KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inatarajiwa kukutana Ijumaa kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na suala la Tusisila Kisinda winga ambaye amesajiliwa Yanga.
Ikumbukwe kwamba Kisinda amesajili Yanga akitokea Klabu ya RS Berkane lakini usajili wake umekwama kukamilika kutokana na usajili wake kuchelewa kwa mujibu wa kanuni ya 62, (1) ya ligi kuu toleo la 2022.
Inaelezwa kuwa kamati hiyo huwa inakutana kwa ajili ya kuweza kujadili masuala mbalimbali ambayo yanakuwa yanawasilishwa mezani.
Ni Said Soud yeye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambayo aliwahi kusema kuwa huwa wanakutana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mpira.
Pia nyota mwingine ambaye anatajwa kujadiliwa ni pamoja na Joash Onyango ambaye anatajwa kwamba amepeleka ombi la kuvunjiwa mkataba na mabosi wake wa Simba..
Ahmed Ally, Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa Onyango ni mchezaji wao na amesaini mkataba wa miaka miwili hivyo bado yupo ndani ya kikosi hicho.