Home Habari za michezo SIMBA YAFANYA MAGEUZI NDANI YA WIKI TATU,…. ROBERTINHO ATAMBA

SIMBA YAFANYA MAGEUZI NDANI YA WIKI TATU,…. ROBERTINHO ATAMBA

Habari za Simba SC

Dar es Salaam. Simba imemtambulisha Che Fondoh Malone ikiwa ni hatua za mwisho kumalizia utambulisho wa wachezaji iliowasajili, huku ikiondoka leo kwenda Uturuki itakapoweka kambi ya wiki tatu.

Baada ya Malone, aliyetambulishwa juzi, sasa anayefuata ni kipa Mbrazili Caique de Santos na wachezaji wengine wasiozidi wanne akiwemo beki mmoja na kiungo mmoja wazawa na baada ya hapo watafunga hesabu.

Mwananchi wamejuzwa kuwa kambi ya Simba nchini Uturuki haitazidi wiki tatu, kwani itaanza Jumatano na kurejea mwanzoni mwa mwezi ujao ili kuwahi tamasha lao la ‘Simba Day’ kabla ya mechi za Ngao ya Jamii zitakazochezwa Uwanja wa Mkwakwani, kuanzia Agosti 9, Simba ikianza na Singida Fountain Gate.

Akizungumza jana, Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alitamba kuwa kambi wanayokwenda kuweka Uturuki itakuwa ya mapinduzi na atahakikisha kila kitu cha msingi kinafanyika kabla ya kurejea nchini.

Robertinho anaamini licha ya kuwa wiki tatu ni chache kwenye kujenga timu, lakini atahakikisha anaweka sawa kila kitu akishirikiana na wataalamu wengine kwenye benchi la ufundi ili timu hiyo irudishe ufalme ilioupoteza.

“Ni muda mchache lakini nadhani tutautumia vilivyo kufanya mapinduzi na maboresho ya timu yetu.

“Tutafanyia kazi mambo mengi katika kipindi hicho, ikiwemo utimamu wa miili, umoja, ushirikiano, mbinu na mifumo tutakayoitumia mara kwa mara katika mechi zetu za ndani na kimataifa,” amesema

Robertinho aliyejiunga na timu hiyo katikati ya msimu uliopita akitokea Vipers ya Uganda.

“Tunataka kila kitu tukimalize katika muda huu ili tukirejea tuwe tayari kwa mapambano, tunatambua tutakuwa na mashindano zaidi ya matatu kwa msimu ujao, hivyo lazima tujenge timu imara na yenye watu wenye utayari wa kupambana ili kuwapa furaha mashabiki wetu lakini kubwa zaidi ikiwa ni kutwaa mataji na kufikia malengo.”

Hata hivyo, kocha huyo ameupongeza uongozi wa Simba kwa wachezaji wapya iliowasajili akiamini watamfaa na wataleta uimara zaidi katika kikosi chake.

“Uongozi unaendelea na usajili na hadi sasa tulipofika ni sehemu nzuri, ubora wa wachezaji ambao wamesajiliwa tayari utaongeza ushindani kikosini lakini utatupa uhakika wa kufanya vizuri zaidi,” amesema.

Hadi sasa, Simba imewatambulisha wachezaji wapya watatu, ikianza na mshambuliaji Willy Onana raia wa Cameroon, winga wa Ivory Coast, Kramo Aubini na Malone (Cameroon), aliyetambulishwa jana, huku ikiwa imebakiza wachezaji wasiozidi wanne kufunga hesabu.

Nyota wapya hao wamepishana na Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Mohamed Oattara, Joash Onyango, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Ismael Sawadogo, Agustine Okrah, Nelson Okwa na Victor Akpan waliopewa ‘Thank You’.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Simba, Azam FC imeondoka nchini juzi kwenda Tunisia itakakoweka kambi yake ya maandalizi ya msimu mpya.

Ofisa Habari wa Azam FC, Hashim Ibwe amesema malengo ya msimu yanaanza sasa, wakiwa na nia ya mataji.

SOMA NA HII  YANGA WAIPIGA KIJEMBE SIMBA KISA VIKAO VYA USIKU.... KAMWE AFUNGUKA HAYA

1 COMMENT