Home Uncategorized KOCHA SIMBA: YANGA WAMESAJILI MAJEMBE

KOCHA SIMBA: YANGA WAMESAJILI MAJEMBE


MAMBO ni moto ndani ya Yanga. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya usajili wa timu hiyo ilioufanya mpaka sasa kupongezwa na baadhi ya makocha wa kutoka nje ya nchi ambao wamewahi kufundisha soka hapa nchini. Mpaka sasa Yanga imewasajili wachezaji tisa wapya ambapo sita kati ya hao ni wa kutoka nje ya nchi.

Wachezaji wa nje ya nchini ni Erick Rutanga kutoka Burundi, Patrick Sibomana (Rwanda), Lamine Moro (Ghana), Issa Bigirimana (Rwanda), Maybin Kalengo (Zambia) pamoja na Farouk Shikalo (Kenya). Wazawa ni Abdulaziz Makame (Zanzibar), Ally Sonso (Lipuli FC) na kipa wa Mbao FC, Metacha Mnata.

Kutokana na usajili huyo, aliyewahi kuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma ameliambia Championi Jumatatu kuwa wachezaji ambao Yanga imewasajili kutokea Ligi Kuu ya Rwanda ambako yeye anafundisha soka kwa sasa, wana uwezo wa juu na amepongeza kwa usajili huo.

Wachezaji hao ni Rutanga ambaye alikuwa akiitumikia Rayon Sports, Sibomana (Mukura Victory) pamoja na Bigirimana (APR).

“Nimesikia kuwa Yanga imewasajili wachezaji hao, hakika ni usajili mzuri ilioufanya kwani wote ni wazuri na watakuwa na msaada mkubwa kwa timu hiyo.

“Wanajitambua lakini pia ni watu ambao bado wanatafuta mafanikio, kwa jinsi ninavyowafahamu niwaambie tu Yanga kuwa wamepata wachezaji wazuri kama kweli wamewasajili,” alisema Djuma.

Kwa upande wake aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina ameipongeza Yanga kwa usajili wa Moro ambaye ni beki wa kati pamoja na mshambuliaji, Kalengo ambao wao wanatokea katika Ligi Kuu ya Zambia.

Lwandamina amesema: “Ninawajua vizuri, hivyo naamini watakuwa na mchango mkubwa kwa Yanga kutokana na uwezo wao.

“Beki Lamine Moro ni mzuri kutokana na kuwa na kila kitu anachotakiwa kuwanacho beki, anajua kukaba, anajua kupambana lakini pia ana nguvu na uwezo mkubwa wa kucheza kwa kichwa mipira ya juu.

“Kwa upande wake, Kalengo yeye nimemfundisha katika timu ya Zesco, anajua kufunga kwa kutumia miguu lakini pia kichwa, vilevile anajua kumiliki mpira na ana kasi kubwa,” alisema Lwandamina.

SOMA NA HII  KAZE MAMBO MENGINE YANUKIA IHEFU