Home Habari za michezo BOSI WA SOKA UGANDA ATIA NGUMU MICHO KUTUA JANGWANI…MWENYEWE ADAI YANGA NI...

BOSI WA SOKA UGANDA ATIA NGUMU MICHO KUTUA JANGWANI…MWENYEWE ADAI YANGA NI FAMILIA YAKE..

WAKATI Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Uganda, Milutin Sredojevic ‘Micho’, akihusishwa na kuja kurithi mikoba ya Mtunisia Nasreddine Nabi katika kikosi cha Yanga, Mserbia huyo ameanika kila kitu kuhusu tetesi hizo zilizosambaa kwa kasi baada ya kuonekana Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi akiwa viongozi wa klabu hiyo juzi.

Micho alikuwa miongoni mwa wageni kutoka nje waliohudhuria ‘Dabi’ ya Simba na Yanga katika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, shukran zikiwaendea, Agustine Okrah aliyewatanguliza Wekundu wa Msimbazi dakika ya 15 na Stephane Aziz Ki aliyeisawazishia timu yake sekunde chache kabla ya kuelekea mapumziko.

Tetesi za Micho kuandaliwa kuja kuchukua mikoba ya Nabi, inachagizwa na madai ya kukosekana maelewano katika benchi la ufundi la Yanga, ikidaiwa kuwa haelewani na msaidizi wake, Cedric Kaze, lakini kubwa likiwa ni kushindwa kuipa timu hiyo mafanikio kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutofikia malengo ya kufuzu hatua ya makundi kwa kutolewa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.

Hata hivyo, Micho ambaye amewahi kuinoa Yanga mwaka 2007 na kuipa taji la Ligi Kuu Bara wakati timu hiyo ikiwa chini ya Mwenyekiti, Imani Madega, amekanusha taarifa hizo za kuwa njiani kurejea kuinoa.

Kocha huyo ambaye ana rekodi ya kushiriki ‘dabi’ nne kubwa ikiwamo Kariakoo Dabi (Yanga na Simba), Omdurman Dabi (Al Hilal dhidi ya El Merrick), pamoja na Cairo Dabi, (Zamalek na Al Ahly), bado ana mkataba na Timu ya Taifa ya Uganda.

Akizungumza jana, Micho alisema kilichomleta nchini ni kuangalia mchezo wa dabi ya timu hizo kongwe mbili, Simba na Yanga ambao ulipigwa juzi.

Alisema hakuja nchini kwa sababu ya taarifa za kufanya mazungumzo na Yanga, kwani lengo lake lilikuwa ni kushuhudia mchezo huo pamoja na mchezaji wa timu yake ya taifa, Khalid Aucho.

“Licha ya kuja kuangalia moja ya kati ya dabi bora kwa sasa Afrika Mashariki na Kati, pia Yanga ni familia yangu, nilikuja kumwangalia mmoja wa viungo wangu, Khalid Aucho.

“Mchezo ulikuwa mzuri ila Aziz Ki kwangu alikuwa mchezaji bora licha ya bao alilofunga la ‘free kick’ (mpira uliokufa), nimemfuatilia tangu dakika ya kwanza mpaka mwisho,” alisema Micho.

Alisema anawapongeza sana makocha wazawa wanaokinoa kikosi cha Simba, Juma Mgunda na Selemani Matola kwa timu yake kucheza mpira mzuri na kutawala mchezo licha ya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Katika mechi hiyo, Simba ilimiliki mpira zaidi vipindi vyote viwili na kama safu ya ushambuliaji ingekuwa makini, ingeweza kumaliza kipindi cha kwanza ikiwa mbele kwa mabao matatu.

Gazeti la Nipashe pia lilibisha hodi kwa Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa), kutaka kujua endapo Micho amemaliza mkataba wa kuinoa timu hiyo ama la, ambapo lilizungumza na Ofisa Habari wa Fifa, Ahmed Hussein Marsha na kueleza si rahisi kocha huyo kuondoka.

Marsha alisema “‘He can’t join'” (hawezi kujiunga Yanga) na kwamba, kwa kuwa bado ana mkataba wa kuinoa timu hiyo ya taifa.

SOMA NA HII  WAKATI SIMBA WAKIENDELEA KUJIVUTA VUTA...YANGA WAFANYA KWELI KWA MANZOKI...KUKIWASHA SIKU YA WANANCHI...