Home Habari za michezo BANGALA AFUNGUA KILA KITU, KUHUSU KUTUA AZAM, AWATAJA MAXI, SKUDU, TUHUMA ZAKE...

BANGALA AFUNGUA KILA KITU, KUHUSU KUTUA AZAM, AWATAJA MAXI, SKUDU, TUHUMA ZAKE NA SIMBA

yannick

KIRAKA anayeondoka Yanga, Yannick Bangala
amefanya mahojiano na akatoa mengi ya moyoni lakini akawapa fundisho mashabiki huku akigusia usajili wa Maxi na Skudu.

Lakini amezungumzia pia tuhuma za kwamba aliwahi kudaiwa ameihujumu Yanga kwenye mechi ya watani wa Jadi.
Staa huyo raia wa DR Congo, anafurahia jinsi mashabiki wanavyotoa sapoti kwa wachezaji kuhakikisha wanajisikia vizuri na wanapata morali ya kujituma zaidi, lakini amewashauri kupenda zaidi timu kuliko mchezaji, kiongozi ama mtu binafsi ili wasiumie anapoondoka mtu kama yeye, Djuma Shabaan au Fiston Mayele.

“Sisemi hilo kwa ubaya, maisha ya wachezaji, makocha na viongozi ni ya kupita, hivyo wakimpenda mtu kupita kiasi akiondoka yanakuwa yanabakia maumivu makubwa kwenye mioyo yao, ni kweli wanafanya kazi kubwa kutupa sapoti ila waipende klabu maana hiyo ni yao milele,”anasema na kuongeza;

ALSO READ
Mrithi wa Mayele atambulishwa Yanga
Soka 1 hour ago
“Mashabiki wa Simba na Yanga wamebeba hisia kali sana, kiasi kwamba mchezaji wa upande wa pili wakikuona naye wanaweza wakawa wanakufikiria vibaya wakati nje ya uwanja tuna maisha ya undungu ama kama vijana tunaweza tukabadilishana mawazo ya hapa na pale,”anasema. Amewataka mashabiki wapunguze kupenda watu binafsi.

Kuhusu usajili wa Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ kwamba pamoja na vituko anavyofanya vinavyowafanya mashabiki kumuona hajatulia ni mchezaji mzuri anayeweza kuisaidia sana Yanga.

“Ni kweli ana vituko sana, kiuwezo ni mchezaji mzuri kama ninavyosisitiza wachezaji wapewe utulivu na nafasi watafanya mengi yenye manufaa kwa klabu,”anasema.

Huyo Maxi Mpia aliyesajiliwa kutoka AS Maniema Union ya DR Congo anasema ni hatari, kikubwa alichokiomba ni mashabiki, kocha na viongozi kumpa utulivu wa kutimiza majukumu yake na wawe makini pia kwenye mapenzi yaliyopitiliza.

“Nakumbuka wakati nipo AS Vita niliwahi kumwambia kocha wangu amsajili Max na Aziz Ki ni wachezaji wazuri sana,ikashindikana kwa sababu Maxi alikuwa tegemeo kwenye klabu yake, pia wakati wa Nabi nilimshauri hivyo hivyo.

“Kabla ya kumsainisha Maxi rais wa klabu, Injinia Hersi Said aliniita ofisini kwake akaniuliza unamuonaje mchezaji huyo ni mzuri nikamwambia ndio nikamuelezea ufundi wake, nafurahia anaichezea klabu kubwa ambayo kiwango chake kitakuwa msaada mkubwa,”anasema.

MAXI NI ZAIDI YA FEI?
Bangala ambaye anadai ndoto yake ilikuwa ni udaktari akachemka kusoma baada ya kunogewa na soka, anasema uwezo wa Maxi anaamini ataziba pengo la Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anaitumikia Azam “Japokuwa Fei Toto tayari ameonyesha uwezo wake,ila naamini Maxi kama ataondoa presha atafanya makubwa ambayo mashabiki watajionea wenyewe.”

Anamzungumzia Fei Toto aliyekuwa anamfundisha Kiswahili, kwamba ana vituko sana tofauti na mtazamo wa wengi kumuona mpole anayeweza kuishi na kila mtu.

MBONA BADO YUPO DAR?
“Naheshimu mkataba wangu, ndio maana nasisitiza ni mali ya Yanga, nina mambo ambayo napaswa kumalizana mimi na mabosi wangu, hivyo siwezi kuyaweka wazi,” Mwanaspoti linajua kwamba staa huyo anasubiri malipo yake ya kusitishiwa mkataba.

TUHUMA ZAKE DHIDI YA SIMBA
Anasema katika maisha yake amecheza dabi nyingi kabla ya kuja Yanga na timu zenye mashabiki wa kutosha, ila mechi ya watani wa jadi anaiona ni ya tofauti kwa namna inavyochukuliwa na jamii.
“Kwanza kama mchezaji ni muoga unaweza ukaogopa kucheza mechi na ukadanganya unaumwa, kwani matangazo ni mengi ambayo yanakuwa yanaleta presha kubwa sana, kwa upande mwingine ni mechi ambayo mchezaji mkubwa inakupa heshima ya kuonyesha ukubwa wako.

“Changamoto nyingine tangu nilipojiunga na Yanga tumeifunga Simba mara nyingi,viongozi walikuwa na raha kila mmoja anamsifia mchezaji, siku ambayo tumefungwa kila mmoja anaingilia mlango wake, baadhi wanakwenda mbali zaidi kuwatuhumu wachezaji kama wamechukua pesa upande wa pili jambo ambalo siyo kweli, kikubwa unapuuza.”

“Mimi binafsi yalinikuta tulipopoteza dhidi ya Simba nilisikia Kuna kelele kwamba nimechukua fedha lakini kwakuwa sio kweli hazikunisumbua kichwani kwangu niliziacha na kuendelea na kazi yangu.”

Anazitaja timu ambazo amecheza zina dabi na mashabiki wengi ambazo ni FC Les Stars, Motema Pembe na AS Vita za nchini kwao Congo na FAR Rabat ya Morocco.
“Pamoja na hayo mkifungwa mashabiki na viongozi walichukulia ni moja ya matokeo, ila huku ni tofauti kidogo, lazima utasikia Bangala hajakaba vizuri, kipa kafanya kile,”anasema.

MAFANIKIO YAKE YANGA
“Naanza na mafanikio ya uwanjani, msimu wa kwanza kucheza Yanga ulikuwa wa mafanikio makubwa sana, nilicheza nafasi nyingi uwanjani na kujitolea. Msimu wa pili haukuwa mzuri sana kwangu, kwa sababu nilichoka kutokana na kutumika sana msimu uliopita, hivyo kocha Nabi akawa ananipa muda mwingi wa kupumzika kwa ajili ya kunitumia kimataifa na ilikuwa hivyo ndio maana sikucheza kwa kiwango cha juu kama ilivyokuwa msimu wa kwanza.

“Kila nafasi niliyokuwa nacheza ilikuwa na wachezaji wenye kiwango kikubwa, mfano beki ya kati yupo Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Bacca, kati yupo pia Zawadi Mauya, Mudathir Yahya, Khalid Aucho yaani kila mmoja alikuwa kwenye kiwango kikubwa na unaweza ukaona ni namna gani nilitakiwa kupambana sana kila ninapobadilishwa nafasi.”

ALIKUWA HANA FURAHA?
“Ni maneno ya mashabiki sikuwa na shida yoyote zaidi ya kuchoka kutokana na kutumika zaidi msimu ule wa kwanza na kocha Nabi aliliongea hilo mara nyingi kwenye vyombo vya habari kwamba ananipumzisha.”
Anazungumzia mafanikio ya Yanga kufika hatua ya fainali ya CAF, kwao haikuwa bahati mbaya baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa kwani walifanya kikao cha kuhakikisha wanaitumia nafasi nyingi kuonyesha uwezo wao.

“Kwanza mchezaji yeyote anayejitambua kitu cha kwanza anatamani kucheza michuano ya CAF, baada ya kufanya kikao na viongozi, tukafanya chetu wenyewe kama wachezaji kwamba lazima tupambane tuchukue taji la Afrika tuliweka juhudi za kushinda kila mchezo wa nyumbani na ugenini na hatimaye tukafika Fainali ni bahati mbaya tu tumelikosa taji kutokana na kanuni likaenda kwa wapinzani wetu USM Alger,”anasema na kuongeza;

“Kiujumla ulikuwa msimu wa aina yake, kutokana na jinsi tulivyokusanya mataji kuanzia Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi Kuu Bara hivyo nadhani imeongeza kitu kikubwa sana kwenye karia yangu ya soka.”

YANGA IMEMPA GHOROFA
Anasema kabla ya kuja Yanga, alikuwa amenunua nyumba, lakini ndani ya miaka miwili aliyokaa kwa Wana Jangwani amejenga nyumba ya ghorofa mbili, anakiri viongozi walikuwa wanawajali na alizitumia kwa akili bonasi walizokuwa wanapewa.

“Nina hatua ya maendeleo kupitia Yanga, ujue kila mchezaji ana akili yake ya kutunza pesa na kufanya vitu vya maana, pesa za bonasi zimenisaidia hivyo bado kidogo namalizia nyuma yangu ya ghorofa mbili sijaimalizia lakini iko mwishoni,”anasema na kuongeza;

“Viongozi wanafanya kazi yao vizuri ya kuhakikisha wachezaji tunapata ahadi zao, vinginevyo tusingekuwa tumecheza kwa kiwango kikubwa namna ile ndani ya misimu miwili mfululizo.”

KADI NYEKUNDU MOJA TU
Licha ya Bangala kucheza nafasi za kukaba (5, 6) anasema katika maisha yake yote amewahi kupata kadi nyekundu moja mwaka 2018 zilikuwa fainali za CAF walicheza dhidi ya Raja Casablanca.

“Aina yangu ya uchezaji siwezi kupata kadi hovyo kwani nacheza tachi mbili, hata ikitokea nikapata njano huwa naumia sana na wala kocha hawezi kunilaumu kwani inakuwa ya faida, mfano unaona ukiacha kumkaba zaidi anakwenda kufunga,”anasema.

SOKA LA TANZANIA BAB’ KUBWA
Anasema sio mchezo Ligi Kuu Bara kuingia kwenye ligi bora tano Afrika (TOP 5), anaiona ni tafsiri kubwa ya soka kukua, huku akilipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kulipambania na kuhakikisha linakuwa juu.

“Ndio maana wachezaji wengi wazuri kutoka mataifa mbalimbali wapo hapa, kwani ni soka linalotazamwa na nchi mbalimbali, klabu na TFF wanafanya kazi nzuri sana,”anasema.
Mbali na hilo, anazungumzia namna alivyoumia kwa kuitazama

‘Yanga Day’ kwenye televisheni “Mimi bado ni mchezaji wa Yanga yapo mambo ambayo napaswa kuyaweka sawa na viongozi wangu, ila kama mchezaji nilikuwa nawaza na mimi ningekuwa kwenye furaha ambayo wenzangu walikuwa wanapata, ila ndio soka.
“Jinsi ambavyo niliona mechi ya Yanga na Kaizer Chiefs wachezaji walijitahidi kuonyesha uwezo wao, nadhani kocha ataongeza nguvu kwenye kombinesheni na kwa usajili huo naona bado tuna nafasi ya kunyakua taji, ingawa nimeona hata wapinzani wetu wanasajili vizuri,”anasema.

GSM APEWE MAUA YAKE
Anasema kwake anamuona Ghalib Said Mohamed (GSM) kama baba yake kutokana na alivyowachukulia wachezaji, akimpa maua yake kwamba sio muongeaji, mpole na anatokea kwenye matukio makubwa na maalumu.

“Kwanza siyo muongeaji mpole sana, mkiwa na majukumu makubwa mbele yenu, anakuja kutoa ahadi yake na mkifanikiwa anatimiza, kutokana na ukimya wake ni ngumu sana kumzoea, ingawa ni kama baba namna anavyoishi na wachezaji,” anasema na kuongeza;

“Hata uwanjani nadhani anakuja mechi kubwa ambazo anakuwa anatupa moyo kwamba tunaweza kufanya makubwa, ila ni mtu safi sana.”

Ukiachana na Ghalib pia kuhusu injinia Hersi hana tatizo naye, kwani ni bosi wake na urafiki wake upo kikazi zaidi “Sina tatizo kabisa na rais urafiki wetu ni kazi zaidi, nadhani kubwa ni hilo.”

KUMBE SIMBA,AZAM ZILIMSAKA
Kuna kipindi kulivuma taarifa za kuhitajika na Simba na Azam, analizungumzia hilo kwamba mchezaji yeyote anayefanya vizuri, lazima atafuatwa na klabu kama hizo, hasa kipindi ambacho aliibuka mchezaji bora wa msimu (2021/2022).

“Ni kawaida kufuatwa na timu kama hizo, kwani ligi ina ushindani lazima watatafuta wachezaji wazuri, pamoja na hayo yote lakini niliwasisitiza bado ni mchezaji wa Yanga na nina mkataba, hivyo siwezi kuzungumza timu nyingine labda wawafuate viongozi wa Yanga,”anasema.

SIRI YA WAKONGO KUTOBOA
Kulingana na maisha ya nchini kwao, anasema mchezaji anapopata nafasi ya kwenda kucheza taifa lingine hafanyi mchezo kwani anakuwa anapambana kwa ajili ya ndugu zake aliowaacha nyuma.

“Nadhani kama kuna taifa linaongoza kwa watu wao kwenda nchi mbalimbali, ikiwemo Ulaya basi ni Wakongo, tunajua aina ya maisha yetu hivyo hatuwezi kuchezea fursa hata kidogo, pia tuna moyo wa kujituma na kupambana sana, ndio maana unaweza ukaona tunafanikiwa sana sehemu tunazokuwepo na siyo soka pekee, angalia hata wanamuziki,”anasema na kuongeza;

“Familia zetu sio za kitajiri na tunategemea nguvu zetu ili kuishi vizuri na tunaacha ndugu wengi wanaotutegemea hvyo hatuwezi kufanya jambo au kazi kwa ulegevu hivyo ndivyo tulivyo.”

MAISHA NJE YA UWANJA
Ni kweli Yanga ilikuwa na Wakongo wengi lakini pia Simba, wanachukuliana kama ndugu nje ya mpira, ila kinachomtisha zaidi ni ushabiki uliopo baina ya klabu hizo mbili.

“Ni kama vita ushabiki wao, wanaweza wakakuona na mchezaji wa Simba unaanza kudhaniwa tofauti na kukuona labda una namna ya kuhujumu timu, ila siyo kweli ili kuepusha vitu tunakuwa tunakaa mbalimbali labda kuwe na tatizo kubwa sana,”anasema.

SOMA NA HII  TSHABALALA,KAPOMBE HALITETE WASAIDIWE