Home Habari za michezo TUSIPOTEZE MUDA…HAWA QATAR NI KAMA TAIFA STARS TU…TOFAUTI YAO NA SISI NI...

TUSIPOTEZE MUDA…HAWA QATAR NI KAMA TAIFA STARS TU…TOFAUTI YAO NA SISI NI UTAJIRI TU..

Juzi usiku pale Doha ilinichukua dakika tano tu za pambano kati ya wenyeji wa Kombe la Dunia Qatar dhidi ya Ecuador kuamini kwamba wenyeji wetu Qatar walikuwa ‘Taifa Stars’ iliyo tajiri. Haikuhitaji kuchukua muda mrefu.

Walitawaliwa ndani ya dakika chache wakageuka kuwa kichekesho. Wakafungwa bao moja la haraka haraka ambalo wengi hawakuelewa vema kwanini lilikataliwa hadi teknolojia ilipofanya kazi ngumu ya kutuelewesha kwamba mfungaji alikuwa ameotea.

Walipokuwa na mpira walipoteza kwa haraka. Mpira haukuweza kukaa mguuni kwa haraka. Lakini pia wapinzani waliweza kuwasoma wao kwa haraka. Walijua huyu alikuwa anataka kupiga pasi wapi na wangeingilia kati na kuuchukua mpira.

Hawakuwa na stamina wala nguvu, achilia mbali kasi. Ilionekana kuwa mechi ya wanaume dhidi ya wavulana. Walifungwa mabao rahisi na mara zote haikujulikana uhodari wao ulikuwa wapi. Haikujulikana kama walikuwa hodari katika kujihami, kushambulia au kumiliki mpira. Mpaka tunakwenda mapumzikoni walikuwa hawajagusa mpira katika eneo la kumi na nane la Ecuador.

Kifupi ni kwamba hawapo katika kiwango cha kucheza katika Kombe la Dunia. Kilichosababisha wacheze ni kwa sababu wao ni waandaaji wa michuano hii. Hata unapopiga hesabu ya wao kufuzu kama wasingekuwa waandaaji bado haoni wangeweza kufuzu vipi mbele ya Australia, Japan na Korea Kusini.

Kwanini waandaaji ni wabovu kiasi hiki? Waliamua kufanya maandalizi makubwa ndani ya uwanja halafu wakasahau jambo moja tu. inawezekana timu yao imekaa kambini miaka minne. Inawezekana walikuwa wanaishi katika hoteli za kifahari kwa miaka minne. Inawezekana walikuwa wanafanya mazoezi katika viwanja vya kisasa vilivyopitiliza. Inawezekana wameahidiwa mabilioni ya pesa wakivuka hatua ya makundi.

Hata hivyo, kuna jambo moja tu walisahau. Walisahau kutoka nje ya mipaka yao na kwenda kujifunza kwingine. Wachezaji wao wote wanacheza soka ndani ya nchi yao. Afadhali nchi yao yenyewe ingekuwa walau kama Tunisia au Morocco. Hapana, ni Qatar.

Mastaa wao wakiongozwa na staa Akram Afif ambaye ni mtoto wa staa wa zamani wa Simba, Hassan Afif wote wanacheza nyumbani. Wamejifungia nyumbani kwahiyo huwa wanajidanganya kwa viwango vyao wenyewe. Hili ndilo tatizo ambalo hata Tanzania na timu yetu ya taifa tunalo.

Tofauti ni kwamba kina Afif na kile kikosi ambacho umekiona mastaa wao wanacheza nyumbani na ni matajiri. Wale kina Afif wanaendesha magari ya kifahari kama Lamborghini, Range Rover, Ferrari, Aston Martin Languish na mengineyo.

Wanalipwa mabilioni ya fedha ambayo yanasababisha wasitamani kucheza nje. Wanaishi katika ‘apartment’ za kifahari na zaidi ya kila kitu kwamba licha ya kuwa katika maisha haya wanafurahi zaidi kuwa katika maisha waliyokulia.

Wale Ecuador karibu wote wanacheza nje ya nchi yao. Achilia mbali kwamba wapo katika bara ambalo linajua soka, lakini wametawanyika. Wapo wengi wanaocheza Ulaya, Marekani, Brazil na kwingineko. Huko wanacheza mechi za maana kila wikiendi.

Hii ndio tofauti uliyoina. Enner Valencia aliyefunga mabao mawili na kukataliwa moja kwa sasa anacheza zake Fenerbahce lakini alishacheza katika kikosi cha West Ham. Moises Caecido anacheza Brighton, Carlos Gruezo anacheza FC Augsburg, Angelo Preciado anacheza Genk, Roberto Arboleda anacheza Sao Paulo ya Brazil. Na wengine wapo katika mfumo huu huu.

Timu kama yao inaweza isiwe bora mbele ya Brazil, Ufaransa, Argentina na wengineo lakini inaweza kujipigia vibonde wanaojifungia nyumbani Qatar kwa namna yoyote ambayo wanajisikia. Na ndio maana walipomaliza kazi katika kipindi cha kwanza wakaamua kupumzika katika kipindi cha pili.

Ambacho Qatar walipaswa kukumbuka katika soka la kisasa ni kuwapeleka mastaa wao wakapate uzoefu wa kucheza nje. Walau mastaa wao wangeenda kucheza katika timu za kawaida Ulaya wangeweza kupata hisia za upinzani katika soka halisi.

Sio lazima kucheza Real Madrid au Barcelona lakini kama wachezaji wa Qatar wangekuwa wanacheza klabu kama Nice, Troyes, Verona, Wigan, na nyinginezo za aina hii wangeweza kuwa katika hali ya ushindani zaidi kuliko kile ambacho tumekiona juzi pale kwao.

Hali hii inanikumbusha timu yetu ya taifa. Tutawapamba wachezaji wetu kadri tunavyoweza lakini kama hawachezi soka la kiushindani kama Mbwana Samatta, Novatus Dismas, Simon Msuva au Kelvin John basi hatuna ambacho tunaweza kufanya kwa ajili ya timu ya taifa.

Mpira una viwango vyake. Si ajabu Qatar walikuwa wanajiona wapo tayari kwa ushindani pindi walipokuwa wanacheza wenyewe kwa wenyewe wakiwa kambini lakini wamekwenda kucheza na Ecuador wakaonyeshwa kwamba mchezo wa soka una viwango vyake.

Hakuna kitakachobadilika pindi watakapocheza na Senegal kisha Uholanzi. Wote hawa wawili wapo katika viwango vya ushindani wa kimataifa. Senegal imejaza mastaa wanaocheza Ulaya kama ambavyo ilivyo kwa Uholanzi. Ni ngumu kwa Qatar kufanya chochote labda miujiza ya Mungu itumike.

Hata hapa Afrika kwa jinsi timu yetu ya taifa inavyoundwa nadhani tunahitaji miujiza kufanya vizuri katika soka ngazi ya timu ya taifa. wachezaji wetu watacheza vizuri hapa lakini wababe wetu wakiwa ‘serious’ lazima watatuonyesha utofauti.

Ni kama majuzi rafiki zetu DR Congo walivyoamua kutuonyesha utofauti. Tulicheza nao kwao wakaleta masikhara tukaambulia sare. Mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wakaamua kuwaita wachezaji wao wote wanaocheza nje kwa ajili ya kuonyesha utofauti. Wakatupiga mabao 3-0 safi kabisa bila ya upendeleo.

Wale rafiki zetu kule Kaskazini Morocco, Tunisia na Algeria wana watu wanacheza Ufaransa, Ubelgiji na kwingineko. Wengine wamezaliwa huko huko Ulaya. Tunaweza kubishana nao hapa na pale lakini mwisho wa siku lazima tofauti itaonekana.

Mpira una viwango vyake. Tuendelee tu kuwasisitizia wachezaji wetu watoke nje pindi nafasi zinapojitokeza. Tunafahamu kwamba kuna wengi walikata tamaa na wakarudi, halafu kuna wale ambao hawataki hata kusikia habari ya kucheza nje. Ukweli ni kwamba wanatuangusha.

Ligi yetu ni kama ya Qatar tu. Haiwezi kumuandaa mchezaji kucheza Kombe la Dunia. Kuna wachezaji wengi ambao wameshindwa hata kutamba katika Ligi mbalimbali za Afrika lakini wamerudi Tanzania na wanaonekana wanatesa sana. Ni kipimo tosha kwamba Ligi yetu haiwezi kumwandaa mchezaji wetu kucheza Afcon mara kwa mara au kwenda Kombe la Dunia. Tutahitaji kubahatisha. Kama Misri ambao wana Ligi ya ndani nzuri wanashindwa kwenda Kombe la Dunia, vipi kuhsu sisi?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here