Home Habari za michezo KUNA JOHN BOCCO MMOJA TU, MPENI MAUA YAKE

KUNA JOHN BOCCO MMOJA TU, MPENI MAUA YAKE

Habari za Simba SC

Kuna John Bocco mmoja tu nchini. Jamaa mmoja mrefu, ‘kauzu’ flani mwenye mzuzu kidevuni. Huyu ndiye nahodha wa Simba akitimiza msimu wa saba akiwa na kikosi hicho.

Simba ilimnyakua msimu wa 2017-2018 kutoka Azam FC. Alitua msimu huo akitoka kuitumikia Azam kwa misimu tisa. Ndio, misimu tisa tangu aliposhiriki kuipandisha Ligi Kuu msimu wa 2008-2009.

Yeye ndiye aliyefunga mabao mawili yaliyoipandisha Azam daraja kutoka Ligi ya Taifa kituo cha Dodoma mwaka 2007. Azam ilimnyakua kutoka Cosmopolitan, baada ya kufanya makubwa akifunga mabao kadri atakavyo, licha ya wababe hao wa zamani wa nchi kushindwa kupenya katika mechi ya mwisho iliyopigwa Uwanja wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa.

Achana na mabao 84, aliyoifungia Azam katika misimu tisa aliyoitumikia timu hiyo, lakini Bocco pia alinyakua tuzo ya Mfungaji Bora msimu wa 2011-2012 alipofunga mabao 19.

Mwamba huyo akiwa Azam alikuwa akizivuruga Simba na Yanga akizitungua kila anapokutana nazo iwe kwenye Ligi Kuu Bara, Kombe la Mapinduzi, Ngao ya Jamii au Kombe la Shirikisho (zamani FA), kiasi kwamba mashabiki wa klabu hizo wakaanza kumchukia. Hii ilitokana na kumuona kama straika anayezikomoa timu hizo, lakini mabadiliko yaliyofanyika Azam mwaka 2017, ilisababisha Simba na Yanga kuanza kumvizia.

Yanga ikawa ina kila dalili za kumbeba, lakini Simba inafanikiwa kumbeba na mwamba huyo, akaanza kufanya kazi yake kwa ufanisi. Tangu ajiunge na timu hiyo ikiwa ni misimu saba kwa sasa amekuwa akiendelea kufunga. Yaani anafunga na kufunga tena, hadi anakera.

Cha ajabu hivi karibuni mashabiki wa Simba wasiojua thamani ya nahodha huyo na nyota wa kimataifa wa Tanzania wamemzomea na wachache waliokosa aibu wamediriki kumtupia chupa za maji. Ni kama wameshindwa kuelewa kwanini, Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameamua kumbakisha kikosini, wakati kulikuwa na kila dalili za kupewa ‘Thank You’, lakini mwanaume bado yupo na anaendelea kuwasha moto vilevile licha ya kuanza kupungua kasi.

Misimu minne ya kwanza Bocco akaipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara, baada ya timu hiyo kusota kwa misimu mitano mfululizo bila kubeba taji hilo, lakini naye akanyakua tena kiatu cha Mfungaji Bora akifunga mabao 16 akimpiku jiooni kabisa, nyota mwenzake, Chris Mugalu aliyekuwa anaonekana kubeba tuzo hiyo.

HAINA KULALA

Kama hujui, Bocco ameingia kwenye historia ya soka la Tanzania kuwa kufunga mfululizo ndani ya misimu yake 16 aliyopo kwenye Ligi Kuu Bara. Hii haijawahi kutokea tangu alivyofanya Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyefunga mabao mfululizo kwenye misimu 13 akiwa na timu tano tofauti.

Chinga ndiye aliyekuwa anashikilia rekodi ya Mfungaji Bora wa muda wote kwa kufunga jumla ya mabao 153 katika misimu hiyo 13, ikiwamo ile ya mabao mengi ambaye bado haijavunjwa ya 1998 alipofunga mabao 26.

Hata hivyo, Bocco katikati ya wiki hii, aliifikia rekodi ya mabao 153 baada ya kufunga bao la pili la Simba ilipoizamisha Tanzania Prisons kwa mabao 3-1.

Kidume hicho leo kina nafasi ya kuandika rekodi ambayo inaweza kuja kuwasumbua washambuliaji wengine wajao kama atafunga bao kwenye mechi na Singida Big Stars inayopigwa Uwanja wa Liti, mkoani Singida kuanzia saa 10:00 jioni.

Bao atakalofunga litamfanya Bocco ndiye awe kinara wa muda wote wa ufungaji mabao kwa kumpita Chinga One, anayelingana naye kwa sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti mapema, Bocco aliwahi kukaririwa kwamba, yeye kazi yake ni kufunga na huwa hana jingine analofikiria uwanjani zaidi ya hivyo na hata anaposhindwa kufunga anajisikia vibaya.

Kocha wa Simba, Robert Oliveira ‘Robertinho’ alinukuliwa juzi na gazeti hili akisema anavutiwa na Bocco kwa sababu anazingatia maelekezo anayompa, hivyo ataendelea kumtumia, hata kama mashabiki wa klabu hiyo wanamchukulia poa na kudiriki kumtupia chupa na hata kumzomea bila kujua thamani aliyonayo nyota huyo kwake.

Hapo chini ni mabao na misimu ambayo Bocco amekuwa akifunga ikiwamo misimu aliyokuwa akisumbuliwa na majeraha, lakini hakuacha kufunga kwani kazi yake ni kufunga kama alivyokuwa akifanya Mmachinga nyota wa zamani wa kimataifa ambaye kwa sasa ni kocha.

SOMA NA HII  AZIZI KI AFUNGUKA KILICHOMFELISHA MSIMU ULIOPITA,..... SASA MAMBO NI HIVI