Home Habari za michezo KISA YANGA KUKUTANA NA WASAUZI…ABDI BANDA AIBUKA NA HILI JIPYA…’AMFUNDISHA KAZI’ NABI…

KISA YANGA KUKUTANA NA WASAUZI…ABDI BANDA AIBUKA NA HILI JIPYA…’AMFUNDISHA KAZI’ NABI…

Habari za Yanga SC

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi amepewa mchongo mzima kama anataka timu yake iibuke na ushindi dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, mchezo wa nusu fainali wa Kombe la Shirikisho Afrika, utakaopigwa Mei 10 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Beki wa Chippa United inayofanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Mtanzania Abdi Banda anaifahamu vizuri Marumo Gallants walipocheza nayo mechi ya Ligi Kuu ya nchini huko na amesema siyo timu ya kubeza.

Banda anasema walishinda kwenye mchezo wa raundi ya kwanza walipovaana na timu hiyo, lakini wakajikuta wakipoteza mchezo wa pili, lakini kazi haikuwa rahisi kwao na hivyo Yanga wanatakiwa kuwa makini na maeneo kadhaa.

“Kwanza kabisa Yanga ijiandae isije ikapotezwa na msimamo wa Marumo kwenye Ligi Kuu ya huku, hao jamaa ni hatari, wanacheza kwa kasi, kitimu, mbinu na akili kubwa kuliko nguvu na wana vijana wengi wenye uchu wa mafanikio.

“Pili, kwa asilimia 90, Yanga inatakiwa imalize mechi Tanzania, huku siyo rahisi kama wanavyozungumza mashabiki wao mitandaoni, ila naamini Kocha Nabi ni mtaalamu wa mbinu atakuwa ameifuatilia vya kutosha na kuandaa vijana wake kwa ajili ya ushindi.

“Tatu, ili Yanga ipate ushindi dhidi ya hii timu itumie viungo wengi pale kati ili kutibua mipango ya wapinzani wao kwa kuwa ni sehemu ambayo kwenye kila mchezo wapo vizuri sana, umakini uwe mkubwa wa kuhakikisha hawapotezi nafasi za kufunga, naamini kwa kufanya hivyo watafanikisha malengo yao ya kwenda fainali,” alisema.

Alisema timu hiyo ina wachezaji wenye uwezo wa kubadilika uwanjani kulingana na mchezo unavyokwenda, hivyo inakuwa rahisi kwao kupata matokeo.

“Nne, Yanga ni timu ya Tanzania, lazima ijue njia ya kupenya ili isonge mbele kwenye hiyo michuano, unapotaka kumshinda mpinzani wako lazima umkabili kwenye uhalisia wake na siyo vingenevyo, Yanga wanatakiwa kuwachunguza zaidi wapinzani wao,” alisema.

Jambo la tano, alimtaja straika hatari zaidi ndani ya kikosi hicho ni Ranga Chivaviro ambaye kwenye michuano hiyo ana mabao matano sawa na Fiston Mayele wa Yanga na mabeki watatakiwa kumtupia jicho la umakini.

“Ana jicho la kuona nafasi za kufunga, hakati tamaa hadi aone mpira tayari umechukuliwa na wapinzani wake, hivyo wasije wakapuuza mipira ya kufa inayokuwa mbele yake, pia ana kasi ambayo inaweza ikawachanganya mabeki kama hawatakuwa wepesi,” alisema.

Banda ni kati ya wachezaji wazoefu kwa soka la Tanzania akiwa ameitumikia timu ya Taifa, Taifa Stars kwa miaka kadhaa, Simba, pamoja na Mtibwa Sugar na kote alionyesha kiwango cha juu, hii ni mara yake ya pili anacheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini, baada ya awali kuitumikia Baroka kwa mafanikio.

SOMA NA HII  SIMBA DAY: SIMBA 0-0 TP MAZEMBE