Home Habari za michezo SIMBA WAANZA KUSHUSHA VIFAA….ONANA APEWA MIWILI ….BRUNO GOMES WA SINGIDA AITWA DAR...

SIMBA WAANZA KUSHUSHA VIFAA….ONANA APEWA MIWILI ….BRUNO GOMES WA SINGIDA AITWA DAR CHAP…

Tetesi za Usajili Simba

KAZI imeanza Msimbazi, baada ya mabosi wa klabu hiyo kutarajia kuanza kutambulisha nyota wapya inayowasajili kwa msimu ujao, ikiwa tayari imempa mkataba wa miaka miwili winga Mcameroon, Leandre Onana, huku ikimuita jijini Dar es Salaam, Bruno Gomes wa Singida Fountain Gate FC.

Onana ndiye Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda akifunga mabao 16, inadaiwa amesainishwa mkataba huyo mapema wiki hii na leo huenda akatambulishwa rasmi, akiwa ni pendekezo la Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

Lakini wakati Onana akitarajiwa kutambulishwa, kiungo mshambuliaji wa Singida, raia wa Brazil Bruno ameitwa jijini kwa ajili ya kumalizana na mabosi hao wa Msimbazi kabla ya kutangazwa kuwa mmoja ya nyota wapya wa timu hiyo kwa msimu ujao ambao Wekundu wamepania kurejesha heshima.

Tayari Bruno aliyefunga mabao 10 msimu huu kwenye ligi, yuko Dar es Salaam akiambatana na viongozi wa Singida na kama mambo yataenda kama ilivyopangwa atasaini mkataba wa miaka miwili pia.

Mbarazili huyo pia ni pendekezo la Robertinho ambaye aliwaambia vigogo wa Simba anamtaka ili akasaidiane na Clatous Chama, Saidi Ntibazonkiza na Mzamiru Yassin eneo la kiungo.

Moja wa vigogo wa Simba (jina tunalo) alithibitisha Onana na Gomes wamezungumza nao ili kuwasajili na huenda wakatambulishwa mmoja baada ya mwingine.

“Onana na Gomes ni shabaha yetu na kuanzia kesho mnaweza kuona tarifa rasmi kuhusu wao,” alisema kigogo huyo na kufafanua; “Tayari huyo winga (Onana) tumemalizana naye na sasa tupo kwenye hatua za mwisho kumsainisha Bruno kwani tupo naye hapa Dar es Salaam, ikiwa ni mwanzo wa pazia la usajili kwa kikosi kijasho.”

Aidha  Simba ipo kwenye hatua za mwisho kumrudisha beki wake wa zamani, David Kameta ‘Duchu’ aliyekuwa Mtibwa Sugar.

Simba inaamini miaka miwili ambayo Duchu alipelekwa kwa Mkopo Geita Gold na Mtibwa imetosha kumfanya aimarike zaidi sasa atarejea ili kushindania namba na Shomari Kapombe aliyemiliki namba mbili kwa muda mrefu.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alithibtisha timu yake msimu huu itachukua mchezaji inayemtaka kwenye timu yoyote.

“Siwezi kuweka wazi tumemsajili nani na nani lakini unachotakiwa kujua ni kwamba kila mchezaji tunayemtaka tutampata bila shida yeyote. Simba ni timu kubwa,” alisema Ahmed.

Kwa sasa Simba imevunja kambi yake na baadhi ya wachezaji wake wapo timu za taifa huku kocha Robertinho akiwa tayari kwao Brazil, lakini jana klabu hiyo ilitoa taarifa ya kuachana na baadhi ya watu wa benchi la ufundi na kuwatangazwa wapya walioingia kwa kazi za msimu ujao.

Mabosi hao pia wamepitisha panga kikosini na hadi sasa Augustine Okrah ametangazwa rasmi, huku Ismael Sawadogo, Gadiel Michael, Habib Kyombo, Mohamed Mussa, Beno Kakolanya na Mohamed Ouattara wakisubiriwa nao kutangazwa baada ya kumalizika kwa taratibu za kuagana nao pamoja na baadhi ya watu wa benchi la ufundi.

SOMA NA HII  BALEKE ALIAMSHA SIMBA HUKO....ATOA MSIMAMO WAKE MAZIMA KUHUSU MUSTAKABALI WA MSIMU UJAO...