Home Habari za michezo MECHI YA SIMBA NA YANGA SIO VITA…MSIHATARISHE MAISHA YA WATU…MPIRA NI BURUDANI

MECHI YA SIMBA NA YANGA SIO VITA…MSIHATARISHE MAISHA YA WATU…MPIRA NI BURUDANI

Habari za Simba

Wikiendi hii shughuli zote za michezo zitasimama kupisha dakika tisini za machozi, jasho na damu ambapo wababe wa soka la Tanzania Simba na Yanga watashuka dimbani kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara mchezo ambao umebeba mambo mengi kuanzia ndani na nje ya uwanja.

Ni mchezo ambao umebeba historia kubwa kwa watani hawa ambapo ni bora timu ikose ubingwa lakini si kufungwa na mtani wake hivyo ni mchezo ambao umebeba maisha ya mashabiki wa timu hizi kwani si ajabu kuona shabiki wa Simba na Yanga akipoteza fahamu na hata kupoteza maisha kabisa kutokana na mshtuko wa matokeo ambayo awali hakuyatarajia.

Kuelekea mchezo huu Yanga wapo kileleni nyuma yao wapo Simba hapa ndipo ugumu wa mchezo huu unaanzia ambapo Yanga watahitaji ushindi ili kutanua wigo wa pointi na kujichimbia kileleni au Simba waibuke na ushindi na kuwashusha Yanga kileleni na kufufua matumaini ya kuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Tukiachana na haya yote tuuangalie mchezo huu kwa undani, ni mchezo ambao Simba ikishinda itapata pointi tatu na hata Yanga ikishinda pia itapata pointi tatu hivyo haupaswi kuwa mchezo wa kukamiana na kuumizana jambo ambalo halitakuwa na afya kwenye mpira wetu.

Matamanio ya wengi ni kuona soka la kuvutia lililojaa ufundi na udambwidambwi mwingi na siyo piga mpigeni mwisho wa siku mnaharibu ladha ya mechi husika, ingieni kwenye mchezo huu mkijua kuwa hakuna pointi sita ni pointi tatu hivyo onyesheni soka safi na la kuvutia.

Kila mchezaji ajue kuwa ana jukumu la kumlinda mwenzake hivyo hautakuwa uungwana kuona Kapombe akimuumiza kwa makusudi Bangala au Job akimuumiza kwa makusudi Baleke huku akijua fika kuwa soka ndiyo mustakabali wa maisha yenu na mnapata mkate wenu kupitia mchezo huu adhimu.

Mashabiki pia sijawasahau hampaswi kwenda na matokeo yenu uwanjani bali mnapaswa kumheshimu mpinzani wenu, uwe shabiki wa Yanga usiwachukulie poa Simba na wewe shabiki wa Simba usiwachukulie poa Yanga ili msije kuhatarisha afya zenu kutokana na kujiamini kulikopitiliza na pale matokeo yanakuja tofauti mambo yanakuwa magumu kwa upande wenu.

Waamuzi ambao mtapewa nafasi ya kusimamia sheria 17 za mchezo wa kandanda kwenye mtanange huu mnapaswa kuwa makini zaidi ya mnavyofikiria ili msije kuingia lawamani kutokana na maamuzi ambayo yanaweza kuhatarisha maisha ya mamilioni ya Watanzania pia kuzitia hasara timu hizi kutokana na kufanya maandalizi ya kutosha halafu wakose matokeo kwa uzembe wenu.

Jambo la kuvutia mchezo huu unakuwa wa kipekee kutokana na timu zote mbili kuwa kwenye hatua ya Robo Fainali kwenye michuano ya kimataifa Simba wakiendeleza historia yao ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Yanga wakiandika historia kwa mara ya kwanza kutinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho.

Hii inadhihirisha ubora uliopo kwa timu zote mbili tofauti na ilivyozoeleka miaka ya nyuma Kurwa akiwa unga Dotto anakuwa wa moto au Dotto akiwa unga Kurwa anakuwa wa moto.

Makosa ya kibinadamu hayaepukiki lakini mnapaswa kuwa makini na kutenda haki kwa kila timu ili tuonje ladha halisi ya Dabi ya Kariakoo. Kila la heri Watani.

SOMA NA HII  YANGA NJIA NYEUPE, HII NDIO HALI YA AL MARREIKH