Home Geita Gold FC SIO SIMBA NA YANGA TU ZENYE NEEMA….GEITA GOLD NAO WAPATA ‘BINGO’ ...

SIO SIMBA NA YANGA TU ZENYE NEEMA….GEITA GOLD NAO WAPATA ‘BINGO’ …GF TRUCKS WAIMWAGIA MAMILIONI YA UDHAMINI…

 


WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, Geita FC imepata udhamini wa mwaka mmoja kutoka kampuni ya GF Trucks & Equipment.

Udhamini huo utaisaidia Geita FC kufikia malengo yake kwenye michuano hiyo na ligi kuu Tanzania Bara.

Akizungumza wakati wa kutangaza udhamini huo, Meneja Biashara Mkuu wa GF Trucks, Salman Karmali, alisema kampuni hiyo umeamua kuidhamini Geita kutokana na jitihada za klabu hiyo katika kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

Alisema wanaamini udhamini huo utaisaidia timu hiyo kuweza kufanya vizuri kwenye mashindano watakayoshiriki ndani na nje ya nchi.

“Udhamini wetu unajumuisha pesa ambazo tutatoa kwa klabu lakini kutokana na makubaliano ya pande zote mbili hatuwezi kuainisha kiasi cha pesa, lakini ni udhamini wenye faida kwampande zote mbili,” alisema Karmali.

Aidha, alisema mbali na pesa, pia yapo mambo nje ya mkataba ambayo kampuni ya GF inaweza kuyafanya kwa klabu hiyo.

“Mafanikio waliyoyapata Geita msimu uliopita imetufanya kuidhamini timu hii, tunaamini udhamini huu utawasaidia sana Geita kufanya vizuri,” alisema Karmali.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Geita FC, Simon Shija, alisema kutokana na majukumu waliyonayo msimu huu ujio wa GF Truck utawasaidia kuweza kufikia malengo yao.

“Udhamini huu unatupa uhakika Geita Gold FC wa kutatua changamoto zetu, tuna uhakika wa kusafiri kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine kwenye ligi msimu huu, ushirikiano na wadhamini wengine tulionao kama Anglo Gold Ashanti pia unatupa uhakika wa kusafiri nje ya nchi kwenye michuano ya CAF,” alisema Shija.

Msimu huu wababe hao kutoka mkoani Geita wataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa pamoja Azam FC.

Geita Gold FC imepata nafasi hiyo baada ya kushuka nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

SOMA NA HII  JEAN BALEKE AJIVISHA MABOMU ATOA KAULI NZITO KWA MASHABIKI WA SIMBA