Home Habari za michezo DABI YA KARIAKOO UNAAMBIWA IMEANZA NJE YA UWANJA HAPA GAMONDI PALE ROBERTINHO

DABI YA KARIAKOO UNAAMBIWA IMEANZA NJE YA UWANJA HAPA GAMONDI PALE ROBERTINHO

Yanga SC na Simba SC

Jumapili ya Novemba 05 mwaka 2023 mishale ya saa 11 jioni, Miamba ya Soka la Bongo (Simba SC na Young Africans) itakwenda kukutana kwa mara ya kwanza msimu huu 2023/24, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzaniua Bara ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.

Mpaka sasa miamba hiyo yenye historia nzito katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati inalingana alama kwenye msimamo wa Ligi kuu Tanzania Bara, huku ikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, lakini makocha wa timu hizo, Miguel Angel Gamondi na Roberto Oliveira ‘Robertihno’ wamechimbana mkwara mzito kwa kusisitiza ni mchezo mkubwa na ngumu lakini alama tatu zipo kama kawaida.

Ingawa Simba SC wako nyuma kwa mchezo mmoja, rekodi zinaonyesha mara ya mwisho watani hao kukutana Simba SC iliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-0, lakini mapema wakati wa ufunguzi wa msimu huu 2023/24 timu hizo zilikutana kwenye Fainali ya Ngao ya Jamii na Simba SC kushinda tena kwa mikwaju ya Penati 3-1 na kuchukua taji hilo lililokuwa linashikiliwa na Young Africans kwa misimu miwili mfululizo.

Kocha wa Simba SC, Robertinho maarufu kama Mtaalam wa soka la malengo ‘Objective Football’, amesema anatambua ubora wa wachezaji wa Young Africans kwani ni miongoni timu bora na yenye ushindani hasa kwenye ligi, lakini kikois chake kitakwenda kwenye mchezo huo kwa ubora mkubwa.

Kocha Robertinho ambaye ni raia wa Brazili mwenye uzoefu na soka la Bara la Afrika, amesema endapo wachezaji wake watacheza kwa ubora kama ambavyo walicheza mchezo wa Mkondo wa Pili wa African Football League dhidi ya Mabingwa wa Soka wa Bara la Afrika Al Ahly ya Misri, hana presha kwani ushindi utakuwa upande wao.

Kocha huyo ambaye timu yake haijapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu msimu huu, amesema kikosi chake kwa sasa kimeiva akiwa na wachezaji wanaoweza kuanza na kutengeneza ushindi, pia akiwa na wale ambao wanaweza kuja kuingia na kubadilisha mchezo.

“Young Africans wana timu bora lazima uwaheshimu wapinzani wako, ila napata matumaini makubwa zaidi kwani nina wachezaji wenye uzoefu mkubwa, kitu ambacho tutatakiwa kukifanya ni kurudi kucheza kwa ubora kama ambavyo tulicheza kule Misri dhidi ya Al Ahly” amesema Robertinho ambaye aliwahi kuifunga Young Africans akiwa na Vipers ya Uganda.

“Tunatakiwa kutumia nafasi zetu tutakazozitengeneza, mchezo mkubwa kama huu wa watani hautakuwa na nafasi nyingi sana, lakini kitu kizuri kwa sasa tuna wachezaji ambao wanaweza kuanza na kutengeneza ushindi, pia wapo ambao wanaweza kuingia na kubadilisha mchezo, jambo ambalo tumeshafanya huko nyuma.”

Wakati Robertinho akisema hayo, Kocha wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi ambaye ni Muargentina amnesema wanakwenda kumalizia maandalizi yao ya mchezo mkubwa ambao uko mbele yao akijua wapinzani wao walimpokonya taji la Ngao ya Jamii.

Amesema ugumu wa mchezo huo utaamuliwa na ubora wa wachezaji jambo ambalo halimpi presha kwani ana uhakika na kikosi alichonacho kipo tayari kwa mchezo huo mkubwa mkubwa na wachezaji wake wamepania kufanya kila kinachowezekana kupata pointi.

“li uwe bora unatakiwa kushinda michezo mikubwa na midogo kubwa na ndogo na huo ni mwendelezo kwani wachezaji wangu wana huo uwezo,” amesema Gamondi ambaye licha ya kutokuwa na Mshambuliaji tegemeo staili yake ya uchezaji imekuwa ikiruhusu kila mchezaji kufunga.

“Simba SC nawajua nimewaona wakicheza na nimekutana nao pia ila mchezo huu utakuwa tofauti kutokana na ugumu wake,” amesema Gamondi ambaye ameipeleka Young Africans kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya miaka 25 kupita.

“Naamini tutafanya vizuri, tunawaheshimu wapinzani wetu kwani wana wachezaji wenye uzoefu ila timu itakayocheza kwa ubora ndio itakayoshinda, mashabiki wetu waje uwanjani kutekeleza wajibu wao wa kuwapa nguvu wachezaji, sisi tuna timu bora na tunaamini tunaweza kuibuka na ushindi kwenye mchezo huu kama kila mmoja atafanya majukumu yake ipasavyo.”

Dabi hiyo ambayo Simba ndio mwenyeji itachezwa kwenye Uwanja wa Mkapa baada ya uwanja huo kufanyiwa marekebisho makubwa, mchezo ukitarajiwa kuanza mishale ya 11:00 jioni.

SOMA NA HII  WANASIMBA WANAMTAKA MWAMBA HUYU ARUDI MSIMBAZI