
SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMAMOSI