Home Habari za michezo SIMBA, YANGA NI REKORI NA HESHIMA…… DAKIKA HIZI KUAMUA HUKUMU HII

SIMBA, YANGA NI REKORI NA HESHIMA…… DAKIKA HIZI KUAMUA HUKUMU HII

Habari za michezo

Vikosi vya Simba na Yanga zinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi za marudiano za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kila moja kutoka kupata ushindi kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, huku makocha wa timu hizo wakikabiliwa na dakika 180 za kujenga heshima na kuweka rekodi kya kutimiza malengo ya klabu hizo.

Yanga imetoka kupata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Namungo na wikiendi ijayo itaikaribisha Al Merrikh ya Sudan iliyoifumua Kigali kwa mabao 2-0, wakati Simba imetoka kuinyoosha Coastal Union kwa mabao 3-0 siku chache tangu ilipopata sare ya 2-2 ugenini kwenye mechi za CAF kwa Power Dynamos ya Zambia ambao wanarudiana nao Oktoba Mosi kwenye Uwanja wa Azam Comples, Dar es Salaam.

Makocha Miguel Gamondi na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wana mtihani wa kutakiwa kuziweka timu zao katika nafasi nzuri kutimiza malengo yao msimu huu, ingawa wanapaswa kujipanga vilivyo kutokana na aina ya timu watakazokabiliana nazo na ugumu wa ratiba zao.

Timu hizo kila moja italazimika kucheza mechi mbili za mashindano tofauti ndani ya siku tano katika miji na viwanja tofauti nchini.

Kocha Gamondi wa Yanga, Jumamosi ijayo ataiongoza timu hiyo katika mchezo dhidi ya Al Merrikh katika Uwanja wa Azam Complex, kisha baada ya hapo, Oktoba 4 atakuwa ugenini kukabiliana na Ihefu katika Uwanja wa Highland Estates, uliopo Mbalali mkoani Mbeya.

Mchezo ya Al Merrikh hauonekani kama utampa presha kubwa Gamondi, kwani timu yake inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili iweze kusongambele na kuingia hatua ya makundi ya mashindano hayo ambayo haijacheza kwa miaka 25 tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 1998. Ikipenya hapo kwake itakuwa rekodi kuiingiza Yanga makundi tangu 1998, lakini mtihani mgumu ni mchezo wa ligi dhidi ya Ihefu, siku nne baadaye utakaochezwa Uwanja wa Highland Estates huko na hii ni kwa sababu kuu mbili.

Sababu ya kwanza ni muda mfupi ambao timu itaupata kujiandaa baada ya kumalizana na Al Merrikh, huku ikilazimika pia kusafiri,lakini sababu ya pili ni kumbukumbu ya ugumu wa michezo baina yao na Ihefu ambayo msimu uliopita iliwatibulia rekodi ya kucheza mechi 49 bilaa kupoteza.

Ihefu ilitibua rekodi hiyo Novemba mwaka jana kwa kuifunga mabao 2-1 katika uwanja huohuo ambao mechi ya Oktoba 4 itachezwa. Upana wa kikosi, unaweza kuwa silaha nzuri kwa Gamondi kuvuna matokeo mazuri katika michezo hiyo ambayo hapana shaka ushindi utaziweka vyema hesabu zao msimu huu.

Gamondi alisema kwa sasa hesabu na mipango yake amezielekeza katika mchezo dhidi ya Al Merrikh.

“Mchezo ulio mbele yetu ni dhidi ya Al Merrikh. Tayari tumepata ushindi wa mabao 2-0 ugeni i lakini huu ni mpira wa miguu tunapaswa kuuheshimu na kujipanga vizuri katika mechi ya marudiano ili tuweze kufanya vizuri,” alisema Gamondi.

Kwa upande wa kocha Robertinho wa Simba, ana mtihani mgumu kidogo katika mechi mbili mbele yake na ikiwa ataushinda hapana shaka timu yake itaenda katika mechi ya ufunguzi wa mashindano ya African Football League ikiwa katika hali nzuri ya kisaikolojia.

Dakika 90 za kwanza ngumu kwa Robertinho ni zile za mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ambayo Simba itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi ikihitaji ushindi ili iweze kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 ugenini, Zambia wiki iliyopita.

Ukiondoa matokeo ya kwanza baina ya timu hizo, jambo lingine ambalo hapana shaka linampa presha Robertinho ni majeraha ya beki tegemeo, Henock Inonga aliyopata katika mechi ya Coastal yanayoweza kumfanya akose mchezo huo wa Wazambia. Ishu ni kwamba Simba haina rekodi tamu Chamazi.

Lakini baada ya mechi hiyo, Simba italazimika kusafiri hadi Mbeya siku nne baadaye itakuwa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Tazania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine itakayochezwa Oktoba 5.

Prisons imekuwa na historia ya kuisumbua Simba inapokuwa nyumbani na kudhihirisha hilo, maafande hao wamepata ushindi katika mechi mbili kati ya tatu walizokutana huko.

Kana kwamba haitoshi, kitendo cha Prisons kutopata ushindi katika mechi tatu zilizopita za ligi dhidi ya Singida Big Stars, Azam na Tabora United kinaweza kuzidi kuongeza ugumu kwa Simba katika mechi hiyo, kwani bila ya shaka wenyeji watalazimika kutumia nguvu kubwa ili kusaka ushindi wa kwanza msimu huu.

Kocha Robertinho alisema kikosi alichonacho kina uwezo wa kufanya vizuri katika mechi hizo zote mbili zilizo mbele yao.

“Ni mechi ngumu lakini kwa sasa tuna kikosi bora ambacho kinaweza kufanya vyema katika mechi hizo zote na nyingine ambazo zitakuja mbele yetu. Jambo zuri ni kuwa sasa timu iko imara na kisaikolojia tuko vizuri hivyo hatuna wasiwasi,” alisema Robertinho.

SOMA NA HII  ROBERTINHO:- SASA HIVI SIMBA INACHEZA SOKA NINALOLITAKA....