Home Habari za michezo KISA ‘MISHUTI YAKE YA MWANA UKOME’ FEI TOTO AIBUKA NA HILI YANGA….AFICHUA...

KISA ‘MISHUTI YAKE YA MWANA UKOME’ FEI TOTO AIBUKA NA HILI YANGA….AFICHUA SIRI YA KUWATESA MAKIPA…


KIUNGO fundi wa mpira anayekipiga Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ juzi usiku alifunga mabao mawili kwa mashutu makali akitokea benchi na kuinusuru timu hiyo isilale mbele ya Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, kisha akasema kama kuna watu wanadhani huwa anabahatisha kufunga mabao ya aina hiyo, basi pole yao.

Fei alisema kufunga kwake mabao kwa mashuti huwa habahatishi kwani anayafanyia kazi muda mrefu kwenye mazoezi ya timu hiyo na kwamba ataendelea kufunga sana hasa anapokutana na timu inayojisahau dhidi yake.

Feisal aliyeingia kipindi cha pili kwenye mechi hiyo akichukua nafasi ya Denis Nkane, amesema kuwa mwendelezo wake wa kuwatungua makipa kwa mashuti ya mbali ni matokeo ya mazoezi makali anayofanya mazoezini kila siku chini ya uangalizi wa makocha.

Kiungo huyo anayeichezea pia Taifa Stars alisema akiwa katika uwanja wa mazoezi kabla ya kuanza, wakati yanaendelea au kumalizika huwa anatenga muda wa kupiga mashuti si chini ya mipira kumi ambapo kuna ambayo anapatia na mengine anakosea.

Alisema kutokana na aina hiyo ya mazoezi imekuwa kama utamaduni kwake hata katika mechi akipata mpira nje ya boksi huwa anajaribu kupiga shuti na bahati nzuri kwake kuna yale ambayo yanakuwa mabao.

“Siri kubwa ni kuendelea kulifanyia kazi hilo la kupiga mashuti katika uwanja wa mazoezi ndio maana hata kwenye mechi ikitokea huwa nafanya vizuri kutokana ni utamaduni wangu na si kama nabahatisha,” alisema Fei Toto na kuongeza:

“Hata kocha kwenye mazoezi amenieleza kama nikiendelea kulifanyia kazi hilo na kulitumia katika mechi naweza kufunga mabao aina hii yasiyopungua nane ndani ya msimu mmoja.

“Unajua mabeki wa timu pinzani ikitokea kwangu nimepata nafasi ya kupiga shuti huwa hawaamini kama naweza kufanya hivyo akili zao zinakuwa kwenye mawazo ya mimi kutoa pasi kwahiyo nafanya tukio hilo la kushtukiza na kuipatia timu yangu faida kwa kufunga bao kutokana na shuti la mbali.”

Nyota huyo pia alieleza kuusoma mchezo dhidi ya Azam akiwa benchi na alivyoingia alikuwa anatimiza kile alichokiona akiwa kwenye benchi hivyo ilikuwa kazi nyepesi kwake kuwaangamiza Waoka mikate wa Chamazi.

SOMA NA HII  WAZAZI WALIOMPA MTOTO WAO MCHANGA JINA LA MAYELE WAFUNGUKA..."SIWEZI KUMBADILISHA JINA HATA IWEJE"...

“Nikiwa benchi kabla ya kupata nafasi ya kuingia nilishuhudia mchezo wa ushindani hasa eneo la kiungo wapinzani wetu walikuwa bora sana wana kasi na nguvu,” alisema na kuongeza:

“Matokeo yaliyopatikana ni juhudi za wachezaji wote tulicheza kwa kushirikiana nilitumia nafasi mbili za kupiga mashuti yaliyolenga lango na mengine yalitoka nje nafurahi kuwa mmoja wa wachezaji walioipa timu matokeo.”

Fei amekuwa na muendelezo wa kufunga mabao ya mashuti ya mbali akizifunga Simba kwenye mechi ya ngano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mara mbili kila walipokutana kwenye hatua hiyo pia amezifunga KMC, Polisi Tanzania kwenye mechi za Ligi Kuu Bara katika misimu iliyopita.