Home Habari za michezo HII SASA KALI SIMBA YACHUKUA POINTI TATU NJE YA UWANJA

HII SASA KALI SIMBA YACHUKUA POINTI TATU NJE YA UWANJA

Habari za Simba leo

Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye ni Kocha Mkuu wa Simba, mapema tu amezinasa mbinu za Power Dynamos ya Zambia jambo linaloashiria kwamba tayari amewamaliza wapinzani wake hao nje ya uwanja.

Kocha huyo ambaye ana kazi ya kuiondosha Power Dynamos katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutinga hatua ya makundi kunako michuano hiyo, amesema wapinzani wao hao ni moja ya timu inayocheza kwa kujilinda pamoja na kushambulia kwa kushtukiza jambo ambalo amelifanyia kazi.

Agosti 6, Mwaka huu, timu hizo zilicheza mechi tya kirafiki kwenye Tamasha la Simba Day, ambapo ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 2-0 Power Dynamos.

Kikosi cha Simba kimeelekea Ndola nchini Zambia kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya Power Dynamos unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ya Septemba 16, mwaka huu, kisha marudiano Oktoba Mosi, 2023, Dar. Mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Robertinho amelisema kuwa: “Tunakabaliana na wapinzani ambao wanabadilika kulingana na aina ya mchezo, hivyo tupo tayari kuwakabili kwa kuwa wanacheza kwa kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza, hilo tunalitambua.

“Wachezaji wanazidi kuimarika na kila wakati makosa tunayafanyia kazi hasa kwenye eneo la kufunga ambalo ni muhimu. Kikubwa ni kujituma na kufanya vizuri kwani Simba ni timu kubwa.”

KIKAO CHAFANYIKA Kabla ya kikosi cha Simba hakijaondoka Dar, Robertinho alifanya kikao na wachezaji wa timu hiyo, huku kubwa zaidi amewasisitiza kurudi na ushindi, ikishindikana, wapate sare.

“Katika mashindano hayo ya kimataifa, kila timu inatakiwa kupata ushindi nyumbani kwake, na ugenini unahitaji sare yoyote itakayokuweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuatia.

“Hivyo nimefanya kikao na wachezaji wangu na kuwasisitizia kupambana katika michezo ya ugenini, kikubwa hatutakiwi kufungwa zaidi ya sisi ushindi kama tukikosa, basi tupate sare,” alisema Robertinho.

PHIRI, CHAMA WAIBEBA SHOO Wakati huohuo, nyota wawili wa Simba raia wa Zambia, Clatous Chama na Moses Phiri, wamepania kwelikweli kuisaidia timu yao kupata ushindi ugenini kabla ya kurudi nyumbani kumaliza kazi ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza nasi, Phiri alisema: “Nafahamu kuwa tunakwenda kukutana na ndugu zetu kutoka taifa letu, hii sio sababu ya sisi kushindwa kupambana kwa kuwa kila mtu yupo katika kituo chake cha kazi.

“Tunatakiwa kuhakikisha tunaisaidia timu yetu kufikia malengo yao, sisi tupo tayari kupambana kwa kuwa bahati nzuri tayari tumecheza nao, kwa hiyo inatupa unafuu zaidi.”

SOMA NA HII  KOCHA SIMBA APIGILIA MSUMARI SAKATA LA CHAMA