Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA PILI NA BAMAKO…YANGA WAPANGA UMAFIA HUU KUMALIZA SHOW MAPEMA…

KUELEKEA MECHI YA PILI NA BAMAKO…YANGA WAPANGA UMAFIA HUU KUMALIZA SHOW MAPEMA…

Mashabiki wa Yanga

Klabu ya Yanga imetangaza rasmi kuzindua Kampeni ya hamasa kuelekea mchezo dhidi ya Bamako ya Mali.

Hayo yamesemwa  na Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe wakati akizungumza na wanahabari kuhusu maandalizi ya mchezo wao huo wa marudiano wa kundi D utakaopigwa jijini Dar es Salaam Machi 8, 2023.

“Huu mchezo wa tarehe 8 kauli mbiu yetu ni rahisi sana “KWA MKAPA NI FULL SHANGWE” tunataka uwanja ujae, mashabiki wakaamue mechi ili wapinzani wajue chaka waliloingia sio.

“Hii mechi ya Bamako tumeikabidhi kwa mshabiki wetu, na tunaposema Full Shangwe tunamaanisha kushangilia kuanzia dakika ya kwanza hadi ya 90, hakuna kupoa tunataka Bamako walikurudi Mali wakahadidhie kwamba Tanzania hakuna timu bora yenye mashabiki kama Yanga.

“Kesho pale Buguruni Chama tunakwenda kuzindua rasmi kampeni ya Hamasa zetu kuelekea mchezo wetu na Bamako na tunawaalika wana Yanga wote mje mtazame Uzinduzi wa Hamasa zetu ili tukaujaze Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Tunataka Real Bamako wakiondoka Tanzania waende wakawaambie watu wa nchi yao kwamba wamekutana na Klabu yenye mashabiki bora Afrika. Ili sisi Yanga tufuzu robo fainali hatuhitaji kusubiria hesabu za Klabu nyingine,tunatakiwa kushinda mechi zetu dhidi ya Bamako na Monastir.

“Sisi Jumatano ijayo pale kwa Mkapa tunakwenda kushinda mchezo wetu dhidi ya Real Bamako na kufikisha alama [7] kwenye kundi letu, na Bamako wanapaswa waje wafahamu kuwa Yanga SC ni hatari wanapokuwa nyumbani.

“Kile ambacho kimetokea kwenye mchezo wetu dhidi ya TP Mazembe inatakiwa kiwe mara mbili katika mchezo wetu dhidi ya Real Bamako, na safari hii tunakwenda na Slogan ya “FULL SHANGWE” twende tukaujaze Uwanja.

“Tumesikia propaganda kuwa uwanja wa Mkapa Yanga haifanyi vizuri kimataifa. Sasa ule ushindi dhidi ya Mazembe ni kionjo tu, Mambo makubwa yanakuja. Mechi ya Bamako kuanzia dakika ya 1-30 wawe wamekufa za kutosha, wasije wakapata kona dakika 90 wakasawazisha,” amesema Ally Kamwe.

Katika kundi lao, Yanga wapo nafasi ya pili wakiwa na alama 4 nyuma ya US Monastir wanaoongoza kundi wakiwa na alama 7. TP mazembe alama 3 na wa mwisho ni Real Bamako wenye alama 2.

Aidha, Kamwe ameongeza kuwa mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons wa Kombe la TFF utachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamanzi, baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa katika Ukarabati.

SOMA NA HII  LOMALISA ASHTUA YANGA...AFUNGUKA A-Z MPANGO WA SIRI WA YEYE KUTUA JANGWANI....