Home news GAMONDI ATAMBA, AWEKA WAZI REKODI YAKE HII MPYA LIGI YA MABIGWA

GAMONDI ATAMBA, AWEKA WAZI REKODI YAKE HII MPYA LIGI YA MABIGWA

Habari za Yanga leo

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amefichua kuwa, anafahamu timu hiyo ina rekodi mbaya kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kushindwa kucheza hatua ya makundi kwa zaidi ya miaka 20 sasa, hivyo amejiandaa kuandika rekodi mpya.

Yanga Septemba 16, mwaka huu, wanatarajiwa kushuka ugenini nchini Rwanda kuvaana na Al Merreikh ya Sudan katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kuelekea mchezo huo, kikosi cha Yanga kinajivunia kasi yao ambapo hatua ya awali waliiondosha ASAS kutokea nchini Djibouti kwa jumla ya mabao 7-1, huku pia wakiwa na mwenendo bora kwenye Ligi Kuu Bara ambapo wanaongoza msimamo na pointi zao sita walizokusanya kwenye michezo miwili ya kwanza, wakifunga mabao kumi, hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa.

Msimu uliopita, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, kwenye mashindano ya kimataifa walianzia Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo walitolewa hatua ya mtoano na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika ambapo walifanikiwa kumaliza washindi wa pili.

Akizungumza na Spoti Xtra, Gamondi alisema: “Kikosi kinaendelea na maandalizi ya mwisho ya michezo hii ya hatua ya mtoano, nafahamu msimu uliopita tuliondolewa katika hatua kama hii na timu kutoka Sudani, najua kuna zaidi ya miaka 20 timu haijacheza hatua ya makundi, hivyo tunafahamu ugumu na umuhimu wa michezo hii.

“Tumejipanga kuwa na rekodi na historia mpya msimu huu, malengo yetu ni kuhakikisha tunafuzu makundi na kufika mbali zaidi kwani tunaamini kwenye ubora wa kikosi tulichonacho.”

Katika maandalizi yao kuelekea mchezo huo, jana asubuhi kikosi cha Yanga kilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Kiluvya FC inayoshiriki First League na kushinda mabao 6-0 kwenye Uwanja wa Avic Town, Kigamboni, Dar.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHO NA MAMELOD.....AUCHO MDOGO MDOGO AANZA KUZIPANGA GIA