Home Habari za michezo MTEGO WA MAYELE YANGA SASA HADHARANI

MTEGO WA MAYELE YANGA SASA HADHARANI

Habari za Yanga leo

NYOTA wa zamani wa kimataifa waliowahi kuwika Simba na Yanga, Edibily Lunyamila na Dua Said wameanika mtego ulioachwa na Fiston Mayele ndani ya Yanga wakidai unaweza kumtesa straika anayesajiliwa kuziba pengo la Mkongomani huyo anayeondoka.

Yanga inatarajia kuanza maisha bila huduma ya Mayele aliyemaliza akiwa kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara sambamba na Saido Ntibazokiza wa Simba kila mmoja akifunga mabao 17 na pia kinara wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kutokana na kuuzwa Pyramids ya Misri.

Wakati mashabiki wakitamani kufahamu mrithi ataletwa kutoka nje kuchukua nafasi ya Mayele, mastaa wa zamani akiwamo pia Abdallah Kibadeni wamefunguka namna Yanga ilivyoachiwa mtihani na straika huyo aliyefunga jumla ya mabao 33 katika Ligi Kuu kwa misimu miwili.

Winga wa zamani wa Yanga na Simba aliyetamba pia Malindi na Taifa Stars, Lunyamila alisema kumpata mbadala wa Mayele ni ngumu kwani hakuwa na mpinzani kikosini, hivyo ni lazima anayekuja awe mkali zaidi ya mshambuliaji huyo.

Lunyamila alisema Mayele hana anachodaiwa na Yanga kwa vile amefanya kazi kubwa, lakini kumpata atakayefanya makubwa zaidi yake au kama yeye ni fumbo.

“Yanga haitabomoka kumkosa mtu kama Mayele kwani ina viungo wengine na kuondoka kwake ni jambo sahihi na itawapa nafasi waliopo kuonyesha kile walichokuwa nacho. Mashabiki wasiwe na hofu mpira ndivyo ulivyo wasishangae Musonda anakwenda kuwa hatari zaidi ya Mayele au mwingine yeyote, hivyo wasihofu kikosi kitaendelea kufanya vizuri kwani wapo walio bora pia,” alisema, huku Kibadeni akisema mpira ni kazi kama zilivyo zingine na anayekuja ana kazi ya kujitambua kama alivyokuwa Mayele ili aweze kufanya makubwa.

“Mayele alifanikiwa kwa kujielewa kwake na sio kingine, hivyo mrithi wake akiweza kujitambua kuwa anatakiwa kufanya nini, basi Yanga itakuwa imepata mafanikio,” alisema.
Dua alisema mrithi wa Mayele anatakiwa kufanya makubwa zaidi ya straika huyo, kwani atakuwa akiangaliwa sana ili kuona nini anafanya.

“Yanga ni timu yenye mashabiki wengi wanahitaji mchezaji bora, hivyo ubora ndio unaohitajika zaidi kwa huyo mrithi kwani ni lazima alete matokeo mazuri uwanjani,” alisema Dua.

SOMA NA HII  MAJANGA HAFIZ KONKANI AGOMA KUVAA VIATU VYA MAYELE, ISHU IKO HIVI