Home Habari za michezo BANGALA AFUNGUKA MAZITO KABLA YA KUSEPA, HUYO MRITHI WA MAYELE ANAMTIHANI HUU...

BANGALA AFUNGUKA MAZITO KABLA YA KUSEPA, HUYO MRITHI WA MAYELE ANAMTIHANI HUU HAPO YANGA

KUTOKANA na kiwango alichokionyesha Fiston Mayele ndani ya misimu miwili akiwa Yanga ni kama ameacha mtihani mkubwa kwa mrithi wake kuhakikisha anaisaidia klabu kwenye nyakati zinazohitaji majibu.

Kiraka wa Yanga, Yanick Bangala aliweka wazi anayekuja kuchukua nafasi ya Mayele atakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha heshima yake inalindwa, kwani atahitaji kujitengenezea CV yake mbele ya mashabiki ambao walipenda kazi ya mtangulizi wake (Mayele).

Ndani ya misimu miwili ya Ligi Kuu Bara, Mayele alifunga jumla ya mabao 33 (2021/22, mabao 16) na (2022/23, mabao 17), ukiachana na hilo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) alikuwa mfungaji bora alimaliza na mabao saba timu yake akiifika fainali ya michuano hiyo.

Mbali na hilo, ikumbukwe Mayele ndiye alikuwa mchezaji bora wa msimu wa 2022/23, alichukua tuzo ya mfungaji bora, kikosi bora na bao bora, jambo ambalo Bangala analiona ni mtihani mkubwa kwa mrithi wake.

Bangala alisisitiza: “Mayele kaacha mtihani mkubwa kwa straika anayekuja nyuma yake, kiwango chake kilikuwa juu, hata sisi wachezaji tulikuwa tunajiamini kupata ushindi akiwepo uwanjani, alikuwa anajua afanye nini na kwa wakati gani.
“Mashabiki walikuwa wanampenda kutokana na kile alichokuwa anakifanya, walijua kabisa akiwepo lazima watacheka na kutetema, sasa anayekuja nyuma yake atakuwa na kazi ya kuwaaminisha wamepata mtu sahihi.”

Ukiachana na Mahop anayetajwa, Bangala anaamini uwepo wa Kennedy Musonda akipewa nafasi nzuri na akajituma anamuona ni straika ambaye anaweza akaisaidia Yanga kwenye mashindano mbalimbali ya msimu ujao.

“Musonda ni straika mzuri, anajiamini na apewe utulivu na mashabiki hapo wajifunze jambo wapende sana timu yao kuliko mchezaji ambaye anapita ndani ya timu, hilo litawafanya wawe na amani yanapotokea mabadiliko yoyote,” alisema Bangala ambaye anaondoka kwenye timu hiyo.

SOMA NA HII  YANGA WAANZA VISIGIZIO MAPEMA