Home Habari za michezo WAKATI YA FEI TOTO HAYAJATULIA…BIGIRIMANA NAYE ALIAMSHA YANGA SC…

WAKATI YA FEI TOTO HAYAJATULIA…BIGIRIMANA NAYE ALIAMSHA YANGA SC…

Bigirimana akiwa Yanga SC

Wakati Yanga SC ikipiga hesabu kali juu ya mastaa wake wa kigeni nani atoke ili washushe majembe mapya, moja ya majina ya mastaa wanaotajwa kuwa kwenye mipango ya kuondolewa ni kiungo Mrundi Gael Bigirimana lakini mwenyewe wala hana presha na hilo.

Katika dirisha dogo hili lililowazi tangu Desemba 16, Yanga SC ina mpango wa kuongeza wachezaji wasiopungua wawili wa kigeni lakini inahitaji kupunguza wengine wawili kutokana na idadi ya ‘mapro’ (12), kutimia na miongoni mwa majina yaliyo mezani yakijadiliwa kukata ni pamoja na la Bigirimana huku wengine wakiwa ni Heritier Makambo, Tuisila Kisinda na Jesus Moloko.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga SC zinaeleza kocha mkuu wa kikosi hicho, Nassredine Nabi bado anataka kumuona Yacouba Sogne arudi kikosini na ataanza kuonyesha ubora wake kwenye mashindano ya Mapinduzi Cup yatakayofanyika kuanzia Januari visiwani Zanzibar na kama hawatamridhisha lolote linaweza kutokea.

Ili Yanga SC iongeze majembe katika usajili, wanahitajika kutoka wachezaji kuanzia wawili na Bigirimana, Kisinda, Moloko na Makambo ndio wanapigiwa chapuo la kuondoka jambo ambalo Bigirimana amesema hana presha anachotaka ni kukaa mezani na mabosi wake wayamalize.

“Nilijiunga na Yanga SC mwanzoni mwa msimu huu lakini hadi sasa sijapata muda wa kutosha na nafasi ya kudumu ndani ya kikosi cha kwanza, naamini katika muda na kadri siku zinavyokwenda nazidi kuzoea na kujua namna gani natakiwa kucheza na wenzangu.

“Haikuwa rahisi kwangu kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza kwani muda mwingi sikucheza Afrika hivyo nilihitaji kuzoea mazingira ambapo naamini kwa sasa nipo tayari kupambana zaidi,” alisema Bigirimana aliyewahi kuichezea Newcastle United ya Ligi Kuu England na kuongeza;

“Kuhusu kuondoka Yanga SC sijawaza kwakuwa hayo ni mambo ya kiuongozi, kama wataona sihitajiki watanijulisha na baada ya hapo tutakaa mezani kuyamaliza kutokana na mkataba ulivyo na sina shida juu ya hilo.”

Pamoja na hayo, huenda Bigirimana ambaye amebakiza miezi sita kwenye mkataba wake akasalia ndani ya Yanga kutokana na kandarasi yake kuwa na vipengele vigumu kuvunja na kama ataondoka basi Wanajangwani watalipa pesa ndefu.

SOMA NA HII  BAADA YA KUTOA GUNDU JUZI.....MUGALU KAANZA NGEBE...AFUNGUKA ALIYOYAPITIA...ADAI AMEPONA...