Home Habari za michezo KUELEKEA KARIAKOO DABI….PUMZI YA SIMBA IKO HAPA….YANGA MTAPIGWA KAMA NGOMA…

KUELEKEA KARIAKOO DABI….PUMZI YA SIMBA IKO HAPA….YANGA MTAPIGWA KAMA NGOMA…

Simba kwa sasa roho kwatu baada ya chama lao kuimarika ikiwa chini ya kocha Juma Mgunda, huku Moses Phiri akizidi kung’ara na kuwafanya viongozi kutamba kwamba ameiva kwenye michuano ya ndani na kimataifa, kwamba apewe pasi tu uwanjani amalize mambo mapema.

Phiri hadi sasa amefunga mabao tisa katika mechi tisa, yakiwamo matano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mengine manne ya Ligi Kuu Bara na wikiendi hii anaenda kuikabili Yanga kwa mara ya kwanza kwenye Kariakoo Derby na mashabiki wanataka jamaa apewe pasi tu atupie.

Viongozi hao wana kumbukumbu ya mechi ya mwisho ya timu yao dhidi ya Yanga, haiwapi furaha, lakini makali ya nyota wao wanne akiwamo Phiri imewapa mzuka mwingi kabla ya kuvaana na watani.

Kwa kuanzia, Simba imepata jeuri ya uwepo wa utatu hatari na tishio kwa mabeki hivi sasa unaoundwa na viungo Clatous Chama na Augustine Okrah pamoja na Phiri lakini kama ufahamu, kuna silaha nyingine ya siri ambayo imekuwa ikitumika kusaka mabao, yaani beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Tathmini iliyofanya na Mwanaspoti imebaini kumekuwa na ushiriki mkubwa wa nyota hao wanne hao katika kutengeneza mabao ya Simba msimu huu na hapana shaka wakiendelea na moto wao, lango la Yanga linaweza kuwa matatizoni Jumapili.

Kati ya mabao 11 ambayo Simba imefunga katika mechi tano za Ligi Kuu ilizocheza hadi sasa, wanne hao wamehusika na mabao tisa kwa kufunga ama kupiga pasi ya mwisho, sawa na 81.8% huku wachezaji wengine wakihusika na mabao mawili tu sawa na 18.2%.

Katika mabao hayo tisa ambayo wanne hayo wamehusika nayo, Phiri ndio amekuwa hatari zaidi kwani amehusika na mabao manne ambayo yote amefunga yeye, Chama akifuatia kwa kufunga bao moja, kupiga pasi za mwisho mbili na kusababisha mabao manne.

Mabao hayo matatu ambayo Chama amesababisha, moja ni katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ambapo beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alijifunga wakati alipokuwa akizuia krosi yake, lingine ni faulo aliyochezewa dhidi ya Geita Gold iliyozaa bao la Augustine Okrah, pia alifanyiwa faulo iliyozaa bao moja katika mchezo walioshinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na ndiye alipiga faulo iliyochangia kupatikana kwa bao la pili la Simba katika sare ya mabao 2-2 na KMC.

Pamoja na Okrah na Tshabalala kila mmoja kuhusika na bao moja, mmoja akifunga na mwingine kupiga pasi ya mwisho, wawili hao wamekuwa wakihusika katika uanzishaji au muendelezo wa mashambulizi yanayozaa mabao.

Okrah mbali na bao lake moja alilofunga, ndiye alifanyiwa faulo iliyozaa bao pekee la ushindi la Simba dhidi ya Prisons, wakati Tshabalala, alitoa asisti moja katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji na ndiye alipiga pasi kwa Chama ambayo ilipelekea afanyiwe faulo iliyozaa bao moja la Simba dhidi ya Geita Gold.

Ikumbukwe ukiondoa Tshabalala ambaye alicheza mechi dhidi ya Yanga kwenye Ngao ya Jamii ambayo walipoteza kwa mabao 2-1, Chama na Okrah hawakucheza kwa muda mwingi kwenye mechi hiyo huku Phiri ambaye ndiye tegemeo la Simba kwa sasa, akikosekana hata kwenye benchi la wachezaji wa akiba.

Chama aliyekuwa katika kiwango bora katika mechi hiyo dhidi ya Yanga ya Ngao ya Jamii, alicheza kwa dakika 59 kabla ya kutolewa na kuingizwa Okrah aliyecheza kwa dakika 31 tu.

Simba imeonekana kuwa moto wa kuotea mbali katika kufumania nyavu msimu huu ambapo hadi sasa imekuwa na wastani wa kupachika mabao mawili kwa mchezo, huku kazi kubwa ikionekana kufanywa na Chama, Okrah na Phiri katika upatikanaji wa mabao hayo. Katika mechi 10 za kimashindano ambazo Simba imecheza msimu huu, imefunga jumla ya mabao 20, ambapo 11 imepachika kwenye Ligi Kuu, nane kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na moja kwenye Ngao ya Jamii.

Akizungumzia makali ya nyota wake hao, kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema; “Wanafanya vizuri kwa sababu wanacheza kwa ajili ya timu. Lakini sio wao tu, kiujumla timu nzima inapambana kuhakikisha tunafanya vizuri na huo ndio wajibu wao kama wachezaji. Naamini kuna mengi mazuri yanakuja.”

SOMA NA HII  KAZI NI KUBWA KWA SIMBA MBELE YA AS VITA MAMBO YAMEBADILIKA