Home Habari za michezo HIVI NDIVYO MAXI ALIVYOMPOTEZA SKUDU KIBABE NDANI YA YANGA…

HIVI NDIVYO MAXI ALIVYOMPOTEZA SKUDU KIBABE NDANI YA YANGA…

Habari za Yanga

Kiungo wa Yanga, Maxi Nzengeli amefanya mapinduzi ndani ya kikosi baada ya kumpindua kama utani Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ ambaye usajili na hata utambulisho wake ulifunika, tofauti na kazi iliyopo uwanjani kwa sasa.

Katika usajili wa Yanga jezi namba 6 ndio iliyobamba na kusubiriwa kwa hamu na kuja kutambulishwa kwa Skudu kutoka Afrika Kusini, lakini winga huyo ameshindwa kuonyesha kilichosubiriwa baada ya Maxi kufanya makubwa akiipa heshima namba 7.

Katika mechi tano ambazo Yanga imeshacheza kwenye Ligi Kuu Bara, Maxi amefunika akizidi kuwakuna mashabiki wa klabu hiyo kwa kazi kubwa aliyoifanya akishirikiana na Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua.

Data zinambeba Maxi, kwani katika dakika 450 za mechi tano za Yanga, staa huyo kacheza dakika 309, amefunga mabao matatu na asisti mbili.

Maxi alicheza dhidi ya KMC dadika 17 (asisti moja), JKT Tanzania dakika 90 akifunga mabao mawili, Ihefu dakika 22, Namungo dakika 90 na Geita Gold dakika 90 akifunga bao moja na asisti moja. Hali ni tofauti kwa Skudu hadi sasa ametumia dakika 57 dhidi ya Ihefu na Jonas Mkude ambaye pia usajili wake ulitikisa kwani tangu atoke Simba kacheza dakika saba pekee dhidi ya JKT Tanzania.

Nyota anayeonekana kumsogelea Maxi ni Aziz KI kwani hadi sasa amefunga mabao tatu na asisti moja, anafuatiwa na Pacome mwenye mabao matatu bila asisti wakipishana kidogo dakika walizotumia uwanjani.

MSIKIE MWENYEWE

Maxi alisema anaendelea kuizoea ligi ya Tanzania akitaka kuvunja rekodi aliyoanza nayo ya kufunga na kuasisti kwa timu hiyo iliyomsajili kutoka AS Maniema ya DR Congo.

Maxi anasema msimu uliopita katika ligi ya DR Congo hadi iliposimama alitengeneza asisti tatu na kufunga manne katika mechi nane Maniema.

“Ninapocheza kama kiungo jukumu langu kubwa ni kuzalisha pasi za mabao hili ndio nataka liwe linatangulia kwangu hizi mbili ni chache sana nataka kutoa pasi za mabao zaidi kuliko kufunga,” alisema Maxi na kufichua kuwa mzuka unaomfanya kufanya makubwa uwanjani ni umati wa mashabiki ambao wapo kila wanakokwenda.

Alisema baada ya kupoteza mechi dhidi ya Ihefu walikubaliana hawatakiwi kurudia kosa kuwaumiza mashabiki wao ambao wanawaamini.

“Hapa watu wanapenda sana mpira, kila unapokwenda unakutana na mashabiki wengi. Tena, sisi tunasafiri na ndege lakini wako mashabiki wengine wanasafiri kwa umbali mrefu kwa mabasi. Hawa ndio wanatufanya tuongeze juhudi uwanjani,” alisema.

SOMA NA HII  MBRAZILI ATOA AHADI YA KIBABE SIMBA....MASHABIKI WAPAGAWA KINOMA...