Home Habari za michezo HII HAPA MIEZI MIWILI YA UBABE YANGA

HII HAPA MIEZI MIWILI YA UBABE YANGA

Habari za Michezo

Umebaki muda usiozidi wiki moja ili itimie miezi miwili tangu msimu wa soka wa 2022/2023 uanze hapa nchini na tayari umeshuhudia msisimko na mvuto wa aina yake kwa mechi mbalimbali za mashindano ya ndani na yale ya kimataifa kwa klabu za Tanzania.

Yanga walianza msimu wakiwa na kibarua cha kutetea mataji matatu waliyoyapata msimu uliopita ambayo ni Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii huku pia wakiwa na deni la kufanya vyema katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu uliopita kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, walijikuta wakishindwa kutetea Ngao ya Jamii kwa kupoteza mbele ya watani zao Simba kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana katika dakika 90 za mechi ya fainali hiyo iliyochezwa Tanga katika Uwanja wa Mkwakwani, Agosti 13.

Pamoja na kuanza msimu kwa kupoteza Ngao ya Jamii, mambo mengine yanaonekana kutokuwa mabaya kwa Yanga ndani ya kipindi hiki cha miezi miwili na makala hii inakuletea orodha ya mambo yaliyowapa furaha Wanayanga na kuwasahaulisha machungu ya kuporwa taji moja na watani wao.

Moto wa mabao

Msimu uliopita, Yanga licha ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu haikuwa na makali sana ya ufungaji kulinganisha na watani wao Simba ambao walimaliza msimu wakiwa wamepachika mabao mengi kwenye ligi kuzidi wao. Katika Ligi Kuu 2022/2023, Yanga ilifunga mabao 61 ikiwa ni wastani wa mabao 2.03 kwa mchezo wakati Simba ilimaliza msimu ikiwa imepachika mabao 75 ikiwa ni wastani wa mabao 2.5 kwa mchezo.

Hata hivyo katika mechi nne za kwanza za Ligi Kuu msimu huu ambazo Yanga imecheza dhidi ya KMC, JKT Tanzania, Namungo na Ihefu SC, Yanga imefumania nyavu mara 12 sawa na wastani wa mabao matatu kwa mechi.

Jambo linaloipa faraja zaidi Yanga kwamba msimu huu inaweza kufunga idadi kubwa ya mabao ni mgawanyo wake ambapo nyota wake wanane tofauti ndio wameyafunga ambao ni Dickson Job, Mudathir Yahya, Pacome Zouzoua, Aziz Ki, Clement Mzize, Yao Attohoula, Hafidh Konkoni na Maxi Zengeli.

Kukimbiza mitandaoni

Mitandao ya kijamii ni fedha hasa pale unapokuwa na namba kubwa ya wafuasi na watu wanaofuatilia kurasa zako ambapo inaweza kushawishi kampuni na taasisi au hata watu tofauti kuweka fedha ili kutangaza huduma na bidhaa zao.

Katika miezi miwili ya mwanzoni msimu huu, Yanga wanaonekana kuwa katika hali nzuri kwenye kurasa za mitandao ya kijamii kwa kuvutia kundi kubwa la watu kutokana na maudhui mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyaweka.

Kuthibitisha hilo, utafiti uliofanywa na Deporfinanzas, umeitaja Yanga kuwa klabu iliyoongoza Afrika kwa mwezi Agosti kuwa na mwingiliano (interactions) mkubwa katika kurasa zake za kijamii ikiwa na mwingiliano milioni 10.1 huku ikifuatiwa na Simba yenye milioni 9.36.

Kumaliza unyonge Afrika

Kwa miaka 25 Yanga ilikuwa haijawahi kuonja ladha ya hatua ya kutinga katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu iliposhiriki mara ya mwisho 1998 ingawa imewahi kuingia mara kadhaa na hata kwenda juu zaidi ya hapo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, miezi miwili ya hivi karibuni imetosha kuhitimisha unyonge huo baada ya kupenya kwa kishindo katika hatua mbili za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa kuzitupa nje timu za ASAS ya Djibouti na Al Merrikh ya Sudan.

Ilianza kwa kuitoa ASAS katika raundi ya awali kwa kuichapa idadi ya mabao 7-1, ikishinda mabao 2-0 katika mechi ya kwanza na na ile ya marudiano ikaibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1, zote zikichezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Katika hatua iliyofuata ikaifurusha Al Merrikh kwa ushindi wa mabao 3-0, mechi ya kwanza ugenini huko Rwanda ikishinda mabao 2-0 na kisha ikapata ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya marudiano hapa Dar es Salaam.

Jambo la kufurahisha ni namba kubwa ya mashabiki ambao walisafiri na Yanga kwenda Rwanda kuisapoti katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Al Merrikh.

Tuzo Ligi Kuu

Mwanzo mzuri katika Ligi Kuu uliifanya Yanga ianze msimu kwa kunyakua tuzo mbili za mwezi Agosti ambazo ni ile ya mchezaji bora pamoja na ya kocha bora kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Miguel Gamondi alinyakua tuzo ya kocha bora akiwapiku Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wa Simba pamoja na Hemed Suleiman ‘Morocco’ wa Geita Gold wakati upande wa mchezaji bora mshindi alikuwa ni Maxi Nzengeli aliyewapiku Jean Baleke wa Simba na mwenzake wa Yanga, Aziz Ki.

Wenyewe watamba

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe anasema kuwa watahakikisha kile walichokivuna kinaendelea kupatikana katika siku za usoni.

“Miezi hii imekuwa ya kihistoria kwetu kwani tumefanya vizuri nje na ndani ya uwanja. Hii yote ni matokeo ya uongozi bora chini ya Rais wetu Injinia Hersi Said na sapoti kubwa ambayo tunaipata kutoka kwa Wanayanga.

“Malengo yetu ni kufanya vizuri zaidi ili Yanga iendelee kuthibitisha ukubwa wake na kupata mafanikio ambayo kila Mwanayanga anataka kuona tukiyapata,” anasema Kamwe.

SOMA NA HII  KAZE AWAACHIA YANGA UJUMBE HUU