Home Habari za michezo SIMBA, YANGA HAWATAKI UTANI KWA MASHABIKI WAO

SIMBA, YANGA HAWATAKI UTANI KWA MASHABIKI WAO

KLABU za Simba na Yanga hivi karibuni zimeingia makubaliano maalumu na Benki ya NMB kwa ajili ya kusajili wanachama na mashabiki wa klabu hizo zenye maskani yake Kariakoo,
Dar es Salaam.

Lengo la ushirikiano huo ni klabu hizo kongwe kutaka kuepuka utegemezi kutoka kwa matajiri na wafadhili wao ili zijiendeshe kupitia nguvu ya wanachama wao ukiachilia mbali umiliki wa hisa kwa timu hizo.

Mafanikio ya klabu yenye malengo makubwa kama Simba na Yanga yanatokana na misingi imara ya uwekezaji uliofanywa ndani yake ikiwemo wafadhili na wanachama ambao ndio
mtaji namba moja.

Pamoja na ukongwe wa klabu hizo mbili lakini timu hizo zimeshindwa kuishi kwenye uhalisia wake na zimekuwa zikiombaomba na wakati mwingine kutembeza bakuli kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.

Ili uwe na kikosi bora lazima usajili wachezaji wazuri wenye ubora, ili ushinde mataji makubwa lazima uwe na kocha bora, vyote hivi ni vigumu kuvitimiza kama klabu haina fedha.

Kwa kutambua hilo ndipo uongozi wa NMB na klabu hizo ukazungumza na kufikia makubaliano ya kusaidiana kusaka wanachama na mashabiki utakaorahisishia timu hizo kuvuna fedha kwa wanachama na mashabiki wao.

KLABU YA SIMBA
Kwa upande wa Simba, ili kupata fedha kutoka kwa wanachama wake wameanzisha akaunti za aina tatu tofauti ambazo ni mwanachama au shabiki wa Simba akiifungua itamrahisishia mambo mengi kwa wakati mmoja tofauti na ilivyokuwa awali.

Akaunti ya kwanza ni Simba Akaunti ambayo mwanachama au shabiki wa Simba kulipia malipo yake ya uanachama ya kila mwezi kwa urahisi na kwa wakati kila inapofika muda wa kulipia.

Mbali na hapo pia kadi hiyo itakayokuwa na rangi za timu hiyo zitamsaidia kufanya miamala ya kifedha kama ilivyo kadi za kawaida. Akaunti ya pili ni Simba Queens, hii ni akaunti ya
kwanza kuanzishwa na benki hiyo na ndio benki pekee kuwa na akaunti ya wanawake nchini, kama ilivyokuwa Simba Akaunti.

Akaunti hiyo pia inamsaidia mwanachama kulipa malipo yake ya uanachama kirahisi na kwa wakati pamoja na kupata huduma nyingine za kifedha kirahisi zaidi. Akaunti ya tatu ni Watoto Simba Akaunti, hii inawahusu watoto kuanzia miaka mitano hadi 18, na ada ya kufungua akaunti hii ni Sh 5,000 pekee.

YOUNG AFRICANS
Upande wa Yanga, makubaliano yao na benki hiyo ni kuanzisha kadi maalumu kwa ajili ya
wanachama wa timu hiyo, ambazo pia zitawasiadia katika huduma zingine za kibenki.

Yanga imeamua kuitumia benki hiyo kwa kuwa ina matawi mengi hapa nchini na kufanya kujisajili kuwa rahisi na kwa gharama nafuu.

Hii ni fursa nzuri ambayo wanachama na mashabiki wa klabu hizo mbili wanapaswa kuichangamkia na kama kweli wanataka timu zao zitoe ushindani kwenye mashindano ya Caf ikiwezekana zibebe ubingwa wa Afrika, hawana budi kuimarisha misuli yao ya kifedha ili kusajili wachezaji wenye viwango vinavyoendana na ukubwa wa mashindano.

Hiki ni kipindi cha usajili, ndio muda ambao timu hukitumia kujiimarisha kuelekea msimu unaofuata kwa klabu za Simba na Yanga zinapaswa kuwa na fungu kubwa la fedha kwa ajili ya kusajili wachezaji wenye ubora ili kumudu ushindani.

Inawezekana kwa Tanzania hili likawa geni, lakini ni utaratibu wa kawaida kwa timu zinazoendeshwa na wanachama na zimekuwa zikifanikiwa kutokana na harambee ya michango kutoka kwa mashabiki wake.

Timu kama Barcelona, Real Madrid na nyinginezo zimekuwa zinaendeshwa kwa kutegemea ada ya wanachama wake kupitia ada ya mwezi, ambayo wamekuwa wakilipa kupitia utaratibu maalumu uliowekwa na uongozi wa klabu.

Mfano ada ya mwanachama kwa mwezi kwenye klabu ya Yanga au Simba ni Sh 2,000, hivyo kwa mwaka ni Sh 24,000 na kama klabu ina wanachama milioni 5, basi kwa mwaka itapata Sh bilioni 120.

Fedha hizo zinaweza kuzisaidia klabu hizo katika usajili wa wachezaji na mambo mengine, na ukichangia na feha kutoka vyanzo vingine, timu hizo zitakuwa matajiri wakubwa.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Iman Kajula anasema wanajivunia kuungana na benki hiyo sababu huduma zao zinapatikana kwa urahisi na hiyo itawasaidia kukufanya kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa wanachama wao ambao bado wanajukumu la kuichangia timu yao ili
kupata furaha.

Kauli yake inaungwa mkono na Rais wa Yanga, Hersi Saidi ambaye anasema tangu mchakato huo uanze Julai 10, mwaka huu wameona manufaa makubwa ikiwemo idadi ya wanachama kuongezeka na makadirio yao ni kukusanya wanachama zaidi ya milioni nane katika kipindi cha miaka miwili ya mkataba wao.

“Simba na Yanga ni klabu kubwa nchini ndio maana tukaamua kufanya nazo kazi
tukiamini zinaweza kufikia malengo kwa ukubwa wao na uzuri benki yetu inafika kila kona ya Tanzania kama ilivyo umaarufu wa timu hizo,” anasema Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na
Biashara wa NMB, Filbert Mponzi.

SOMA NA HII  BAADA YA KUITUNGUA TENA YANGA SC...SOPU NAYE ALIAMSHA KWA DIARRA...