Home Azam FC SIMBA MAJANGA MATUPU KWA UPANDE WA MASTAA WAZAWA…UKWELI MCHUNGU HUU HAPA..

SIMBA MAJANGA MATUPU KWA UPANDE WA MASTAA WAZAWA…UKWELI MCHUNGU HUU HAPA..

Habari za SImba SC

Simba ina kibarua kigumu cha kufanya katika dirisha hili la usajili linaloendelea kutokana na uhaba wa wachezaji wazawa katika kikosi chake kulinganisha na washindani wake wakuu, Yanga na Azam FC.

Ulinganisho wa vikosi vya timu hizo tatu, unathibitisha kuwa baada ya kupunguza idadi kubwa ya wachezaji katika dirisha hili la usajili, Simba imebaki na kundi dogo la wachezaji wazawa jambo linaloifanya hata ikitengeneza kikosi cha wachezaji wa nyumbani, kulazimika kutumia wale wanaocheza katika nafasi tofauti ili tu nyota 11 watimie na sio kwamba ni nafasi zao asilia.

Hii ni tofauti na Yanga na Azam FC, ambazo zikipanga vikosi vyao vya wachezaji wazawa, hazilazimiki kutumia wachezaji wa nafasi tofauti kwenye nafasi nyingine uwanjani, jambo linaloilazimisha Simba kuhakikisha inatoa kipaumbele pia kwa nyota wa nyumbani.

Utofauti mkubwa wa ubora kiushindani baina ya nyota wa kigeni na wale wazawa, umeifanya Simba kuingia katika dirisha hili na mtihani huo wa kusaka wazawa ambao wataifanya isiwe na presha wakati inapokosa wageni kikosini kulinganisha na Azam FC na Yanga.

Ili kikosi cha wazawa cha Simba kitimie kwa mujibu wa wachezaji waliopo kwenye timu kwa sasa, wapo wachezaji watalazimika kupangwa katika nafasi ambazo wamekuwa hawazichezi mara kwa mara ili tu iweze kutimia 11, jambo ambalo mara nyingi makocha wamekuwa hawalipendelei.

Kikosi cha wazawa cha Simba kinaweza kuundwa na kipa Aishi Manula na mabeki wa pembeni Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na wale wa kati wanaweza kuwa Kennedy Juma na Nassoro Kapama.

Viungo ni Mzamiru Yassin na Jimmyson Mwanuke, mawinga ni Kibu Denis na Mohamed Musa, huku washambuliaji kuwa John Bocco na Habibu Kiyombo.

Katika benchi, Simba inabaki na makipa wawili wazawa, ambao ni Ally Salim na Feruzi Teru pamoja na beki wa kulia Israel Mwenda.

Kikosi cha wazawa cha Yanga kinaundwa na kipa Metacha Mnata na mabeki wa pembeni Dickson Job na Kibwana Shomari, huku mabeki wa kati wakiwa Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca.

Upande wa viungo kuna Jonas Mkude, Mudathir Yahya na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, washambuliaji wakiwa Nickson Kibabage na Denis Nkane, huku mshambuliaji wa kati akiwa Clement Mzize na kwenye benchi itabakiwa na Abuutwalib Mshery, Farid Musa, Crispin Ngushi na Zawadi Mauya.

Azam FC haijapishana sana na Yanga ingawa yenyewe eneo ambalo linaweza kuipa presha ni la golini, kwani italazimika kumtegemea kinda Zuberi Foba, ambaye hana uzoefu wa kutosha ingawa ina wachezaji wenye kiwango bora na uzoefu wa kutosha wa ndani.

Hadi sasa, kikosi cha wazawa cha Azam FC kinaweza kuundwa na Foba, mabeki wa pembeni Nathaniel Chilambo na Edward Charles, huku Lusajo Mwaikenda na Abdallah Kheri ‘Sebo’ wakiwa katika nafasi ya beki wa kati.

Viungo ni Sospeter Bajana, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Yahya Zayd, huku wachezaji wa mbele wakiwa Iddi Selemani ‘Nado’ Abdul Selemani ‘Sopu’ na Ayoub Lyanga.

Katika benchi, Azam FC ina Pascal Msindo, Cyprian Kachwele na Tepsi Evance.

Nyota wa zamani wa Yanga, Ramadhani Kampira alisema kuwa Yanga imefanikiwa kwa wachezaji wazawa kwa sababu inawapa thamani.

“Kwa muda mrefu Yanga imekuwa ikiwapa kipaumbele zaidi wachezaji wazawa na huwa hailazi damu wakati inapomuona mchezaji anayeonyesha kiwango kizuri. Timu nyingine zinapaswa kujifunza katika hilo na kuwapa kipaumbele wachezaji wetu,” alisema Kampira.

Kocha wa soka la wanawake, Edina Lema alisema kuwa kinachoisaidia Yanga ni kundi kubwa la wachezaji wake kucheza mara kwa mara.

“Yanga ina wachezaji bora wanaotumika kuliko Simba na Azam. Karibu nusu ya timu wanapata nafasi. Jambo la msingi ni kuwa hakuna ulazima wa kutumia nafasi 12 za wachezaji wa kigeni kwa sababu hakuna timu inayoweza kupatia katikakusajili wachezaji hao wote.

“Zinaweza kusajili wachezaji saba au nane na nyingine tukajaziwa wachezaji wadogo wazawa wanaoweza kukaa kwenye klabu kwa muda mrefu,” alisema Lema.

SOMA NA HII  WANACHAMA SIMBA WACHARUKA......MANGUNGU,TRY AGAIN WAWEKWA KITIMOTO