Home Habari za michezo MASHABIKI SIMBA WACHARUKA, KWANINI PHIRI?

MASHABIKI SIMBA WACHARUKA, KWANINI PHIRI?

Habari za Simba

Licha ya Kocha wa Simba, Robertinho kusisitiza kila mechi ina mpango wake, mashabiki wa klabu hiyo wamecharuka. Wamechachamaa wakihoji kila kona; “Kwanini Moses Phiri haanzi?”

Tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii hususani ile rasmi ya Simba ni kwamba kila kinapopostiwa kitu chochote hata kama hakihusiani na mechi mashabiki wamekuwa wakitiririka kwa wingi kuhoji hatma ya Phiri huku wakitaka aanze kuaminiwa na Kocha.

Mashabiki hao wamekuwa wakipiga presha wakishinikiza hata kwenye mechi ya leo dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Mkapa aanzishwe kwa madai kwamba kwa ana uwezo mkubwa kuliko wachezaji wanaoanzishwa na timu inahaha kupata matokeo chanya.

Lakini huku hayo yakiendelea habari mpya ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba staa huyo aliyetumika dakika 112 akifunga mabao mawili msimu huu, ameomba kuondoka kwenye dirisha dogo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema sababu kubwa ni kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

Staa huyo ambaye alisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Zanaco ya nchini kwao huu ni msimu wa mwisho kwake na hakuna dalili ya kuendelea kuwepo licha ya kupendwa na mashabiki wa timu hiyo wanaoshinikiza achezeshwe.

Msimu huu, nyota huyo amecheza michezo minne tu kati ya mitano ya Ligi Kuu Bara akianza na Mtibwa Sugar ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-2, huku yeye akicheza dakika 23, mechi iliyopigwa Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Baada ya hapo alicheza dakika 38,dhidi ya Dodoma Jiji akifunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 ingawa dhidi ya Coastal Union hakupata nafasi huku mechi na Tanzania Prisons akiingizwa dakika za mwishoni.

Mchezo uliofuata na Singida alicheza dakika 44 tu huku akifunga bao moja lililoiwezesha timu hiyo kuibuka na ushinda mabao 2-1 hivyo kuifanya kutopoteza mchezo wowote kati ya mitano ya Ligi Kuu Bara iliyocheza hadi sasa.

Habari za uhakika ni kwamba Phiri hana furaha ndani ya Simba na amekuwa akiwaambia mpaka marafiki zake wa karibu, hivyo ameomba kuondoka dirisha dogo litakapofunguliwa Desemba 16 ili akatafute changamoto sehemu nyingine.

“Ameomba kuondoka kutokana na viongozi na benchi la ufundi kukiuka makubaliano yao waliyoingia ya kuhakikisha anacheza baada ya kupona yale majeraha ingawa imekuwa ni tofauti kwani wamekuwa wakipewa wengine nafasi ya kucheza,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Amekuwa akiingizwa dakika zikiwa zimemalizika na muda mwingine kushindwa kugusa hata mpira mara baada ya kupewa hiyo nafasi, hilo limemfanya ajisikie vibaya na kuomba kwenda kujaribu maisha mengine nje ya Simba.”

Mwanaspoti lilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ ili kuzungumzia suala hilo simu yake iliita bila kupokelewa kwa saa kadhaa.

Lakini Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally alisema: “Phiri ni mchezaji wa Simba na bado ana mkataba na endapo anataka kuondoka kwa sasa hawezi maana hakuna dirisha ambalo liko wazi hivyo ataendelea kuitumikia Simba kwa mujibu wa vipengele vya mkataba wake alioingia na klabu.”

KAULI ZA WADAU

Kocha wa zamani wa Biashara United na Kagera Sugar, Francis Baraza alisema Phiri ni mchezaji mzuri na anatakiwa kupewa heshima yake ndani ya timu hiyo kutokana na kufanya mambo makubwa na kama wangempa nafasi angeisaidia sana safu yao ya ushambuliaji.

“Mchezaji ambaye amefanya vizuri msimu wake wa kwanza walitakiwa kumpa uzito kikosini kwa kumpa nafasi ya kucheza, licha ya kutoka majeruhi ila ameendelea kuonyesha kiwango bora ambacho naamini bado ana uwezo kwa washambuliaji waliopo.”

Staa wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa, alisema anachokiona; “Simba ina kikosi kizuri sana, huenda ikawa timu ambayo itatisha zaidi na kufunga mabao mengi, ninachokiona ni kocha kujua jinsi ya kumtumia kila mchezaji kwa faida yake na kikosi kizima kwa ujumla, nina imani na Phiri ya kufanya vizuri.”

MECHI YA IHEFU LEO

“Mpango wa Ihefu ni tofauti na ule tulioingia nao dhidi ya Al Ahly. Mfano kuna wachezaji walioonyesha ubora mkubwa kwenye mechi zilizopita lakini pia kuna wengine hawakucheza ila sio kwamba ni wagonjwa, hapana ila ni mpango hivyo dhidi ya Ihefu tunaweza kuwashangaza wengi,” alisema Robertinho ambaye amekuwa akikwepa kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja ndani ya kikosi cha timu hiyo.

Licha ya kushindwa kuweka bayana ni sapraizi gani ambayo Simba inaiandaa dhidi ya Ihefu, Mwanaspoti limepenyezewa ni mabadiliko ya kikosi ambapo baadhi ya mastaa huenda wakapumzishwa na kuweka wengine ambao wamekuwa hawajapata muda wa kutosha kucheza kikosini hapo.

Washambuliaji Moses Phiri na Luis Miquissone sambamba na mabeki wa pembeni, Israel Mwenda na David Kameta ‘Duchu’ ni miongoni mwa mastaa wa Simba wanaotarajiwa kucheza mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

PHIRI WA MSIMU ULIOPITA

Phiri alijiunga Simba, Juni mwaka jana kwa mkataba wa miaka miwili, alionyesha kiwango kizuri kilichomfanya kushika nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao 14 nyuma ya Ricky Banda wa Red Arrows FC aliyemaliza na 16.

Msimu wa 2020/2021 akiwa na kikosi hicho cha Zanaco ndipo ambapo alionyesha uwezo mkubwa ambapo aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu nchini Zambia baada ya kufunga jumla ya mabao 17 na kuiwezesha timu hiyo kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nyota huyo wa Zambia msimu wake wa kwanza nchini ila alifunga mabao 10 ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita sambamba na John Bocco huku akiwa nyuma ya mchezaji mwenzao na mfungaji bora Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ aliyefunga 17.

Licha ya ugeni kwenye Ligi na kutumia muda mrefu akiwa majeruhi, Phiri alifunga mabao 10 katika ligi na mengine matano katika mechi 10 za Ligi ya Mabingwa Afrika alizocheza ambako pia alitoa asisti mbili. Soma zaidi maoni ya mashabiki kwenye ukurasa wa 17.

SOMA NA HII  MSERBIA WA YANGA APEWA MAJUKUMU MAZITO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here