Home Habari za michezo ISHU YA SIMBA KUSAJILI MAKIPA WENGI YAWEKWA WAZI

ISHU YA SIMBA KUSAJILI MAKIPA WENGI YAWEKWA WAZI

Habari za Simba

Mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba SC wamesema hawana shida yoyote kutokana na uamuzi wao wa kusajili idadi kubwa ya Walinda Lango kwa sababu imeandaa mikakati maalumu itakayohakikisha wachezaji hao wote wanatumika.

Kwa sasa Wekundu wa Msimbazi ina Walinda Lango watano na idadi hiyo kubwa imetokana na mashindano mengi yanayowakabili, ikiamini wote watakaa langoni kuitumikia timu hiyo.

Walinda Lango hao ni pamoja na Aishi Manula, Ally Salim, Hussein Abel, Ayoub Lakred na Ahmed Feruzi, aliyepandishwa kutoka katika timu ya vijana ya umri chini ya miaka 20 (U-20).

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema wamegundua moja kati ya sababu ambazo timu zote kubwa zinafanya vizuri kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa ni kuwa na Walinda Lango wengi ambao ni bora na waliokamilika.

“Siyo dhambi kuwa na Walinda Lango wengi, tunataka tuwe na machaguo mengi, pia msimu huu tuna mashindano mengi kwa hiyo ni lazima tuwe nao wengi tena bora, niwakumbushe tu makipa tulionao si wale wa bora liende ni makipa kweli,” amesema Ahmed.

Ameongeza usajili wa Lakred, ambaye ni raia wa Morocco ulitokana na Mbrazil, Luis Jefferson kuumia na Hussein alichukuliwa kwa ajili ya kuziba nafasi ya Beno Kakolanya.

Kuhusu maandalizi ya mechi ya michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos, Ahmed amesema mazoezi yanakwenda vizuri na bado timu yao itaendelea kucheza michezo ya kirafiki.

“Hizi tulizocheza ni mechi mazoezi, lakini tutakuwa na mechi zenyewe za kirafiki, ukisikia mechi ya kirafiki ni ile ambayo mwalimu anatakiwa kuona ni jinsi gani Vijana wake wamemwelewa na wanatakiwa kucheza bila presha, ndiyo msingi wa mechi za kirafiki, amesema meneja huyo.

SOMA NA HII  BAADA YA 'KUFOKEWA' NA MO DEWJI KISA KUMSIFIA MANARA, CHAMA AVUNJA UKIMYA...