Home Michezo MRITHI WA KAPOMBE TAIFA STARS…”KUNA KITU WAMEONA…SIJAITWA BURE

MRITHI WA KAPOMBE TAIFA STARS…”KUNA KITU WAMEONA…SIJAITWA BURE

MRITHI WA KAPOMBE TAIFA STARS...KUNA KITU WAMEONA...SIJAITWA BURE

FUNGU la kwanza la kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars tayari kipo Misri baada ya kutua salama tangu kilipoondoka alfajiri ya jana, huku fungu la pili lenye wachezaji wa Yanga likiondoka leo, lakini beki aliyechukua nafasi ya Shomari Kapombe kikosini amewatuliza mashabiki wa soka nchini.

Beki huyo Datius Peter anayekipiga Kagera Sugar kabla ya kuondoka na timu hiyo amewatoa hofu mashabiki akiwahidi yeye na wenzake walioitwa na Kocha Adel Amrouche watafanya kazi vizuri.

Stars inajiandaa kucheza na Uganda katika mechi ya kuwania fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) itakayochezwa Ijumaa hii kabla ya kurudiana Machi 28 jijini Dar es Salaam na jumla ya wachezaji 31 waliitwa na kocha Amrouche, huku mabeki wa Simba,

Shomary Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kuachwa na kuitwa kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye jana hakuambatana na timu hiyo imekuwa gumzo kwa mashabiki baadhi yao wakiwa na hofu na timu kufanya vizuri.

Kocha msaidizi wa Stars Hemed Morocco, alisema Fei aliomba ruksa na ataungana na wenzake leo, lakini, mmoja ya mabeki walioitwa kuziba nafasi ya Kapombe, Datius alisema nafasi aliyoipata ni muhimu kwake na ataitumia ipasavyo kwa kutowaangusha Watanzania.

Beki huyo wa zamani wa Mbao na Polisi Tanzania, aliwaomba mashabiki wa soka kuwa na subira na kuwaombea wafanye vizuri kuliko kuwakatisha tamaa ili waweze kuisaidia Stars isonge mbele.

“Ilikuwa furaha kubwa sana katika maisha yangu ya soka kwasababu kuna kitu wamekiona (benchi la ufundi) kwangu ndiyo maana nimejumuishwa katika kikosi hiki,” alisema beki huyo na kuongeza

“Kuhusu maoni ya mashabiki siwezi kuongelea hilo kwa haraka ila tuwe na subira tufanye kazi ila tunaomba Mungu atubariki tupate nafasi tufanye kazi watupe muda tutafanya vizuri, mimi nahisi tutafanya vizuri Mungu atubariki sana tufanye vyema,” alisema Datius aliyekuwa kati ya wachezaji wa awali wa Stars waliondoka jana na kufika salama Misri kabla ya kuungana na wengine walioitwa.

Stars ipo Kundi F katika michuano hiyo ikishika nafasi ya tatu kwa sasa ikikusanya pointi moja sawa na Uganda, huku Algeria ikiongoza kundi ikiwa na pointi sita na kufuatiwa na Niger yenye alama mbili.

SOMA NA HII  BACCA AFICHUA YANAYOENDELEA YANGA..."SIWEZI KUTAJA SIFA ZA MCHEZAJI...AFUNGUKA HAYA