Home Habari za michezo KAKOLANYA AWAVURUGA MABOSI SIMBA…..SINGIDA BIG STARS ‘WAMTUPIA’ DONGE NONO LA USAJILI…

KAKOLANYA AWAVURUGA MABOSI SIMBA…..SINGIDA BIG STARS ‘WAMTUPIA’ DONGE NONO LA USAJILI…

Golikipa wa Simba SC chaguo la Pili David Kakolanya kujiunga na Azam FC

Wakati baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Simba wakikwea pipa juzi kuelekea Morocco tayari kwa mchezo wao wa kukamilisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablaca, Singida Big Stars inazidi kuichanganya klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam kutokana na kuendelea kokamaa kuipata saini ya kipa wao namba mbili, Benno Kakolanya, imefahamika.

Simba  iliondoka na wachezaji 13, huku ikitarajia wengine tisa kuungana nao nchini Morocco baada ya kumaliza majukumu ya timu zao za taifa.

Hata hivyo, Kakolanya ambaye anaunda kikosi cha Taifa Stars kilichokuwa na jukumu la kuivaa Uganda katika Uwanja wa Benjamin Mkapa  kwenye mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, mkataba wake na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu huu na inadaiwa kipa huyo tayari amesaini mkataba wa awali wa miaka miwili na Singida Big Stars.

Awali, ilidaiwa kuwa Simba ilikuwa tayari kumpa Sh. milioni 50 na mshahara wa Sh. milioni tano kwa mwezi ili kusaini mkataba mpya wa miaka miwili, lakini Singida Big Stars ilichungulia dili hilo na kupanda juu kwa kumwekea mezani Sh. milioni 100 na mshahara kama huo wa klabu yake kwa mwezi.

Akizungumza nasi jana, Meneja wa mchezaji huyo, Seleman Haroub, ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, alisema tayari mazungumzo ya awali yalifanyika na anaimani wataenda vizuri na kipa huyo kusalia ndani ya klabu hiyo.

“Ni kweli kuna baadhi ya timu zimekuwa zikimsumbua mchezaji wetu, hii ni baada ya mkataba wake kuelekea kufikia ukingoni, Mtendaji Mkuu wa Simba, Kajula (Imani) anafanya juu chini Kakolanya aendelee kusalia ndani ya kikosi cha timu yetu kwa msimu ujao,” alisema meneja huyo.

Aliwatoa presha mashabiki wa Simba kuwa mteja wake huyo ataendelea kusalia ndani ya kikosi cha timu hiyo kwa sababu mazungumzo mengine yanaendelea ili kumwezesha kuendelea kuvaa jezi ya Wekundu wa Msimbazi hao kwa msimu ujao.

Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana kutoka ndani ya klabu hiyo, Simba wanapambana kumzuia kipa huyo kwenda kuitumikia Singida Big Stars kwa msimu ujao kwa kuhakikisha wanampa ofa anayohitaji.

Mtoa habari alidai kuwa tayari Singida Big Stars imemwingizia fedha katika akaunti yake, hivyo inachotakiwa Simba ni kukubaliana na dau ili kumpa arejeshe.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira, akizungumza na mwandishi wetu katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kabla ya kukwea pipa kuelekea Morocco kwa mchezo dhidi ya Raja Casablanca, amesema pamoja na kuwa wameshatinga hatua ya robo fainali, lakini anakwenda kupambana kwa ajili ya kusaka ushindi na kukiweka sawa kikosi chake kwa ajili ya mechi zinazofuata kwani anataka kwenda mbali zaidi ya hapo.

“Tuko kwenye kiwango kizuri sasa, kuliko mwanzo tulipokutana nao, hivi sasa wachezaji wangu wapo moto, kuna Kibu Denis, kuna kiwango bora cha Jean Baleke, halafu nyuma hapa nina Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza.

“Wote wapo kwenye kiwango cha juu kuliko mwanzo tulipokutana nao, tunaweza kabisa kulipa kisasi, lakini tunacheza kwa ajili ya kutengeneza ufiti na kujiamini kwa wachezaji kwani timu kubwa kama ile inawafanya wachezaji wasiwe na shaka tena kucheza na timu nyingine kwenye hatua ya robo, nusu fainali na hata fainali,” alisema Robertinho.

Kwa upande wa Ahmed Ally, alisema wanakwenda kucheza mechi ambayo licha ya kwamba inachezwa usiku mzito, lakini haina presha sana kwa sababu wameshatinga hatua ya robo fainali.

“Wachezaji Aishi Manula, Shomari Kapombe, Beno Kakolanya na Mdhamiru Yassin, wao wataondoka nchini Jumatano (kesho) kuja kujiunga na wenzao. Kwa wachezaji wengine ambao wapo kwenye vikosi vya timu za mataifa mengine kama Chama, Enock Inonga, Peter Banda, Pape Sakho, pamoja na Saido, wao watatoka kwenye mataifa yao kuja moja kwa moja kujiunga na kikosi.

“Kwenye kikosi hatutokuwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwa kuwa yeye ana kadi tatu za njano, pia tutawakosa baadhi ya wachezaji ambao ni majeruhi na wengine nao hawajapona vizuri, nawazungumzia Mohamed Outtara, Joans Mkude, Augustine Okra, Ismael sawadogo, Jimmyson Mwanuke na Mohamed Mussa.

“Mechi yetu itakuwa ni Jumamosi saa nne usiku kwa saa za Morocco, lakini hapa nchini ni saa saba usiku,” alisema.

Raja ina pointi 13 mpaka sasa, huku Simba ikiwa na pointi tisa, hivyo matokeo ya mechi hiyo licha ya kwamba hayatoathiri timu hizo kufuzu, lakini hayatoathiri msimamo wa kundi hilo kwani hata Wekundu wa Msimbazi hao wakishinda wataishia pointi 12.

SOMA NA HII  MASHABIKI FENERBAHCE WATAKA ALIYERUHUSU SAMATTA AUZWE AFUKUZWE HARAKA....OZIL ATAJWA..