Home Habari za michezo HUYO OKWA UNAAMBIWA KAMA KAZALIWA UPYA HUKO IHEFU…ANAKICHAFUA HATARI YANI….

HUYO OKWA UNAAMBIWA KAMA KAZALIWA UPYA HUKO IHEFU…ANAKICHAFUA HATARI YANI….

Okwa Akiwa Ihefu

Kiungo wa Ihefu, Mnigeria Nelson Okwa juzi usiku alifunga moja ya mabao mawili yaliyoipa timu hiyo ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Dodoma Jiji na kufunguka amefurahia kufungua akaunti ya mabao akiahidi kufanya vizuri kutokana na benchi la ufundi kumuamini na kumtia moyo.

Okwa anayeitumikia timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba alifunga bao hilo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma, huku lingine likiwekwa kimiani na Yacouba Songne aliyesajiliwa pia dirisha dogo akiwa mchezaji huru baada ya Yanga kushindwa kumrejesha.

“Maisha yamebadilika kwa kiasi kikibwa hapa kwa sababu nimekuwa nikiaminiwa na kupewa nafasi kila ambapo ninahitajika, jambo kubwa kwangu ni kuendelea kuipambania timu ili tufanye vizuri,” alisema na kuongeza;

“Siwezi kuzungumzia tofauti ya hapa na Simba ila hakuna kitu kizuri kama mchezaji unapopewa uhuru zaidi na kuondolewa presha, kwenye timu yetu tunacheza kwa umoja na kila mmoja wetu anafuraha na mwenzake,” alisema.

Kwa upande wa Kocha wa Ihefu, John Simkoko akimzungumzia mchezaji huyo alisema ili apate kile anachohitaji jukumu lake kubwa ni kuwafanya wachezaji wote wawe wamoja akiamini ushirikiano wao ndio siri ya kufanikiwa.

“Kizazi cha sasa hivi na miaka ya zamani ni tofauti sana kwa sababu wachezaji wa sasa wanahitaji kulelewa vizuri, Okwa alianza taratibu lakini kadri muda unazidi kusogea anaonyesha ubora tunaouhitaji,” alisema.

Licha ya Okwa kufunga bao la kwanza ila ni ushindi wa kwanza pia kwa kocha Simkoko tangu alipotangazwa rasmi kuifundisha timu hiyo ambapo mchezo wake wa awali alitoka sare ya bao 1-1 na Singida Big Stars Februari 12.

SOMA NA HII  WAARABU WAPANGA VIINGILIO 'BABU KUBWA' MECHI YAO NA YANGA...TIKETI ZINAUZWA LAKI...