Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kuwa kuna uwezekano mkubwa Simba na Yanga kwa pamoja zikashiriki mashindano ya Africa Super League baada ya timu 24 kupitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Awali zilikuwa timu 8 pekee ambazo zilipangwa kuanza mashindano hayo yatakayofanyika Agosti mwaka huu huku Tanzania ikiwa na mwakilishi mmoja pekee ambaye alikuwa Simba Sc.
“Tukiwa Afrika Kusini, Aprili 5 tulifanya kikao na kamati tendaji ya (CAF), tukapendekeza mashindano ya Africa super league badala ya kuanza na timu (8) yaanze na timu (24).
“Kamati tendaji imeyapitisha hivyo yataanza na timu (24) na kuna uwezekano Tanzania tukatoa timu (2) Simba na Yanga kushiriki michuano hiyo. Tangu mwanzo zilitakiwa timu (24) COSAFA na CECAFA tuna nafasi ya kutoa timu (8), na kila zone zitatoa timu (8) ili kufika (24) lakini awali tuliona kutokana na ufinyu wa muda zianze timu (8) kwanza halafu msimu ujao ndio zicheze (24)..
“Kikao kimeamua zianze tu timu zote (24), bado hawajaweka wazi watatumia vigezo gani kualika timu, ranks au kitu kingine, lakini tunaimani Tanzania tunaweza kutoa timu (2),” amesema Wallace Karia.