Home Habari za michezo BAADA YA KUMKOSA NABI YANGA SASA WAANZA UPYA

BAADA YA KUMKOSA NABI YANGA SASA WAANZA UPYA

Habari za Yanga leo

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga pamoja na mafanikio makubwa waliyoyapata msimu uliopita wakitwaa mataji matatu – Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kutinga fainali Kombe la Shirikisho Afrika watakuwa na kocha mpya.
Mafanikio waliyoyapata Yanga walikuwa chini ya kocha Nasreddine Nabi ambaye ameondoka baada ya mkataba wake kumalizika huku ikitajwa kuwa hakutaka kuendelea na ajira hiyo.
Wakati Yanga wakimpoteza kocha huyo ambaye amewapa mafanikio, pia kuna timu zimewaacha makocha ambao wamezipa mafanikio kama Tanzania Prisons na KMC ambazo zilikuwa kwenye wakati mgumu wa kushuka daraja, lakini zimebaki.
Mwanaspoti linakuletea timu nane ambazo msimu ujao zitaanza msimu na makocha wapya.

YANGA
Baada ya kuondoka kwa Nabi, Yanga imemtangaza Miguel Angel Gamondi kuchukua mikoba yake akitokea timu ya Ittihad Tanger ya Morocco.
Kocha huyu mwenye uraia wa Argentina na Italia, ana umri wa miaka 56 pamoja na kufundisha timu zaidi ya tano katika safari yake yote hiyo mafanikio makubwa aliyowahi kuyapata kama kocha ni kuchukua kombe la FA la Morocco akiwa na Hassania mwaka 2019, vilevile akiwa mkurugenzi wa ufundi wa Wydad Casablanca aliiwezesha kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Morocco.
Mbali na Gamondi, pia hata kocha msaidizi imelazimika kusaka baada ya kuachana na Cedrick Kaze ambaye mkataba wake umemalizika na kuingia mkataba na Moussa N’Daw. Pia italazimika kusaka kocha mpya wa makipa baada ya kuagana na Milton Nienov.

AZAM
Azam itakuwa na benchi jipya la ufundi litakaloongozwa na Youssouph Dabo ambaye atakuwa na faida kidogo kutokana na kuwahi kutua nchini akishuhudia baadhi ya michezo na kuwaona wachezaji wake. Kocha huyo atasaidiana na Bruno Ferr.
Mbali na ugeni wake pia wasaidizi wengine wa benchi la ufundi la Azam FC ambao ni wapya mi Khalifa Ababakar Fall ambaye ni kocha wa makipa, Ibrahim Diop (mchambuzi wa viwango) na Jean-Laurent Geronimi atakayehudumu kama mtaalamu wa mazoezi ya viungo.

MTIBWA SUGAR
Licha ya kocha wao kupambana kuibakiza timu kucheza msimu ujao, inaelezwa Mtibwa Sugar wapo kwenye mchakato wa kusaka kocha mkuu mpya ambaye atakiongoza kikosi hicho kufanya vizuri msimu wa 2023/24.

TANZANIA PRISONS
Baada ya Tanzania Prisons kuibakiza Ligi Kuu msimu ujao ikiponea tundu la sindano, Mohammed Abdallah ‘Bares’ ambaye alichukua mikoba ya Patrick Odhiambo, kocha huyo ametimka kwa makubaliano maalumu.
Bares ambaye alirudishwa Prisons akitokea Mlandege aliyoipa ubingwa wa Mapinduzi msimu huu ametimkia Mashujaa FC iliyopanda Ligi Kuu Bara, hivyo timu hiyo ya Wajelajela imenasa saini ya Fred Felix ‘Minziro’ aliyemaliza mkataba na Geita Gold.

COASTAL UNION
Tangu aondoke Juma Mgunda, Coastal Union haijawa na uvumilivu wa kukaa na makocha baada ya kubaki kucheza Ligi Kuu msimu ujao ikiwa na Fikiri Elias, tayari imeshamvunjia mkataba. Wakati wakimtimua kocha huyo tayari inasemekana wapo kwenye mchakato wa kumalizana na aliyekuwa kocha wa Simba, Goran Kopunovic baada ya aliyemtarajia Abdihamid Moallin kutua KMC.

GEITA GOLD
Baada ya kuipa mafanikio Geita Gold kwa kufanya vizuri misimu miwili mfululizo akiipa nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/23 na kumaliza nafasi ya tano uliofuata, kocha Fredy Felix ‘Minziro’ aliondoka baada ya mkataba wake kuisha.
Na sasa timu hiyo inatajwa kuwa kwenye mazungumzo na Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyetoka kutwaa taji la Ligi Kuu Zanzibar akiwa na KMKM, anatarajiwa kurudi tena Bara kuinoa Geita Gold.

MASHUJAA
Mashujaa msimu ujao utakuwa wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Mbeya City kwa jumla ya mabao 4-1 katika mechi za mtoano (play off) ikiwa chini ya Abdul Mingange.
Mingange ambaye anasifika kwa kupandisha timu anapishana na Mohammed Abdullah ‘Baresi’ ambaye ametangazwa kuinoa timu hiyo msimu ujao.

KITAYOSCE
Timu hii imepanda daraja msimu huu ikipishana na Ruvu Shooting na Polisi Tanzania zilizoshuka pamoja na kuongezwa na kocha mkuu Henry Mkanwa ambaye aliipandisha Kutoka Championship, inasemekana anaweza kufukuzwa muda wowote na kutafutiwa mbadala wake.
Hivyo timu hiyo itaanza msimu mpya ikiwa na benchi jipya la ufundi pamoja na upya kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao, ikielezwa ipo mbioni kuleta kocha kutoka Ulaya.

KMC
Licha ya Kaimu kocha mkuu wa KMC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kufanikiwa kuibakiza timu hiyo baada ya kupewa mkataba wa miezi sita, tayari ameachana na timu hiyo ambayo imemtupia virago.
Julio alijiunga na KMC kuchukua mikoba ya Thierry Hitimana, itacheza Ligi Kuu msimu wa 2023/24 ikiwa na kocha mkuu mpya Abdulhimid Moallin aliyewahi kuinoa Azam ambaye ametangazwa katikati ya wiki hii.

SOMA NA HII  WAKATI SIMBA NA YANGA ZIKISAJILI MASTAA WENGI WA KIGENI...BODI YA LIGI WAIBUKA NA HOJA YA KUWAPUNGUZA...