Home Habari za michezo PAMOJA NA KUSAJILIWA KWA MBWEMBWE ZA DUNIA…ONANA NA KONKON BADO SANA….

PAMOJA NA KUSAJILIWA KWA MBWEMBWE ZA DUNIA…ONANA NA KONKON BADO SANA….

Habari za Michezo

Mshambuliaji Willy Onana wa Simba na Hafidh Konkon wa Yanga wameshtua kutokana na muenendo wao wa kusuasua katika timu zao licha ya kuwa na rekodi nzuri walipotoka.

Onana amesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Rayon Sports (Rwanda) huku Konkon yeye akitokea Bechem United (Ghana).

Onana akiwa Rwanda na kikosi cha Rayon alifunga mabao 16 na kuwa kinara wa wafungaji huku Konkon yeye akiwa na Bechem alifunga mabao 15 katika mechi 26 alizocheza na kuwa nyuma kwa mabao matatu ambayo kinara Abednego Tetteh (18) alimaliza nayo.

Msimu huu wawili hao wote kwa pamoja wamefunga bao moja kila mmoja na wamekuwa wakipata dakika chache za kucheza.

Onana amecheza jumla ya dakika 108 katika mechi tano, alicheza dakika 45 dhidi ya Mtibwa Sugar (Alifunga), dakika 52 na Dodoma Jiji, dakika 10 na Coastal Union, dakika moja na Prisons huku mchezo dhidi ya Singida hakucheza.

Mshambuliaji huyu ameshindwa kufua dafu kwa Jean Baleke ambaye amefunga mabao matano kwenye Ligi Kuu hadi sasa hali ambayo inamfanya akose nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

Upande wa Kon Kon amecheza dakika 205 huku akicheza mechi nne kati ya sita, alitumia dakika 26 mechi na KMC (Alifunga), JKT Tanzania dakika 59, Geita Gold dakika 31 na Azam dakika 1.

Kon Kon kwenye eneo lake kuna vita ya namba dhidi ya Aziz Ki aliyefunga mabao sita.

Wadau mbalimbali wamezungumzia juu ya muenendo wa wachezaji hao tangu waliposajiliwa msimu huu.

Beki wa zamani Simba, Boniface Pawasa amesema anasikitika kuona mshambuliaji Onana anashindwa kuonyesha kitu kwenye timu yake baada ya kuchezeshwa katika eneo ambalo hajalizoea.

Pawasa alisema huenda kocha (Robertinho) bado hajajua namna gani ya kumtumia staa huyo hivyo ni jukumu lake kuongea nae na kumsikiliza kwa manufaa.

“Onana nafasi anayotumika nadhani ni changamoto kwake, huku anacheza kama winga huko alikuwa mshambuliaji inaweza kumfanya ashindwe kufanya vizuri, hili ni jambo la kawaida kwa mchezaji mwingine unaweza kumuamisha namba muda wowote ule akaweza kuendana nayo;

“Kocha amuulize vizuri Onana ni sehemu gani ambayo anaimudu kucheza ni mchezaji mzuri sana huyu, nakumbuka Chikwende alikuwa mzuri lakini hakuweza kufanya vizuri akaondoka namuomba ajiongeze aweze kuendana na kasi ya timu, bila hivyo hatoweza kukaa maana kumvumilia hawatoweza,”alisema Pawasa.

Upande wa beki wa zamani Simba, Fikiri Magoso alisema hadi sasa kuna wachezaji wengi hawajapata nafasi ya kucheza licha ya Onana kucheza dakika chache hivyo inabidi subila itumie kwake.

“Onana ni mchezaji mzuri na anahitaji nafasi ya kucheza zaidi, kucheza akiwa kama winga badala ya mshambuliaji muda mwingine ni mifumo ya kocha,”alisema Magoso.

Mshambuliaji wa zamani Yanga, Hery Morris alisema Konkon amechelewa kuonyesha makeke yake kutokana na kushindwa kuendana haraka na mazingira ya Ligi hapa nchini.

“Bado hajaelewa Ligi ipo vipi na angeelewa na kukopi haraka kama ilivyo kwa Max (Zengeli) ingekuwa ni kawaida kufanya vizuri;

“Kikubwa afanye vizuri mazoezini, ukiwa hauonyeshi ni ngumu kupewa dakika nyingi ndani ya uwanja, kuna muda ukipewa hata dakika 10 tu ukafanya vizuri basi mechi ijayo unapewa dakika nyingi zaidi.”

SOMA NA HII  KUSANYA USHINDI KWENYE MGODI WA ALMASI