Home Habari za michezo KIMENUKAA YANGA…NABI ALIA NA FEI TOTO ISHU YA TIMU KUSHINDA KWA SHIDA…MSIMAMO...

KIMENUKAA YANGA…NABI ALIA NA FEI TOTO ISHU YA TIMU KUSHINDA KWA SHIDA…MSIMAMO WAKE HUU HAPA…

Habari za Yanga

Mashabiki wa Yanga wanajua timu yao inashinda lakini wanatamani kuona wapinzani wao wakipigwa nyingi ombi ambalo kocha wao Nasreddine Nabi amelisikia kisha akatoa sababu.

Nabi amesema kwamba hana haraka kwa timu yake kushinda kwa mabao mengi lakini amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa wapole kidogo kwa kuwa kuna mambo matamu zaidi wanayatengeneza kwa ajili ya michuano ya kimataifa.

Alifafanua zaidi Nabi alisema walilazimika kutengeneza fiziki za utimamu wa mwili kwa siku 7 walizopata kabla ya mechi ya Ruvu yakiwa pia maandalizi ya awali juu ya kikosi hicho kabla ya kuanza mechi za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika zitakazoanza Februari 12.

“Tulidhani tungepata nafasi ya kupata maandalizi kidogo pale baada ya Kombe la Mapinduzi lakini haikuwa hivyo hatukupata bahati kama ambavyo wenzetu wengine walibahatika kuipata hivyo ilikuwa lazima tutumie muda huu,”alisema Nabi.

“Tukaona maandalizi hayo tungeyafanya katika hizi siku saba ambazo tulikuwa kambini, nafikiri ni vile watu wana kiu ya kuona timu inashinda kwa mabao mengi, tunawaelewa mashabiki kiu yao lakini wasiwe na haraka tunatengeneza msingi mkubwa wa hilo pamoja na mashindano ya CAF ambayo mechi zake hazipo mbali.

Aidha Nabi aliwataka mashabiki kuwa na subira kidogo wakati huu wakitengeneza muunganiko mpya wa idara ya kiungo hasa baada ya kukosekana kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ huku viungo wengine wakiwa majeruhi sambamba na ujio wa mshambuliaji Kennedy Musonda.

“Ukiangalia kuna kitu pale kati tunaanza kukitengeneza upya, kwasasa tuna viungo wengi huku baadhi ambao walikuwa wanacheza wakiwa majeruhi, tumelazimika kubadili mambo pale tukiwa pia na ujio wa Mudathir (Yahya) ambaye tunaendelea kumjenga taratibu.

“Hili linahitaji muda kidogo tukitafuta muunganiko wao mpya, tukasema pia tubadili mfumo pia kujaribu kutafuta muunganiko wa washambuliaji wa mbele tukicheza na washambuliaji wawili Musonda (Kennedy) na Fiston (Mayele).

“Yanga tuna timu bora lakini watu wasiwe na shida ya haraka kuona tunashinda kwa mabao mengi, jambo zuri ambalo vijana wanafanya ni kupigana kushinda, ndio lengo letu kuu ni kushinda, tutakuwa mabingwa kwa pointi nyingi kiujumla mengine yatafuata.”

Yanga juzi ilicheza dhidi ya Ruvu Shooting na kushinda kwa bao 1-0, kwa mara ya pili kwa nyakati tofauti Nabi alirudi kutumia mfumo wa 4-4-2 kutoka ule uliozoeleka wa 4-2-3-1 ambao wamekuwa wakiutumia mara kwa mara.

Ishu ya Fei Toto….

Kocha Nabi amesema kwamba bado kuna nafasi ya Feisal Salum katika timu yake, akikumbuka akili ya kiungo huyo ya kufanya maamuzi ya haraka anapokuwa kwenye uso wa lango la wapinzani.

Nabi alisema awali Feisal hakuwa na ubora huo lakini walimhamisha nafasi pamoja na kumuongezea ubora wa kuwa na maamuzi ya haraka ya kupiga mashuti ya kushtukiza ambayo yalimuongezea ubora.

“Ukiangalia mechi kama hii ya jana (juzi) dhidi ya Ruvu tulikosa mtu mwenye ubora kama wa Feisal, anapokuwa karibu na uso lango la wapinzani, nadhani hata matokeo yetu yasingekuwa haya,”alisema Nabi.

“Kama mtakumbuka Feisal hakuwa na ubora huu ambao anao sasa, tulifanya maamuzi ya kumhamisha nafasi na kumwambia awe anafanya vile anapofika kwenye uso wa lango la wapinzani.

Aidha Nabi alisema wakati huu anataka kuhakikisha kazi ambayo waliifanya katika kumtengeneza Feisal sasa wanaihamishia kwa Mudathir ambaye tayari ameshakuwa na vitu vingine bora akijitofautisha na mwenzake huyo.

“Sasa tunaye Mudathir nataka niwaambie huyu jamaa anajua sana kukaba, kitu bora zaidi anakaba sana bila kusababisha makosa ya adhabu ndogo wala kupata kadi, hii ni tofauti na Feisal anapokaba, lakini changamoto ya Mudathir kuna wakati anataka kutoa pasi kwenye eneo ambalo angeweza kufanya maamuzi ya kupiga mashuti, hili tutalifanyia kazi ili awe kama Feisal.

“Angalia kuna nafasi jana (juzi), alikuwa eneo zuri kujaribu lakini akaamua kumpa pasi Sure Boy (Salum Abubakar), tukapoteza ule mpira kwa kuwa Sure Boy hakuwa amejiandaa kupiga shuti.”

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA KESHO...NABI ANGIWA MCHECHETO DHIDI YA NAMUNGO..ADAI NI WAGUMU...