Baada ya kuripoti juu ya kutoweka kambini kwa Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, kocha huyo amevunja ukimya na kufafanua juu ya ukweli wa taarifa hiyo akikiri atakuwa nje ya timu kwa muda wa wiki moja.
Awali tulipenyezewa taarifa kwamba Robertinho alikuwa ameondoka kambi ya timu hiyo iliyopo jiji la Ankara Uturuki ili kwenda darasani kusoma, lakini akizungumza jana alisema sio anaenda kusoma bali anaenda kuwanoa makocha nchini kwao Brazili kwani yeye ni mkufunzi.
Kocha huyo aliyetua Msimbazi mwisho mwa msimu uliopita na kuiwezesha kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Yanga, huku ikiifunga mabingwa hao mabao 2-0, alisema amerudi kwao Brazili kwenda kutoa darasa kwa makocha wa nchini humo.
“Ni kweli sipo na timu nipo Brazil, lakini nina ruhusa maalumu kwa uongozi. Nitakuwa huku kwa wiki moja kwa ajili ya kuwanoa makocha na sio kusoma,” alisema Robertinho aliyewahi kuzinoa Rayon Sport na Vipers, aliyeongeza;
“Majukumu ya timu kwa sasa yapo chini ya kocha Ouanane Sellami akisaidiana sambamba na kocha wa viungo naamini timu itakuwa sawa, kwani wachezaji wanafanya zaidi mazoezi ya viungo na nimeacha programu nyingine za kufanya.”
Simba ipo Uturuki ikiwa ni kambi ya maandalizi ya msimu mpya ikitarajiwa pia kucheza mechi zisizopungua tatu kabla ya kuja kuwasha moto kwenye Tamasha la Simba Day itakayofanyika Agosti 6 kisha kwenda kucheza mechi za Ngao ya Jamii kufungulia msimu mpya wa Ligi Kuu Bara itakayoanza Agosti 15 kisha kuanza jukumu la mechi za kimataifa za CAF litakaloanza Agosti 18.