Home Habari za michezo HIKI WANACHOFANYA YANGA SASA NI KUKOMOA

HIKI WANACHOFANYA YANGA SASA NI KUKOMOA

Gift Fred atambulishwa Yanga

HIKI kinachofanywa na Yanga sasa ni kukomoa. Baada ya kushusha winga kutoka DR Congo, Maxi Nzengeli aliyetoke AS Maniema anayesifika kwa chenga, kasi na kufunga.

Lakini, wakamtambulisha kiungo mshambuliaji mpya aliyetoka kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, Pacome Zouzoua, huku mashabiki wa klabu hiyo mtandaoni wakitamba wakiuliza “mna beki ya kuwazuia.”

Ipo hivi. Yanga inaendelea kujifua kambini Avic Town Kigamboni – Dar es Salaam ikijiandaa na mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kuhitimiska kilele cha Wiki ya Mwananchi itakayofanyika keshokutwa Jumamosi, lakini mabosi wa klabu hiyo wameendelea kuibomoa Asec Mimosas ya Ivory Coast kwa kumchukua staa mwingine fundi anayejua kufunga na kupiga pasi za mabao, Pacome.

Pale Asec Pacome ndiye kiungo mshambuliaji ambaye aliziba nafasi ya Stephanie Aziz KI aliyesajiliwa na Yanga na sasa wote wanaungana Jangwani.

Akiwa amefunga mabao matano sawa na mshambuliaji wa timu yake, Sankara Karamoko kwenye ligi ya kwao, kiungo huyo fundi anayejua kupiga chenga na pasi za maana aliibuka mchezaji bora wa ligi.

Pacome alimzidi mshambuliaji Giby Gauthier aliyekuwa mfungaji bora akifunga mabao manane katika kinyang’anyiro hicho akikabidhiwa gari mpya dogo kwa tuzo hiyo, akiisaidia Asec kuchukua ubingwa na pia kufika hatua ya robo fainali.

Ujio wa mchezaji huyo utazidisha vita katika eneo la kiungo ambapo raia huyo wa Ivory Coast atapigania namba na Aziz KI kucheza kiungo mshambuliaji wa juu.

Yanga itasubiriwa kujua itamkata nani kufuatia kuingia kwa Pacome, huku nafasi kubwa ya kukatwa inaweza kuangukia kwa Yannick Bangala.
Bangala bado hajajiunga na timu, lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba kiungo huyo yupo kwenye sintofahamu kufuatia mabosi wa Yanga kumkalia kooni kwa madai ya makosa ya utovu wa nidhamu.

Pacome anakuwa staa wa tatu ndani ya Yanga kutua Tanzania akitanguliwa na Aziz KI, beki Kouassi Yao, lakini katika Ligi Kuu Bara ni wa nne ambapo tayari Simba ilishamchukua winga wa kulia Kramo Aubin, ambaye alikuwa mfungaji bora wa timu hiyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita

SOMA NA HII  SIMBA MBONA INAFUZU KIBOSI TU.... AKILI YA ROBERTINHO IKO HIVI