Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA KARIAKOO DABI…OKRAH NA PHIRI WAAPA ‘KUIHEMEA’ YANGA…

KUELEKEA MECHI YA KARIAKOO DABI…OKRAH NA PHIRI WAAPA ‘KUIHEMEA’ YANGA…

Achana na ushindi walioupata Simba dhidi ya Primeiro de Agosto na kuwavusha hatua ya makundi, unaambiwa kikosi hicho kwa sasa akili zao wamezielekeza mechi dhidi ya Yanga itakayopigwa Jumapili hii katika Uwanja wa Mkapa.

Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu kutokana na upinzani ulipo baina ya miamba hii kwa sababu ya historia zao, huku kila mmoja akitaka kushinda ili kuwafurahisha mashabiki na kulinda heshima yake isishuke kirahisi.

Nyota wa kikosi hicho, Augustine Okrah alisema sio mechi rahisi kutokana na upinzani uliopo ingawa matokeo yao yaliyopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika yamewapa nguvu hivyo wana imani kubwa ya kuibuka na ushindi.

“Kwetu wachezaji tumejipanga kama tulivyofanya kwenye mchezo uliopita, tunategemea mechi ngumu kwa sababu ya upinzani uliopo ila sisi binafsi malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda,” alisema na kuongeza;

“Hatuwezi kubweteka kwa kile tulichokifanya na de Agosto, isipokuwa imetuongezea hamasa zaidi ya kuona kila kitu kinawezekana kwani yote haya yanachangiwa na umoja uliopo kwetu wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wetu.”

Kwa upande wa straika wa timu hiyo, Moses Phiri alisema hakupata nafasi ya kucheza mechi ya kwanza msimu huu dhidi ya Yanga kutokana na kocha wa wakati huo, Zoran Maki kutompa nafasi lakini sasa nguvu na akili wanaelekeza kwenye mechi hiyo ya dabi.

Alisema kama atapata nafasi ya kucheza kwenye mechi hiyo malengo yake ni yale yale ya kuhitaji kufanya vizuri na kuisaidia timu kama si kufunga basi kuwa msaada kwa mchezaji mwingine kufunga.

“Mechi hiyo ni kubwa hapa nchini, itakuwa ngumu ila tunahitaji kupambana zaidi ili kuendeleza muendelezo wetu mzuri katika ligi na kuendelea kuwa kileleni mwa msimamo kwa pointi si mabao kama ilivyo wakati huu,” alisema Phiri na kuongeza;

“Kwenye ligi nimefunga mabao manne naamini huku ninayo nafasi ya kuongeza idadi ya mabao kutokana na wakati huu napata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwa hiyo sitaki kuliangusha benchi la ufundi linaloniamini.”

“Nafahamu ukubwa wa hii mechi kabla ya kuja hapa Tanzania kujiunga na Simba, naamini ni miongoni mwa mchezo unaweza kuonyesha ukubwa na ubora wa mchezaji kama anaweza akafanya vizuri.”

Timu hizo zinaingia uwanjani zikiwa na pointi 13 kila moja lakini Simba ipo kileleni kutokana na wingi wa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Yanga ambayo inashika nafasi ya pili, kila moja amecheza mechi tano.

SOMA NA HII  MAAJABU YA MORRISON YALIVYOMPOFUSHA FEI TOTO....AKASAHAU YA SADIO MANE NA LIVER...