KOCHA wa viungo wa Simba, raia wa Rwanda, Corneille Hategekimana ametoa onyo kali kwa wapinzani katika Ligi Kuu Bara wakiwemo Yanga na kutakuwa na balaa zito watakapokutana kwa msimu mpya wa mashindano.
Amesema anashangazwa na uwezo mkubwa wa wachezaji wa timu kuweza kuelewa haraka mbinu za mazoezi wanayowapa pamoja na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliviera (Robertinho).
Mtaalam huyo ametoa kauli hiyo kufuatia kuanza kazi rasmi ndani ya kikosi hicho kufuatia kambi ya walioweka nchini Uturuki kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
Kocha huyo wa viungo alisema wamepata sehemu nzuri yenye ubora mkubwa wa kufanya maandalizi na tangu wamefika nchini humo ni siku nne ambazo wamefanya mazoezi kwa wachezaji kuonekana kuelekea kwa haraka.
Alisema licha ya kutokamilika kwa wachezaji wote ndani ya kikosi anaimani kubwa mwisho ya Pre Season watakuwa vizuri zaidi , utimamu wa mwili, kiufundi na mbinu za uwanjani.
“Tangu tumefika hapa tulifanya maziezi ya viungo Gym , tukaenda kwenye bwawa la kuongela ambalo kuna mazoezi yake ni muhimu na kumjenga mchezaji utimamu wa mwili na tumekuwa na programu ya uwanjani kwa kocha Robertinho kuanza kufanya majukumu ya mbinu na ufundi.
Tuko na timu nzuri sana wachezaji wameonyesha kuelewana vizuri kwa kile kinachotolewa kutoka kwetu wanajua nini wanatakiwa kufanya wanapokuwa na mpira au hawana mpira jinsi ya kujilinda na mpinzani, huko mbele kutakuwa na kazi kubwa kwa wapinzani ,” alisema Hategekimana.