Benchi la Ufundi la Simba SC chicni Kocha Roberto Oliviera ‘Robertinho’ limeweka wazi kuwa hesabu ambazo zipo kwa sasa ni kufanya vizuri kwenye michezo yote iliyobaki kwa kuwa bado wapo kwenye vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopo mikononi mwa Young Africans.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 68, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 63, huku kila timu ikisaliwa na michezo minne kuelekea ukingoni mwa msimu huu 2022/23.
Kwenye mchezo uliowakutanisha watani hao wa jadi ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba SC 2-0 Young Africans huku watupiaji kwa Simba SC wakiwa ni Henock Inonga na Kibu Dennis.
Juma Mgunda, Kocha Msaidizi wa Simba SC amesema wanatambua kuna kazi ngumu ya kufanya kwenye michezo iliyosalia lakini wapo tayari kushinda na inawezekana.
“Kuna malengo ambayo tunayo tukiwa ni timu na ukiagalia kwenye suala la ubingwa bado tupo kwenye mstari wa kupambania ubingwa kwa kuwa ligi haijaisha.”
“Ikiwa tupo kwenye mbio za kuwania ubingwa hakuna ambaye amekata tamaa, inajulikana kuwa haijafika mwisho mpaka ifike mwisho.” Amesema Mgunda
Leo Jumatano (Mei 03) Simba SC itaendelea na msako wa alama tatu za Ligi Kuu kwa kucheza ugenini dhidi ya Namungo FC itakayokuwa nyumbani katika Uwanja wa Majaliwa, huku Young Africans ikitarajiwa kucheza dhidi ya Singida Big Stars Alhamis (Mei 04) katika Uwanja wa CCM Liti mjini Singida.