Home Habari za michezo WAKATI DIARRA AKIIPA YANGA MIL 316 MPAKA SASA…HIVI NDIVYO ALIVYOMUACHA MBALI MANULA...

WAKATI DIARRA AKIIPA YANGA MIL 316 MPAKA SASA…HIVI NDIVYO ALIVYOMUACHA MBALI MANULA KWENUE UBORA WA CAF…

MASTAA wa Yanga hadi sasa wameshavuna kiasi cha zaidi ya Sh 316 milioni kama bonasi ya kufanya vizuri kwenye mechi tatu kati ya nne zilizopita za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini hapana shaka kiwango bora cha kipa Djigui Diarra kimechangia kwa kiasi kikubwa kwao kupata mzigo huo mnono wa fedha.

Fedha hizo, Sh  mil 250 ni bonasi kutoka kwa uongozi na mdhamini wa timu hiyo kampuni ya GSM ambapo kila mechi waliyoshinda walipewa Sh 100 milioni na mechi waliyotoka sare ugenini walipata Sh 50 milioni.

Kiasi cha Sh 30 milioni wamekipata kama zawadi ya kufunga mabao sita kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Hassan ambaye kila bao linaklofungwa na timu ya Tanzania kuanzia hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika anatoa kiasi cha Sh 5 milioni na kiasi kingine kilichobakia kimetolewa na wadau tofauti.

Uwezo wa hali ya juu wa Diarra kuokoa mashambulizi ya hatari, umeifanya Yanga kuondoka na pointi saba katika mechi dhidi ya TP Mazembe na nyingine mbili dhidi ya Real Bamako ambazo zimewafanya wapate bonasi hiyo ya fedha kwa kushinda na kufunga mabao katika michezo hiyo.

Takwimu zinaonyesha kama sio uwezo wa Diarra kuokoa michomo ya hatari katika mechi hizo, kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa Yanga kupoteza na hivyo leo hii isinbgeweza kuvuna kiasi hicho cha fedha.

Kwa mujibu wa takwimu, hadi sasa Diarra anashika nafasi ya tatu kwa kuokoa michomo mingi kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na wastani wa kuokoa hatari 3.3 kwa mchezo.

Katika mchezo ambao Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe, Diarra aliokoa hatari tano ambazo kama angeruhusu mabao katika nusu ya hatari hizo, Yanga ingeweza kupoteza au kutoka sare.

Diarra aliokoa hatari nne katika mechi ya ugenini dhidi ya Real Bamako ambayo Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 na Real Bamako na walipokutana hapa Dar es Salaam na Yanga kushinda mabao 2-0, kipa huyo aliokoa hatari moja.

Katika chati hiyo ya makipa waliofanya vizuri katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kinara ni Bechir Ben Said wa Monastir ambaye ana wastani wa kuondoa hatari 5.8 kwa mechi na wa pili ni Ahmed El Shenawy wa Pyramids FC ambaye ana wastani wa kuokoa hatari 3.5 kwa mechi.

Wakati Diarra akitamba kwa kuokoa hatari nyingi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, kipa wa Simba, Aishi Manula yupo nafasi ya tisa katika orodha ya makipa waliofanya sevu nyingi katika hatua hiyo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Manula ameokoa wastani wa hatari mbili kwa mchezo na kinara kwa upande wa mashindano hayo ni Farid Ouedraogo wa AS Vita ambaye ana wastani wa kuokoa hatari nne kwa mchezo.

Kocha wa zamani wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali alisema utulivu na umakini ndio silaha kubwa ya mafanikio kwa Diarra.

“Hana papara anapokuwa anashambuliwa na hesabu zake ni nzuri za kujua asimame wapi na afanye nini kwa wakati gani. Kuna mengi ambayo makipa wetu wa Kitanzania wanaweza kujifunza kwake,” alisema Pondamali.

SOMA NA HII  MKUDE AFUNGUKA A-Z MAISHA YAKE YAKUITUMIKIA SIMBA NA PANDA SHUKA ZAKE...AGUSIA SUALA LA KULEWA ...AMTAJA MORRISON..