Home Habari za michezo SIMBA KUVUNJIWA MWIKO HADHARANI…WATEKELEZAJI WA TUKIO HILO WAAPA

SIMBA KUVUNJIWA MWIKO HADHARANI…WATEKELEZAJI WA TUKIO HILO WAAPA

HII HAPA MASHINE YA SIMBA YARUDI UWANJANI...NI BAADA YA KUKAA NJE MUDA MREFU

MBEYA. KIKOSI cha Ihefu tayari kimetua Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa robo fainali Kombe la Azam (ASFC) dhidi ya Simba utakaochezwa kesho ikiwa ni maadhimisho ya Karume Day.

Licha ya rekodi kutoibeba Ihefu mbele ya Simba, lakini benchi la ufundi limeapa kuvunja mwiko huo kwa kuhakikisha inapata ushindi katika mchezo huo.

Ihefu haijawahi kupata ushindi mbele ya Simba tangu ilipopanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2020/21 na kushuka kisha kurejea tena msimu huu.

Hata hivyo, msimu huu Ihefu ndio imeonekana kuwa bora zaidi kuliko kipindi chote kutokana na uimara wake baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na benchi la ufundi wakati wa dirisha dogo la Januari.

Kocha msaidizi wa kikosi hicho, Zubery Katwila alisema imekuwa fahali kubwa kwao kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambayo kila mmoja anasaka ubingwa kwa aina yake.

“Tumejiandaa vizuri kukabiliana na Simba ambayo ni timu bora lakini kikubwa ni maandalizi yetu yamekuwa bora kwa muda wote ambao ligi imesimama.

“Tunaamini mchezo utakuwa mzuri na wenye upinzani kwa kila upande kutokana na umuhimu wa mchezo huo unavyochukuliwa,” alisema Katwila.

Aliongeza kikosi kipo katika hali nzuri ya kuhakikisha kinapambana na kuleta matunda mazuri kwa mashabiki na wapenzi wa Ihefu.

Katwila alisema huu utakuwa mchezo mgumu zaidi kutokana na aina ya mashindano yalivyo ambayo yanahitaji mshindi mmoja asonge mbele.

Baada ya mchezo huo timu hizo zitakutana tena Jumatatu katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa Uwanja wa Highland Estates, Mbarali ambapo Yanga na Azam zote zilifungwa kwenye uwanja huo msimu huu.

Mshindi kati ya Simba na Ihefu itakutana na Azam katika mchezo wa nusu fainali Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara kati ya Mei 16 na 17.

Azam tayari imekata tiketi ya kucheza nusu fainali kwa kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-0 huku Singida ikiichapa Mbeya City mabao 4-1 na sasa inangoja mshindi kati ya Yanga na Geita Gold.

Mshambuliaji wa Ihefu, Andrew Simchimba ndio kinara wa mabao kwenye michuano hiyo akifunga mabao saba akifuatiwa na Clement Mzize wa Yanga mwenye mabao sita.

Tangu msimu wa mwaka 2015/16 Simba pekee ndio imeweza kutetea ubingwa huo ilipofanya hivyo msimu wa mwaka 2019/20 na msimu wa mwaka 2020/21.

Ikumbukwe mchezo wa fainali utapigwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga, baada ya ligi kumalizika na hii ni mara ya kwanza kwa uwanja huo kutumika kwa fainali tangu msimu wa mwaka 2015/16 michuano hii iliporejeshwa upya.

SOMA NA HII  KUHUSU KUFELI KWA YANGA HERSI ASEMA MANENO HAYA