Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Adel Amrouche ni kama amempiga kijembe mpinzani wake Kocha wa Timu ya Taifa ya Uganda Micho, baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0, Ijumaa (Machi 24) katika Uwanja wa Suez Canal, mjini Ismailia nchini Misri.
Miamba hiyo ya Afrika Mashariki ilikutana katika mchezo wa
Mzunguuko watatu wa Kundi F. wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ huku Uganda wakiwa wenyeji wa mchezo huo kufuatia nchi yao kukosa viwanja vyenye sifa zinazoendana na vigezo vilivyowekwa na Shirikisho la Soka Barani humo ‘CAF’.
Kocha Amrouche ambaye alikuwa katika mtihani wake wa kwanza tangu alipotangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars mapema mwezi Machi, amesema alifanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo ambao amekiri ulikua mgumu.
Kocha huyo kutoka nchini Algeria amesema mara zote amekuwa na Falsafa za kujiandaa kwa kuepuka matokeo ya sare ama kupoteza, na ndicho kilichotokea katika mchezo dhidi ya Uganda ljumaa (Machi 24).
“Tulifanya maandalizi ya kutosha kuikabili Uganda, nimekuwa na falsafa za kujiandaa kwa kukwepa matokeo ya sare ama kupoteza, ndicho kilichotokea katika mchezo wetu hapa Misri.”
Katika hatua nyingine Kocha Amrouche amewashukuru mashabiki wa Tanzania waliojitokeza kuishangilia Taifa Stars, katika mchezo dhidi ya Uganda, huku akifichua siri ya kukubali kufundisha timu hiyo
kwa kusema amekua akivutiwa na ushawishi wa mashabiki ambao siku zote hujitokeza kuwapa morari wachezaji.
“Ninapenda kuwashukuru sana mashabiki waliojotokeza kuishangilia Taifa Stars hapa Misri, kwa sababu walionesha kuwa na Imani wakati wote na walifanikisha suala la kuwapa morari wachezaji wangu ili wapambane na kupata matokeo.”
“Nilifanya maamuzi ya kuja kufundisha soka Tanzania kwa sababu ya mashabiki, nimekuwa nikiona timu za hapa zinapocheza mashabiki wamekua mstari wa mbele kutoa ushirikiano wa kutosha kwa sababu wanapenda soka.”