Home Habari za michezo MAPYA YAIBUKA…YANGA SC VS TP MAZEMBE…GSM AMALIZA MECHI MAPEMAA

MAPYA YAIBUKA…YANGA SC VS TP MAZEMBE…GSM AMALIZA MECHI MAPEMAA

Habari za Yanga SC

ZAMU ya nani leo? Ukisikia watu wanaimba wimbo huu basi ujue kabisa huyo ni shabiki wa Simba wakiwalenga watani wao wa Yanga ambao jioni ya leo itashuka uwanjani kuvaana na TP Mazembe ya DR Congo kwenye mechi ya heshima ya kufungia Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba yenyewe usiku wa kuamkia jana ilishuka uwanjani kumaliza mechi zao, lakini ikakumbana na kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Raja Casablanca, hivyo mashabiki wa klabu hiyo wanaisikilizia leo Yanga inayoshuka uwanjani kuanzia saa 10:00 jioni kucheza na wenyeji Mazembe jijii Lubumbashi.

Mechi ya leo kwa Yanga ni ya kuweka heshima tu, kwani tayari imeshafuzu robo fainali sambamba na US Monastir itakayoshuka baadae saa 5 :00 usiku kumalizana na Real Bamako, mjini Tunis Tunisia, huku kila moja hesabu zao ni kumaliza kinara wa kundi hilo kwani kwa sasa zinatofautiana mabao tu.

Yanga ambayo imeongezwa mzuka na uwepo kwa vigogo wa klabu hiyo akiwemo Bilionea Ghalib Said Mohamed ‘GSM‘, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na makamu wake, Arafat Haji sambamba na wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, Tarimba Abbas na Geofrey Mwambe ambao pia ni wabunge inataka kumaliza ikiwa kilele kama ilivyo sasa ili ipate urahisi kwenye mechi za robo.

Malengo hayo ya kumaliza kileleni ili kuanza ugenini na kisha kumalizia nyumbani kwenye mechi zijazo yakawahamisha kwa muda vigogo wao wasiopungua sita wakitua mapema na timu hiyo jijini Lubumbashi kuhakikisha wanaongeza hamasa kwa mastaa wa timu hiyo.

Vigogo hao hawakuambatana na timu kwenda tu kuangalia mechi, ila kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa na juzi walitua mazoezini kuangalia wachezaji wanavyoandaliwa kwa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Mazembe na kuchezeshwa na waamuzi kutoka Algeria.

Mnara wa hamasa ulikuwa unasomeka namba za juu kabisa kwa wachezaji kuanzia juzi na jana kuonekana kupambana tayari kwa mchezo huo kuendeleza ubabe wao mbele ya Mazembe ambao walipoteza kwa mabao 3-1 hapa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo hiyo sio mechi rahisi kwa Yanga, licha ya kwamba Mazembe imeshapoteza dira kundini na ghaikuwa na msimu mzuri tyangu ikishiriki Ligi ya Mabingwa kabla ya kung’olewa na Vipers na kuanguka kwenye kapu la Kombe la Shirikisho.

Mazembe haitataka kuharibu rekodi yanyumbani dhidi ya Yanga, lakini itakuwa ikitaka kulipa kisasi baada ya kichapo cha mechi ya Kwa Mkapa, pia kumfuta machozi tajiri wa Moise Katumbi na mashabiki kutokana na kuwa na msimu mbaya ikishika mkia wa kundi lao kabla ya mechi za leo.

Timu hiyo imeshinda mara moja tu nyumbani ikiwafunga Real Bamako ya Mali kwa mabao 3-1, kisha ikapoteza dhidi ya Monastir na leo itakamilisha ratiba ikiwa na jumla ya pointi tatu tu.

Tayari Katumbi amerusha taulo, akisema msimu huu amekubali matokeo, ila anakwenda kujipanga kwa kusuka upya kikosi chake, lakini wanajua kwamba kama itapoteza dhidi ya Yanga itawakera zaidi mashabiki wao ambao hawana furaha kabisa na timu yao.

Pigo kubwa kwa Yanga ni kuwakosa watu wao muhimu watatu kwanza watamkosa kocha wao Nasreddine Nabi ambaye amerudi tena kwao Ubelgiji anakoishi kuharakisha kupatikana kwa pasi yake ya kusafiri na kikosi hicho kitakuwa chini ya msaidizi wake Cedric Kaze.

Hata hivyo, SOKA LA BONGO linafahamu Nabi atakuwa anafuatilia mchezo huo kwa ukaribu akiwasiliana kwa karibu na msaidizi wake Khalil Ben Youssef ambaye ni mtaalam wao wa kuchambua mikanda ya video ya mechi za wapinzani.

Mbali na Nabi, pia Yanga itamkosa kipa namba moja Djigui Diarra na kiungo Khalid Aucho wanaotumikia adhabu ya kikanuni ya kukosa mchezo mmoja baada ya kufikisha kadi tatu za njano.

Hadi jana Nabi na Kaze walikuwa wamepanga kumpumzisha Djuma Shaban ambaye ana kadi mbili za njano na kama atapata kadi katika mchezo wa leo atakosa mechi ya kwanza ya robo fainali, pia kama watampumzisha kadi hiyo itafutika baada ya mechi za makundi kukamilika.

Habari njema kwa Yanga ni kuwasili kwa washambuliaji wao wawili tegemeo Kennedy Musonda na Fiston Mayele ambaye kwa mara kwanza Yanga inakwenda kucheza nyumbani kwao ambako ana mashabiki kibao akiishi jijini Lubumbashi.

Akizungumzia mchezo huo Mayele alisema ana kiu kubwa ya kutaka kuona Yanga inashinda mechi hiyo lakini akitaka kuwafunga Mazembe baada ya kuwakosa katika mchezo wa kwaza ambao alipika bao la tatu alilofunga winga Twisila Kisinda.

“Hii mechi itachezwa nyumbani ni rekodi na heshima kwangu, najua haitakuwa mechi rahisi lakini nimejipanga kuwafunga Mazembe kiu yangu ni kuwafunga baada ya kushindwa kufunga kule Tanzania,”alisema Mayele.

GSM na wenzake hawataki unyonge na mpaka jana gazeti hili linaingia mitamboni walikuwa wanajipanga kutoa ahadi nzito ambayo itawapa mzuka wachezaji wao ambayo inaweza isipunguas sh 100 milioni.

Kocha Pamphil Mihayo wa Mazembe alisema ingawa hawana nafasi ya kusonga mbele lakini wataingia katika mchezo huo kwa akili moja tu ya kutaka kuwaomba msamaha mashabiki wao katika mashindanbo ya CAF wakitaka ushindi.

“Hatuna kingine tunachotaka katika mchezo huu zaidi ya kuhitaji ushindi ili kuwafariji mashabiki wetu, umekuwa ni msimu wa anguko lakini tunajua kilichotuangusha, tunataka kushinda hii mechi hatuwezi kukubali kirahisi kuongeza maumivu kwa mashabiki wetu, tunawaheshimu Yanga walishinda kwao mchezo wa kwanza lakini na sisi tuko kwetu,”alisema Mihayo, kiungo wa zamani wa Mazembe.

SOMA NA HII  SIMBA QUEENS vs YANGA PRINCESS LEO NI ZAIDI YA MECHI YA KISASI...UTAMU UKO HAPA...