Home Habari za michezo WAPINZANI WA YANGA HALI TETE…WANA NJAA HATARI TIMU HAINA PESA…JE WATAKUJA?

WAPINZANI WA YANGA HALI TETE…WANA NJAA HATARI TIMU HAINA PESA…JE WATAKUJA?

WAPINZANI WA YANGA HALI TETE...WANAPITIA NJAA YA HATARI TIMU HAINA PESA...JE WATAKUJA?

Zikiwa zimebaki siku mbili tu kwa Yanga kucheza mchezo wa marudiano hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria, hali sio shwari kwa wapinzani wao kutokana na ukata wa kifedha.

Timu hizo zitarudiana Jumapili hii ya Aprili 30 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Nigeria Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa yote na nyota, Fiston Mayele.

Wakati mchezo huo wa marudiano ukisubiriwa tayari Wanigeria hao wameanza kuingiwa na mchecheto baada ya kile kinachodaiwa kukumbwa na ukata wa kifedha jambo ambalo linaweza kuwachelewesha kutua jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kutoka Nigeria, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Stanley Eguma alisema kwa sasa hali yao ya kiuchumi sio nzuri na huenda wakatua siku moja kabla ya mchezo kisha Jumatatu waondoke.

“Rais wetu wa timu bwana, Barrister Green ametuambia hali ya kiuchumi sio zuri hivyo kuna uwezekano mkubwa tukafika Dar es Salaam siku moja kabla ya mchezo kwa maana (Jumamosi) na Jumatatu tuondoke,” alisema Eguma.

Aidha Eguma aliongeza jambo lingine linalowakabili kwa sasa ni kukumbwa na wachezaji wengi majeruhi kitu ambacho kinaweza kuwaletea changamoto katika mchezo wa marudiano ambao ni mgumu kwao na wanahitaji ushindi.

“Mchezo uliopita wachezaji wetu wawili walipata majeraha hivyo nasubiria ripoti ya daktari wa timu kujua kama watakuwa fiti au laah, pamoja na mshambuliaji wetu tegemeo, Paul Acquah ambaye yeye hakucheza kabisa.”

Kwa upande wa Acquah ambaye ndiye kinara wa mabao ndani ya kikosi hicho kwenye Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na manne alisema kama wapinzani wao waliweza kushinda ugenini basi hakuna linaloweza kushindikana.

“Ni mechi ngumu kwetu kwa sababu tupo ugenini na tulishapoteza, tunapaswa kuongeza umakini mkubwa wakati wa kuzuia na kushambulia ili kuwafanya wapinzani wetu nao kutuhofia kwani kwenye mpira kila kitu kinawezekana.

Yanga inahitaji ushindi au sare tu ili kutinga hatua ya nusu fainali ambapo itakutana na mshindi kati ya Pryamid (Misri) au Marumo Gallants ya (Afrika Kusini) ambazo zilifungana bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza.

SOMA NA HII  YANGA WATUA NIGERIA,MATIZI KUPIGA LEO