Home Habari za michezo ROBERTINHO ATAMBA KUHUSU MSIMU UJAO,… LUIS MIQUISSONE ATAJWA

ROBERTINHO ATAMBA KUHUSU MSIMU UJAO,… LUIS MIQUISSONE ATAJWA

Habari za Simba SC

SIMBA imeendelea kujifua nchini Uturuki kwaajili ya msimu mpya huku kocha mkuu wa kikosi hicho Roberto Oliveira akitamba kutisha zaidi msimu ujao.

Robertinho juzi alipata picha kamili ya kikosi chake cha msimu ujao baada ya kutua kambini kwa Winga hatari Luis Miquissone aliyerejea Simba akitokea Al Ahly ya Misri alikovunja mkataba.
Kutua kwa Miquissone kumekifanya kikosi cha Simba kukamilika akiwa mchezaji mpya wa 10 kutua kambini hapo na kufunga hesabu zote kwaajili ya msimu ujao.

Wachezaji wengine wapya waliosajiliwa Simba msimu huu ni wazawa, David Kameta ‘Duchu’, Abdallah Hamis, Hussein Bakari ‘Kazi’ na Shaban Chilunda huku wageni wakiwa kipa Mbrazil Jefferson Luis, Mcameroon Che Malone Fondoh, Muivory Coast Aubin Kramo, Mkongomani Fabrice Ngoma na Mcameroon Willy Onana.

Akizungumza na Mwandishi, Robertinho alisema kwa sasa chama lake limetimia na kazi imebaki kwake na wasaidizi wake katika benchi la ufundi kuandaa kikosi cha mauaji kwa msimu ujao waliopanga kuchukua makombe yote ya ndani na kufika walau nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Wachezaji wote wapo, sasa kinachoendelea ni sisi kuelekeza na kufundisha mbinu za namna tutakuwa tukicheza msimu ujao katika mechi zetu kwa namna tofauti tofauti.

Simba ya msimu ujao nataka iwe ngumu kufungika lakini pia iwe imara kwenye kutengeneza mashambulizi na bora kwenye kutumia nafasi jambo ambalo hadi sasa tupo kwenye hatua nzuri na tunaendelea kufanyia kazi hilo,” alisema Robertinho.

Alisema timu yake inaweza ikacheza mechi mbili nyingine za kirafiki kabla ya kurudi Bongo, baada ya ile ya kwanza dhidi ya Zira FC iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 huku bao pekee la Simba likiwekwa nyavuni na Kibu Denis.

“Tunahitaji mechi mbili nyingine kabla ya kurudi Tanzania ili kupima ufanisi wa wachezaji wetu juu ya kile tulichowaelekeza.
Utaratibu wa kupata mechi hizo unaendelea vizuri na tukizipata zitatusaidia kumalizia kambi,” alisema.

VIGOGO WAVAMIA
Wakati Simba ikiendelea na kambi yao huko uturuki, kama sapraizi juzi usiku vigogo wa timu hiyo walitua kambini na kuteta na wachezaji mawili, matatu kubwa zaidi ikiwa kuhamasisha morali.

Waliambatana na Miquissone,miongoni mwao ni Mwenyekiti wa klabu hiyo Murtaza Mangungu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Salim Abdallah ‘Try Again’.
Walitumia kikao hicho kuwakaribisha wachezaji wapya wa Simba na kuwaeleza malengo yao kwa msimu ujao lile la kubeba makombe yote likipewa kipao mbele zaidi.

Pia waliwapa nasaha kadhaa kuhusu utamaduni wa Simba na kuwataka wapambane kadri wawezavyo ili kuhakikisha malengo yote waliyojiwekea yanatimia.

Simba itarejea nchini Agosti mosi mwaka huu ambapo ikifika wachezaji watapewa mapumziko ya siku mbili kisha watarudi kambini kujiandaa na mechi ya sikukuu ya ‘Simba Day’ Agosti 6, 2023 dhidi ya Power Dynamo kutoka Zambia na baada ya hapo kikosi kitasafiri hadi Tanga kwaajili ya mechi za Ngao ya Jamii zitakazoanza Agosti 9, mwaka huu uwanja wa Mkwakwani.

SOMA NA HII  SIMBA WAIFANANISHA AL AHLY NA ZAMALEK