Home Habari za michezo SIMBA QUEENS vs YANGA PRINCESS LEO NI ZAIDI YA MECHI YA KISASI…UTAMU...

SIMBA QUEENS vs YANGA PRINCESS LEO NI ZAIDI YA MECHI YA KISASI…UTAMU UKO HAPA…

Simba vs Yanga

Wakati Simba Queens na Yanga Princess wakitarajia kumaliza ubishi wa nani zaidi katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu, vita kubwa kati ya makocha wa timu hizo mbili,

Charles Lukulu ambaye anahitaji kuweka heshima kubwa mbele ya Sebastian Nkoma, aliyewahi kuwa kocha wa Malkia wa Simba hao.

Simba Queens na Yanga Princess zitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa leo kumenyana kwenye mechi ya Ligi Kuu raundi ya tatu, zote zikiwa na alama tatu katika nafasi ya tano na sita baada ya kupoteza michezo yao ya ufunguzi ya ligi hiyo.

Vita vya makocha hao ni baada ya Kocha wa Simba, Lukulu kutaka kulipa kisasi kwa kumfunga Kocha wa Yanga Princess, Nkoma katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania utakaopigwa saa 11: 00 jioni.

Makocha hao walikutana katika michuano ya CECAFA huku Lukulu akiwa kocha wa SHE Coparates ya Uganda na Nkoma akiwa anainoa Simba na kufanikiwa kushinda mechi zote mbili katika hatua ya makundi na fainali.

Licha ya kukutana kwa timu hizo huku Simba Queens wakiwa wanaongoza kupata matokeo mazuri mbele ya Yanga Princess, ambapo katika mechi 10 zilizokutana, Simba Queens imeshinda nane, kufungwa moja na sare moja.

Kuelekea mchezo huo, Kocha wa Simba Queens, Lukulu ambaye ni mwenyeji wa mchezo huo, alisema wachezaji wake wako tayari kwa mchezo wa leo na utakuwa mgumu sana kwa sababu ina kikosi imara na kocha mzuri.

Alisema wanahitaji kupata matokeo, hivyo lazima kucheza kwa heshima kubwa kwa kila timu watakayokutana nayo na kwamba pamoja na Yanga kuwa vizuri, lakini Simba Queens ni bora zaidi.

“Hii ni ‘dabi’ yangu ya kwanza, lakini ninaifahamu Yanga nimecheza nao na kuwaona wapinzani wangu, nimeandaa kikosi changu imara na tayari kwa ajili ya kutafuta pointi tatu muhimu katika mchezo wetu wa kesho (leo).

“Ni mpambano wa makocha, Seba aliwahi kufundisha Simba Queens, anaifahamu vizuri, lakini nitaingia na mbinu zangu kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo wa leo,” alisema kocha Lukulu

Nahodha wa Simba Queens, Opa Clement, alisema wamejiandaa vizuri na kwamba kazi kubwa iliyobakia ni kufanya majukumu yao uwanjani ili kuendeleza ubabe wao mbele ya Yanga.

“Tuko tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho (leo), tumechukua ubingwa na tukaenda kuwakilisha CECAFA katika michuano ya kimataifa, lakini tunahitaji kurejea huko kimataifa, hivyo tunalazimika kushinda mechi zote za ligi ikiwamo dhidi ya Yanga Princess kupata alama tatu,” alisema Opa.

Kocha Nkoma, alisema utakuwa mchezo mgumu kidogo kwa sababu ni ‘dabi’ ambayo siku zote inakuwa na ugumu hasa kwa sababu Simba Queens wametoka kucheza mechi kubwa na wanaingia kwa heshima kubwa.

“Tumejipanga vizuri kukabiliana na Simba Queens nina waheshimu sana kwa sababu mchezo utakuwa mgumu kutokana na sina muda mrefu ndani ya Yanga Princess ambayo haijakuwa na muunganiko mzuri,” alisema Nkoma.

Nahodha wa Yanga Princess, Amina Bilal, alisema kila mchezaji ana morali wa mechi hiyo na wako tayari kutafuta matokeo mazuri katika mchezo wa leo.

“Kocha ametuandaa vizuri na kazi kubwa imebaki kwetu na tunaenda kucheza kwa kujitoa kuhakikisha tunafuta uteja na kuondoka na ushindi,” alisema Amina.

SOMA NA HII  KUMBE! SIMBA WANGETULIA WANGEWAFUNGA KMC MABAO MENGI