MCHEZO wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kati ya Simba na Ihefu utapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi saa 1:00 usiku badala ya kuchezwa Uwanja wa Uhuru kama ilivyotangazwa hapo awali, huku wageni wakisema hata huko wao wanaona freshi tu.
Inadaiwa Uwanja wa Uhuru siku ya mchezo huo una matumizi mengine na kulazimisha waandaaji wa michuano ya ASFC, Shirikisho la Soka (TFF) kuhamishia huko kwa kushauriana na wenyeji wa pambano hilo.
Akizungumza na SOKA LA BONGO jijini Dar es Salam, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema sababu kubwa za mabadiliko hayo ni kutokana na Uwanja wa Uhuru uliopangiwa kutumika kwa shughuli nyingine.
“Tumepokea mabadiliko hayo kwa sababu Uwanja wa Uhuru siku hiyo ya Ijumaa utatumika kwa ajili ya mashindano makubwa ya usomaji wa Quran tukufu hivyo tukaona ni vyema tuhamishie mchezo wetu Chamazi,” alisema Ahmed.