Home Habari za michezo BOCCO PASUA KICHWA AWAVURUGA VIONGOZI WA SIMBA, HUKU ISHU YA BALEKE NAYO...

BOCCO PASUA KICHWA AWAVURUGA VIONGOZI WA SIMBA, HUKU ISHU YA BALEKE NAYO IKO HIVI

Habari za Simba

WAKATI mabosi wa Simba wakiweka sawa ishu ya mkataba wa Jean Baleke na TP Mazembe lakini wapo kwenye mjadala mzito unaowapasua vichwa namna ya kuachana na Nahodha wao John Bocco.

Hadi sasa, Simba wamekamilisha usajili wa mastaa wawili wa kigeni huku wakimaliza utata wa mshambuliaji wao Baleke aliyekuwa akidaiwa ana mkataba wa TP Mazembe.

Usajili mpya wa Simba uliokamilika na kutangazwa hadi sasa ni Aubin Kramo na Willy Essomba Onana huku wakiimarisha benchi la ufundi kwa kuwaajili makocha wa makipa Daniel Cadena na viungo Corneille Hategekimana pamoja na Meneja ambaye pia ni Mkuu wa Sayansi ya michezo Mikael Igendia.

Pia wakati wowote watatangaza usajili wa mastaa wao wengine wapya ambao ni kipa Mbrazil, Caique Luiz Santos da Purificao na tayari wameshamtambulisha beki Mcameroon Che Fondoh Malone.

Kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa kulikuwepo na taarifa juu ya mshambuliaji wao Baleke kuwa anahitajika kurejea kwenye timu yake ikidaiwa kuwa Simba hawakumaliza malipo yake ya mkataba wa mkopo wa miaka miwili kwani ulilipwa mwaka mmoja.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Simba ambao baada ya kumsajili waliwahi kutangaza kuwa yupo kwa mkopo, kuwa tayari mabosi hao wamemalizana na TP Mazembe hivyo ataendelea kuwa ndani ya Simba hadi msimu ujao.

Baleke ambaye alimaliza msimu wa ligi akiwa amefunga mabao nane nyuma ya Moses Phiri na Bocco waliofunga mabao 10 kila mmoja.

Kuhusu Bocco, inaelezwa kuwa ndani ya Simba kuna makundi mawili, moja linataka straika huyo mkongwe aliyemaliza msimu na mabao 10 abaki ndani ya timu wakitoa sababu zao na wengine wakishinikiza aachwe ili timu itengenezwe upya kwa kuwaondoa wakongwe wote.

Inadaiwa kuwa Bocco hata wakati wenzake wanafanyiwa vipimo na kuweka alama za kidole kwa ajili ya safari ya kwenda Uturuki kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya hadi jana hakufanya vyote hivyo, kitu ambacho kiliibua maswali mengi.

“Suala la Baleke lipo vizuri, bado ataendelea kuwepo Simba, tayari Mazembe wameishamaliziwa pesa yao, hakuna maneno tena,” alisema kiongozi huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba na kuongeza;

“Kuhusu Bocco, wanaotaka aondoke wanatoa sababu zao kuwa timu ianze upya kutengenezwa hivyo wakongwe wote waondolewe lakini wale wanaotaka abaki sababu zao kubwa ni kwamba kwanza ni Nahodha, amefunga mabao mengi msimu uliopita pia timu lazima ibaki na wakongwe,” alisema

Hata hivyo, changamoto nyingine iliyotajwa kuwa akiondolewa Bocco ni namna ya kumpata mshambuliaji wa kariba ya Bocco ambaye ni mzawa.

“Unajua pia tunajadiliana kuwa akiachwa ni lazima tusajili mshambuliaji mzawa lakini kwasasa unampata wapi, hilo ni tatizo pia kwetu, hatuwezi kusajili wa kigeni, hivyo hatujafikia muafaka juu ya Bocco bado tunabishana ila lolote linaweza kutokea na wakati wowote juu yake.”

Simba sasa eneo la mbele linazidi kuimarika zaidi kwani kuna nyota wengine waliosajiliwa na waliokuwepo kama Bocco, Phiri, Kibu Denis, Saido Ntibazonkiza (mfungaji bora msimu uliopita akifunga mabao 17), Pape Sakho, Kramo na Onana ambaye msimu uliopita amefunga mabao 16 Ligi Kuu Rwanda.
Msimu uliopita safu ya ushambuliaji ya Simba ndiyo iliyoongoza kwa ufungaji wa mabao wakifunga jumla ya mabao 58.

Alipoulizwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally alisema kuwa; “Kila kitu tunafanya kwa utaratibu, hivyo kama kuna taarifa yoyote kuhusu Bocco na wengineo itatolewa ila ifahamike kwamba Nahodha wetu bado ana mkataba wa mwaka mmoja.”

SOMA NA HII  GAMONDI AISHTUKIA SIMBA MAPINDUZI CUP ....AWAITA MASTAA WOTE ALIOWATOSA DAR...